How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Friday, 18 August 2017

Mlevi ataka ashirikishwe mazungumzo ya makinikia

            Siku zinazidi kuyoyoma; bila walevi kujua kinachoendelea kwenye mazungumzo ya kubana watasha watupe uchache wetu wa makanikia tokana na kukosekana kwa umakini kwa watawala waliopita kiasi cha kuruhusu tupigwe na kuliwa mbele na nyuma. Hivyo, tokana na ukimya na usiri ulioghubika mazungumzo haya, Mlevi nimeamua kutaka nishirikishwe kwenye mazungumzo haya tokana na sababu zifuazo:
            Mosi, mimi ni raia wa kaya hii tena mzalendo wa kupigiwa mfano. Sina makando kando kama vile unyakuzi wa ardhi au mali kiasi cha kuhitaji kulindwa na munene nisipelekwe lupango kama wale waliokosa umakini wakaruhusu makinikia na madini kuibiwa kwa miongi zaidi ya miwili. Anayebishia hili atoe ushahidi kuonyesha vinginevyo nimuumbue. Najua wengi watanipinga kwa kusema mie ni mlevi. Kweli nalewa na kuangusha gari. Hata hivyo, siangushi kaya kama washenzi, wazembe na mafisadi waliokosa umakini kiasi cha kuruhusu wapigaji watuibie kwa zaidi ya miaka 20 bila kujali kuwa haya matrilioni waliyoruhusu yaporwe kwa kupewa bakshish na rushwa za peremende yangeondoa kaya yetu kwenye umaskini na uombaomba usio na ulazima.
            Pili, mimi ni mtaalamu bobezi wa masuala ya utatuzi wa migogoro yaani Conflict Resolution. Nina shahada tatu katika fani hii ambazo nilizipata ughaibuni bila kughushi wala kutumia vyeti vya wengine. Japo huwa sijisifu, nimewahi kuitwa hata majuu kuwapa shule juu ya mgogoro wa nyuklia unaoendelea baina ya kaya za magharibi na dogo Kim Jogging Un. Hata kwa jamaa zetu kwenye kaya ya man eats man wameishanitumia mwaliko kwenda kuwasaidia kwenye mkwamo uliotokana na uchakachuaji uliopita. Soma taratibu. Kwani hii ni top secret kama mazungumzo ya makinikia.
            Tatu, mimi nimesomea, kuoa na kuishi majuu. Hivyo, nawajua watasha vilivyo; nao wananijua na kuniheshimia. Siwapapatikii wala kuwagwaya kama jamaa zangu walioachia kila kitu wazi kaya ikabakwa wakaliwa kwa miaka 20 na ushehe. Nakumbuka; hata thesis yangu ya PhD ilikuwa How to Mitigate; and Deconstruct the Causalities of Resource-Based Conflict in Uswekeni Countries: The New Scientific Approach of Doing Away with Protoctracted Conflicts and Rip off-sitatafsiri kwa vile nitaharibu utamu. Kama hutaelewa basi ujue unahitaji kurejea shule lau uwe makali ujuzi na ujuaji wako. Hivyo wanaodhani mimi ni kihiyo au kibashite washindwe na kunyong’onyea. Kwa taarifa yenu, kama siyo kubanwa na masharti ya shahada hii ya uzamivu ya kuandika kurasa zisizopungua 500, nilipanga kuandika kurasa 5,000 ili kuweka rekodi ya kuwa daktari mwenye andiko kubwa kuliko yote ulimwenguni.
            Nne, mbali na kuwa mtaalamizi wa mambo ya usuluhishi migogoro, ni mwanasheria bobezi mwenye shahada mbili za sheria kwenye masuala ya torts au sheria ya makosa inayoshughulikia makosa ambapo baadhi ya watu wamehujumiwa au kudhulumiwa kama kaya yetu ilivyofanyiwa. Hivyo, nina silaha nyingi mbali na umakini wangu za kuweza kuikoa kaya hii toka kwenye makucha ya wachukuaji waitwao wawekezaji na vyangudoa wao wa kiuchumi na kimaadili.
            Tano, nataka niunganishwe kwenye timu ya kujadiliana na watasha kutokana na kuwa na wasiwasi kuhusiana na usiri uliozunguka zoezi zima. Usiri wa nini kwani makinikia ni mali ya wanene au walevi? Mpaka naandika, sijui wanaoshiriki, taaluma, viwango vya elimu na uzoefu walivyo navyo, na kiasi cha uzalendo unaoweza kupimwa na historia za utendaji wao katika masuala ya kikaya na umma kwa ujumla.           
            Sita, pamoja na ulevi wangu sugu, mie ni bonge la mtu makini ambaye umakini wangu hauna kifani. Kwani natumia akili zangu na makinikikia yote kwa umakini zaidi. Fikiria nalewa kila siku lakini sijaachana na bi mkubwa tokana na umakini huu. Ukitaka kujua nimaanishacho wachunguze walevi wasio makini ambao mara nyingi huishia kupeana talaka ukiachia mbali kuwa watumwa wa nyumba ndogo. Mbali na hilo, mimi si rahisi kuhongwa; kwa vile sishobokei ukwasi na anasa za dunia. I am my own man with exceptional probity. Tokana na umakini huu, naamini nikishirikishwa kwenye mjadala wa makinikia, kwa vile unahitaji umakini, naweza kuokoa kaya yetu ikaheshimika na kutajirika hakuna mfano.
            Saba, nataka nishiriki ili niwe natoa mrejesho wa mazungumzo kwa walevi huku nikiwapa majina ya washiriki wa pande zote ili nao lau wapate picha kamili ya kinachoendelea. Pia lazima niwatonye walevi mazungumzo yanakofanyika ili mambo yakienda ndivyo sivyo watie timu na michupa yao na kuadhibu watakaokuwa wanazembea au kutetea maslahi binafsi.
            Kwa vile hili halitawapendeza wapenda kuficha mambo ya umma, najiandaa kwenda kwa pilato kama watanitolea nje. Tuonane wiki ijayo na yajayo.
Chanzo: Nipashe J'mosi kesho.

No comments: