The Chant of Savant

Tuesday 8 August 2017

Magufuli hana haja ya kulalamikia “mawaziri wapumbavu”

            Hivi karibuni akiwa mkoani Tanga, rais John Magufuli alilalamika kuwapo mawaziriwapumbavu kwenye baraza lake la mawaziri.  Alikaririrwa na vyombo vya habari akisema “ Mawaziri wengine ni wapumbavu, hawatoi decision (uamuzi) haraka ndiyo maana nasema ni wapumbavu.” Japo anayosema Magufuli yanaweza kuwa na ukweli hasa tukizingatia baadhi ya sifa za watendaji wake; na namna walivyoteuliwa hata wale wenye rundo la kashfa kama mmojawapo toka mkoani mwake aliyeshiriki kwenye kuingia mikataba mibovu kwenye uwekezaji kwenye sekta ya nishati na madini. Je ni kweli kuwa mawaziri hawa walioitwa wapumbavu ni wapumbavu kweli au ni zaidi ya hili? Pia hapa tunapata picha moja kuwa serikali ya Magufuli inapingana yenyewe kiasi cha mambo yanayopaswa kuishia kwenye vikao vya ndani kuanikwa hadharani sijui ili iweje zaidi ya kuionyesha serikali kama isiyoshikamana?
            Katika makala hii niatajikita kuonyesha ulipo upumbavu. Kwanza, niseme wazi; hakuna shaka kuwa Magufuli alirithi mfumo wa ajabu wa ulaji ambao ima uliasisiwa au kuendelezwa na watangulizi wake–ambao pia amesikika mara nyingi akiwananga na kuwalalamikia kuwa waliuza nchi kiasi cha kugeuzwa shamba la bibi. Kwa wanaojua namna naibu waziri huyu mwenye taaluma ya sheria alivyoshiriki kwenye kuingia mikataba mibovu wanashangaa nini kimembakiza ofisini wakati bosi wake alishatimliwa tokana na madudu yaliyogunduliwa kwenye wizara ambayo ameifanyia kazi tangu atoke shule.
             Kimsingi, hapa upumbavu si suala la watu binafsi bali mfumo ambao Magufuli alionyesha ima kuushindwa au kukubaliana nao aliporidhia kuweka kapuni Rasimu ya Katiba Mpya ambayo ilitaka kuufumua mfumo wa kiulaji na kuweka mfumo wa kuwajibika. Hivyo basi, Magufuli hana haja ya kulalamika, kumtafuta mchawi au kuwatoa sadaka baadhi ya mawaziri wake.
            Pili, Magufuli anapaswa kujua kuwa chanzo cha yote haya ni ile hali ya kugundua kuwa kumbe–pamoja na waziri mkuu Kassim Majaliwa kutoa amri zifungwe mita za kupimia mafuta yanayoingizwa nchini kupitia bandari za Dar es Salaam na Tanga hazijafungwa, sasa mwaka mmoja tangu amri itolewe–mita husika hazijafungwa. Siwezi kusema kuwa kutofungwa kwa mita husika ni matokeo ya ima woga au upumbavu wa mawaziri husika. Ni tatizo la kimfumo. Hivyo, hapa wa kulaumiwa si mawaziri husika bali mfumo.
            Swali linalopaswa kuulizwa na Magufuli na yeyote anayeitakia nchi mafanikio ni; Je ni kwanini mita husika hazijafungwa pamoja na kugunduliwa wizi wa kutisha mwaka mmoja uliopita? Je kuna watu wenye ushawishi wanaingilia maamuzi ya watendaji wa serikali ya Magufuli kama anavyopenda kuiita? Haiwezekani amri itoke juu na ipuuziwe kirahisi bila kuwapo na sababu za msingi. Je wahusika wanajiamini nini na wanafaidika vipi kutokana na kughairi kufunga mita za kupimia mafuta? Je huu ni mradi mkubwa wa wakubwa wenye ushawishi kwenye serikali ya Magufuli au serikali zilizopita? Je wale waliosimamia wizi huu kwa miaka zaidi ya kumi wamechukuliwa hatua gani kisheria? Je Magufuli afanye nini kuopambana na wizi na upumbavu huu wa wazi? Haya ni baadhi ya maswali ambayo Magufuli alipaswa kujiuliza kabla ya kufikia hitimisho la kuwaita baadhi ya mwaziri wake wapumbavu.
            Tatu, Magufuli anapaswa kufahamu kuwa tangu ameingia madarakani, ima kwa kujua au kutojua, ameimarisha mfumo huu wa kujuana kiasi cha kufanya na wengine kuona kuwa inawezekana kuwa kwenye tabaka la wale wasiogushwa. Rejea malalamiko ya muda mrefu dhidi ya mkuu mmoja wa mkoa anayetuhumiwa kughushi vyeti na sifa za kitaaluma ambaye rais ameamua kufa naye tokana na sababu anazojua mwenywe.
            Mbali na hili, wapinzani wamepiga kelele hadi wengine kuwekwa ndani mara kwa mara kuwa mawaziri na watendaji wengi wa Magufuli hawana uhuru wa kutimiza majukumu yao ima bila kuogopa kuingiliwa na rais au kumuudhi. Wengine hufanya maamuzi kwa kujipendekeza kwa lengo la kumfurahisha Magufuli. Mfano wa hivi karibuni ni wa waziri wa mazingira katika ofisi ya Makamu wa rais January Makamba aliyefukuza baadhi ya vigogo wa Baraza la Uhifadhi Mazingira (NEMC) akaishia kuwaona wakirejea ofisini bila maelezo yoyote. Huu ni ushahidi mwingine kuwa mfumo anaosimamia Magufuli haufanyi kazi kwa ushirikiano, ukaribu, uelewano hata pamoja.
            Je nini kifanyike? Mosi, hakuna jibu sahihi kama kwa Magufuli kufufua na kurejesha mchakato wa Rasimu ya Katiba Mpya ambayo ukusanyaji maoni yake uliligharimu fedha nyingi na muda mwingi.
            Pili, Magufuli anapaswa kusahau kuwa anaweza kubadili mfumo kwa kubadili sura za watu wakati mfumo husika ukiendelea kama ulivyo. Haiwezekani;na haitawezekana. Badili mfumo na kuweka uwajibika, mamlaka ya watendaji na mengine kwenye katiba uone. Hapatakuwa na mpumbavu wala mbebwa hata mmoja. Rais wa mstaafu wa Marekani Barack Obama aliwahi kuiambia Afrika kuwa inahitaji taasisi zenye nguvu lakini si watawala wenye nguvu. Je Tanzania tunazo taasisi zenye nguvu au kiongozi mwenye nguvu?
            Tumalize kwa kumshauri Magufuli kuwa asihangaike na kutafuta mchawi kwenye serikali yake bali afumue mfumo na kuufuma upya kwa kutumia Rasimu ya Katiba Mpya ambayo watangulizi wake waliua ili kuepuka kuwajibishwa kwa makosa yao.
Chanzo: Tanzania Daima J'tano leo.

No comments: