Hivi karibuni, jukwaa la wahariri (TEF) lilitoa mpya pale lilipoitangazia dunia kuwa liliamua kumsamehe mkuu mmoja wa mkoa anayesifika kwa vituko kwa vile analindwa na baadhi ya uongozi wa juu nchini. Wapo waliopongeza hatua hii japo walioona hatua hii kama kujijivua nguo kama siyo kujikomba. Wapo waliojitenga na uamuzi huu huku wengine wakiulaani na kuona kama namna fulani ya kujidhalilisha na kuidhalilisha tasnia ya habari. wanaolaani kitendo hiki wanaona kama TEF wajidhalilisha kwa kumwangukia kigogo huyu mwenye tuhuma lukuki nyingi zikiwa za kughushi vyeti vya kitaaluma na kutumia majina bandia jambo ambalo ndilo chanzo cha mkasa uliomkumba na kumlazimisha kuvamia kituo cha Clouds Tv mwanzoni mwa mwaka huu akikilazimisha kirushe mkanda wa kumchafua adui yake aliyesifika kwa kumuumbua na kumuandama, mchungaji mmoja naye mwenye utata juu ya alivyopata ukwasi wake na mahubiri yake ya kisiasa na yenye kuonyesha wazi kujikomba kwa serikali tawala.
TEF wawe wakweli. Kwanza, hawakuamua kumsamehe mhusika kama walivyodai. Kwani, kwa walioshuhudia kitendo kilichofanywa na rais John Pombe Magufuli mkoani Tanga alikokwenda kuweka jiwe la msingi la bomba la mafuta toka Uganda akiwana na mgeni wake rais Yoweri Museveni, watakumbuka namna Magufuli alivyomwita mmilki mmojawapo wa Clouds TV na baadaye mtu wake yule na kuwapatanisha. Kwanza, zoezi lenyewe lilikosa mbinu ya kushawishi umma kuwa ulikuwa usuluhishi bali si ulazimishi. Kwani, rais aliibua suala hili ghafla tena kwenye shughuli ambayo haikuhusiana na utatuzi wa migogoro baina ya watu binafsi.
Pili, kwa hadhi yake, rais hakupaswa kujiingiza kwenye ugomvi usiolingana na hadhi yake. Angemuachia waziri husika amalize mgogoro huu. Tatu, kitendo cha rais kimezidi kumpa kiburi mhusika si kwa wana habari tu bali hata kwa serikali yake kuwa ni mtu asiyeguswa. Je ndoa hii itadumu kwa muda gani? Time will accurately tell yatakapoibuka mengine au kumkingia kifua kutakapozuia mapambano mengine yanayomgusa yeye kama vile kughushi, kujilimbikizia mali na matumizi mabaya ya madaraka. Rais hana uhuru wa kutumia madaraka yake kupendelea au kuumiza mtu yeyote hasa ikizingatiwa kuwa yuko pale kama mtumishi wa umma na si bwana wala mmilki wa taifa.
Kuwa salama, tunamshauri rais kuviacha vyombo vya habari vimalize migogoro yake. Pia rais hana haja ya kuonyesha anavyojipinga kwa kutawala kwa upendeleo wakati siku zote amekuwa akidai anatawala kwa haki bila kumwogopa wala kumuonea mtu.
Nne, rais si mahakama na hana haki kisheria kuvishurutisha kufanya baadhi ya mambo kama ilivyotokea kadhia hii tunayoongelea hapa. Kitendo hiki kilionekana kama aina fulani ya kulazimisha kumalizika kwa mgogoro bila kugusa kiini chake. Bahati mbaya sana, kusuluhisha ugomvi wa watu wawili umetumika kama chambo cha kurubuni TEF kujidhalilisha.
Baada ya TEF Kujidhalilisha wazi wapo wanaoanza kuhoji mambo mengi ambayo hapo mwanzo hayakuwa yakihojiwa. Mfano, wapo wanaodhani kuwa aliyewakosea wanahabarialikataa kata kata kuomba hata msamaha huku akikandia tume iliyoundwa na waziri wa zamani aliyetimliwa baada ya kuunda tume husika kuwa hawakumtendea haki wakati ukweli upo ushahidi kuwa mtuhumiwa alikimbia aliposikia tume ikigonga mlangoni mwake. Hivyo, kwa kujidhalilisha kiasi hiki, TEF wamejenga picha kuwa kuna ukweli uliokuwa umefichwa kuhusiana na kadhia hii nzima jambo ambalo laweza kuwa kweli au la.
Baada ya TEF Kujidhalilisha wazi wapo wanaoanza kuhoji mambo mengi ambayo hapo mwanzo hayakuwa yakihojiwa. Mfano, wapo wanaodhani kuwa aliyewakosea wanahabarialikataa kata kata kuomba hata msamaha huku akikandia tume iliyoundwa na waziri wa zamani aliyetimliwa baada ya kuunda tume husika kuwa hawakumtendea haki wakati ukweli upo ushahidi kuwa mtuhumiwa alikimbia aliposikia tume ikigonga mlangoni mwake. Hivyo, kwa kujidhalilisha kiasi hiki, TEF wamejenga picha kuwa kuna ukweli uliokuwa umefichwa kuhusiana na kadhia hii nzima jambo ambalo laweza kuwa kweli au la.
Yafuatayo ni maswali ambayo TEF inapaswa kuyajibu lau kurejesha heshima yake na kukubali kwa jamii nzima na tasnia ya habari:
Mosi, Je TEF ilishauriana na waandishi wa habari katika kufikia uamuzi wake wa kumfungia na kumfungulia mkuu wa mkoa? Je ni mawazo gani walitoa wadau wa tasnia hii yaliyoifanya TEF kufikia uamuzi huu kama siyo kusulutishwa na rais kumsamehe mtu wake?
Pili, Magufuli alisuluhisha ugomvi wa mtu wake na mmilki wa Clouds TV lakini si tasnia ya habari. Maana, haiingii akilini rais asuluhishe suala ambalo kimsingi liko mahakamani. Kufanya hivyo ni kuingilia uhuru wa mahakama na wahusika hasa wanaodai kukosewa.
Tatu, je TEF walishauriana na Baraza la Habari (MCT) kabla ya kufikia uamuzi wake? Je MCTnayo imeridhika na uamuzi huu tata na wa kudhalilisha tasnia?
Nne, je nani amewapa TEF kuwa wasemaji wa tasnia ya habari wakati kuna MCT?
Tano, je TEF inawakilisha kweli maslahi mapana ya waandishi wa habari wote au wahariri wachache ambao mmoja wa wahariri, Fumbuka Ngw’anakilala aliwatuhumu kutumiwa bila kupinga wala kutoa maelezo.
Sita, je shida za wahariri ni sawa na za waandishi wa kawaida wa habari ambao mara nyingi nao huonja makali ya wahariri kwenye taaluma yao?
Tumalizie kwa kuwataka wana tasnia ya habari kujisimamia na kuendeleza msimamo wao wa hadi haki itendeke. Maana walionyanyaswa si wahariri bali wana habari wadogo wa kawaida. Pia tunamtaka rais Magufuli ajitahidi kutofautisha mambo binafsi na ya umma ukiachia mbali kuacha upendeleo wa wazi ambao unapingana na mahubiri ambayo amekuwa akiyahubiri kila aendako ya haki na usawa. Mwisho, afikie akubali kuwa mtu wake halindiki; na asipoangalia atamchafua na kumuangusha.
Chanzo: Tanzania Daima J'pili kesho.
No comments:
Post a Comment