Juzi kijiwe kilipigwa na butwaa. Ni baada ya mahekalu ya bei mbaya kupigwa chini kule Kimara. Wengi walidhani ni mbavu za mbwa tu zilizokuwa zikipigwa chini kutokana na kilichofanyika kwenye bonde la Mkwajuni ambalo nalo siku hizi halisikiki limefikia wapi. Kweli mambo yanaenda yakibadilika!
Mgoshi Machungi anayeishi Kimara Mwisho anaingia akiwa mshawasha na tabasamu kuashiria ana jambo lisilo la kawaida. Anaamkua na kuomba muuza ampige na kikombe cha gahawa ili amwage sera. Baada ya kupiga funda mbili tatu anasema “wagoshi, hakika mambo yanaaza kubadiika kayani.” Anakunywa kahawa yake na kutaka kuendelea kabla ya kuendelea Mpemba kumchomekea “yakhe umaanishani kusema mambo kwa ufupi kana kwamba tumo kichwani mwako. Sa hayo mambo yabadilika vipi; hebu eleza uzuri lau tuelewe.”
Mgosi anajibu “Osie, huna haja ya kunihaakisha. Tuiza boi nikutuize na tikutosheeze.”
Kabla ya kuendelea Mpemba anajibu “yakhe tuheshimiane. Wewe ni wa kudai wataka ntuliza mie! Kwa taarifaako mie naweza kutuliza wewe na familia yako yote tena kwa siku moja.”
Mgoshi anakula mic “hapa sasa ubaya uko wapi ami. Kama wewe unataka kutuiza famiia yangu, kwanini sikutuize wewe hata ikiwezekana sasa? Basi ngoja nikutuize; utuie. Niiposema mambo yanaanza kubadiika niimaanisha uvunjaji wa mahekau ambao nimshudia kwa macho yaku pae Kimaa wakati nakuja. Jamaa wameangusha mahekau ya mamiioni ya shiingi bia kujai ni ya akina nani. Hii nimeipenda sana.”
Mpemba anajibu kwa mstuko “kumbe wamaanisha haya mahekalu yaniyoangusha kupita upanuzi wa barabara! Hapa nami nkubaliana nawe. Hata hivyo, naona hili zoezi kama vile la upendeleo yakhe. Kwetu Mikocheni lipo hekalu la yule mchunaji alojipachika cheo aitwaye Geti Rwakatarehe. Hekalu lake, licha ya kujengwa kusiko, lasababisha mafuriko kwani limejengwa kwenye nkondo wa nto. Mbona hili halijaguswa au nto si barabara iniyosafirisha maji kwenda baharini?”
Msomi Mkatatamaa anaamua kutia guu “kusema ule ukweli, nami naungana na wanaosema kuwa zoezi hili linakwenda ndiyo siyo. Wapo waliobarikiwa wasioguswa kama ilivyotokea kwenye sakata la kughushi vyeti vya kitaaluma au kutumia majina ya bandia kusomea vyuoni ambapo wapo walioadhibiwa na waliobebwa wazi wazi hata baada ya umma upiga kelele. Huyu mama tatanishi ajiitaye mchungaji wakati ni mchunaji na mwanasiasa hawezi kuvunjiwa hekalu lake. Ni muishiwa wa chama twawala. Nani atamgusa?”
Sofia Lion aka Kanungaembe anamchomekea Msomi “kaka huyu mama mwenzetu we acha. Mara umesahau namna shule zake zilivyokutwa zikitumia umeme wa wizi? Nini kilifanyika zaidi ya magazeti kuandika na kunyamaza? Hivi, unajua biashara anazofanya kidhabi huyu ambaye hupenda kuwadanganya akina mama kuwa anaweza kudumisha ndoa zake wakati yeye msimbe? Kaya hii we acha tu. Mtu analala maskini; na kuamka tajiri; hakuna anayehoji!”
Mijjinga anakula mic “zoezi hili usiniambie. Kuna jamaa yangu mfanyakazi wa benki aliangusha hekalu pale Kimara. Si nalo limekumbwa na panga la kuporomoshwa na kumuacha akiandamwa na shinikizo la damu.”
Kapende anakula mic “mie siwaonei huruma walioangushiwa mahekalu au mbavu za mbwa. Kama unajenga sehemu isiyoruhusiwa kisheria unategemea nini? tulizoea utawala usiofuata sheria na kulalamika. Sasa tumepata utawala unaofauta sheria hata kama ni kwa mapungufu kama mliyoeleza, tunaendelea kulalamika! Mie nadhani hata hekalu la huyu manzi mtatanishi na mchunaji litabomolewa kama umma utaamua kushika bango na kuuliza kulikoni badala ya kulalamika.”
Kabla ya kuendelea Mipawa anampoka mic na kuchonga “nakubaliana nawe. Tumezidi kulalamika kwa mambo ya muhimu na ya hovyo. Kama tunaona haki haitendeki, kwanini tusipige kambi nje ya hekalu na manzi huyu tuone lisirikali litatwambia au kutufanya nini? Napendekeza kesho tulianzishe tuone nini majibu ya wahusika.”
Kanji anakula mic “mimi iko uunga kono Pava. Vatu iko lalamika sana. Kama nataka pinduji nenda kwa hekalu ya hii manji na chunaji. Kama sirikali nasindwa bomoa venyeve.”
Mheshimiwa Bwege anaamua kula mic “siwashauri muende kupiga kambi pale. Cha mno nashauri tuandamane kwenda kwenye tume ya mazingira. Kama watashindwa kutatua tatizo husika, twende kwa mkuu wa mkoa anayejitia kujali matatizo ya mkoa huu tuone kama ataweza kutafuna mfupa uliowashinda fisi. Kimsingi, hapa kuna siasa zinafanyika. Hata hivyo, tokana na kutotabirika kwa dokta wa majipu, uwezekano wa hekalu hili kupigwa chini ni mkubwa. Ni suala la muda tu. Sina shaka. Hata hawa akina Bashite wanaoonekana hawaguswi, ni suala la muda. Bado arobaini yao haijafika. Kesho nitaandika barua kwa mamlaka zinazohusika nione watajibu nini.”
Mzee Maneno anachomekea “ngoja ngoja bwana? Hakuna cha kujipa matumaini kama mbwa kukalia mkia wakati tukishuhudia upendeleo tena kwa vihiyo. Tunahitaji kufanya kitu kuhakikisha mahekalu youte ya wanene yaliyojengwa kinyume cha sheria yanaporomoshwa haraka.”
Kijiwe kikiwa kinachanganya si akapita mchunaji Getty na hawara yake mpya! Acha tumzomee kabla ya kutokomea mtaa wa Uhuru nasi kuachana naye tusimpe umaarufu wa dezo.
Chanzo: Tanzania Daima J'tano leo.
No comments:
Post a Comment