TAARIFA kuwa ndege yetu iliyokuwa itue
nchini kutoka nchini Canada ilikonunuliwa imezuiwa kutokana na deni la
mkandarasi, zinatia kichefuchefu, kuudhi na kuzua maswali mengi zaidi ya
majibu. Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye
pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alidai kuwa ndege yetu
imeshikiliwa kutokana na
kuvunja mkataba wa ujenzi wa barabara ya kutoka Wazo Hill
hadi Bagamoyo baina yake na Kampuni iitwayo Stirling Civil Engineering Ltd inayoidai
serikali dola milioni 38 na ushei. Kuna mambo ambayo serikali inapaswa kuyaweka
wazi. Je, Kampuni ya Stirling Civil Engineering Ltd ni mali ya nani na kama si
kampuni ya Kitanzania iliingiaje nchini au ni yale yale ya PAP, IPTL na madudu
mengine? Maswali hayaishii hapa. Je, kwa nini serikali imekuwa kimya na
inapoongea inatoa majibu ya kukanganya? Kunani hapa? Mkweli na
muongo ni nani katika sakati hili? Baadhi ya majibu unaweza
kuyapata kwa kusikiliza maelezo ya wahusika. Mfano, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Edwin Ngonyani, alikaririwa akisema bila kukiri au kukanusha
akisema: “Ninachojua ndege itakuja. Katika makubaliano ilitakiwa ifike Julai,
lakini ratiba zao kwa miezi miwili ijayo hadi Oktoba, ndege itakuwa tayari na
itakuwa imeshakamilika, ukweli utajulikana baadaye. Wasipoleta watakuwa
wame-breach contract (wamekiuka mkataba).” Mbali na Ngonyani, Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa Idara ya Habari, Zamaradi Kawawa, alikaririwa akisema: “Serikali
ilipata fununu mapema kwamba kuna baadhi ya viongozi wa siasa walikuwa nyuma ya
mpango huo na sasa wamejidhihirisha wazi kuwa wao ndio wapo nyuma ya pazia la
kuhujumu jitihada za serikali kwa masilahi yao.” Haya si majibu ya suala
linaloongelewa. Hata kitendo cha Kawawa kuitisha mkutano wa waandishi wa habari
kinazidi kuiweka serikali pabaya. Alikiri kuzuiwa kwa ndege hiyo. Badala ya
kutoa ufafanuzi wa kina yeye alijielekeza kwenye kutupa lawama zisizo na
mashiko kiasi cha kutia shaka uwezo wake wa kuelewa mambo, ukiachia mbali
kuitetea serikali yake. Sijui kama mhusika ana sifa zinazotakiwa kwenye wadhifa
wake.
Maana, ukisikia maelezo yake, unajenga shaka. Naye Lissu
anasema: “Kampuni ya Stirling ilikubali kuweka masharti nafuu ili Serikali
isilipe deni kubwa, lakini serikali yetu ikakataa.” Si Ngonyani wala Kawawa
aliyekanusha hili. Je, hapa anayehujumu nchi ni nani kati ya wale wanaosema ukweli na wale wanaokalia ukweli
ukiachia mbali kukalia kesi wakati wakijua madhara yake kwa taifa? Je, hapa
nani anaudanganya umma na kwa nini? Je,
kama ukweli utajulikana na tukakuta kuwa kweli ndege imezuiliwa kutokana na
kesi husika hawa wanaotudanganya watajiwajibisha au kuwajibishwa? Je,
Watanzania watakubali kuendelea kuwa na watendaji wasiowajibika kikamilifu kila
jambo linapotokea? Je, watakubali kuwaambia wahusika wawapishe watu wenye kujua
umuhimu wao kwa jamii na kueleza ukweli kwa kila jambo lenye masilahi kwa taifa
bila kuhofia vitumbua vyao? Napenda nitoe ushauri hasa kwa Kawawa na wengineo
walioshiriki kwa namna moja au nyingine kutufikisha hapa tulipo. Wajipime kwa
waliyosema na wachukue uamuzi mgumu. Maana, kila kitu kiko wazi. Muongo na
msemakweli wanajulikana katika kadhia hii. Nadhani mojawapo ya sababu za taifa
letu kuchezewa ni kuwa na watendaji kutojiamini. Hivi Kawawa angekuwa mwanasheria
aliyekabidhiwa kushughulikia kesi hii tungetegemea nini? Je, wapo kina Kawawa
wangapi kwenye ofisi nyingi na nyeti za umma? Mbali na maswali haya hapo juu,
kuna maswali mengine ambayo serikali inapaswa
kuyatolea majibu. Mfano, je, muda wote huu serikali ilikuwa
ikifanya au kungoja nini? Je, ni kwanini mkataba husika ulivunjwa? Nani
waliingia huu mkataba? Je, nini kifanyike?Nadhani tulivyochezewa kama taifa
ifikie mahali itoshe. Hapa lazima tukubali kubadilika haraka vinginevyo
tutazidi kuumia bila sababu za msingi zaidi ya ujinga na ubinafsi. Hapa lazima
serikali iwasake na kuwawajibisha walioingia mikataba hii ya kijambazi; na wale
walioivunja bila kuangalia madhara ya kufanya hivyo. Pia lazima tukiri kuwa
mfumo wetu wa uendeshaji nchi si mzuri kwenye maeneo fulani fulani, ni lazima
tuubadili kutoka kwenye hali tuliyonayo hadi tunakokutaka. Kila kitu sasa
kinategemea jitihada na usongo binafsi vya rais badala ya kuwa na mfumo
unaojiendesha bila kutegemea jitihada binafsi. Nimalizie kwa kusema; ushikwapo
shikamana; wahenga waliasa. Serikali ya Magufuli haina haja ya kunyamaza au
kukwepa ukweli wakati hasara husika ilisababishwa na serikali iliyopita. Ieleze
Watanzania kinachoendelea hasa ikizingatiwa kuwa fedha zinazotumika kununulia
ndege na ndege zenyewe ni za Watanzania ambao kina Kawawa wanajitahidi kuwaweka
sawa. Watanzania wana haki ya kuambiwa na kujua ukweli, kuhoji na kutaka
waliohusika na kadhia hii wawajibike
kisheria ili kuwa somo kwa wengine. Hii nchi ni mali yao na si mali ya
serikali wala yeyote zaidi ya wao wenyewe. Serikali ya Magufuli haiwezi kubeba
lawama zote hasa ikizingatiwa kuwa kadhia hii ilianza kabla ya kuingia
madarakani. Hata hivyo, haiwezi kuachwa jumla. Tangu iingie madarakani na kujua
kuna kesi kwanini ilikaa kimya au ilichukua hatua gani? Haya ndiyo masuala ya
kuangalia ili kuondokana na mazoea ya mafisadi na majizi wachache kuendelea
kuuibia umma wa watu wetu maskini. Je, ukweli kuhusiana na kukamatwa kwa ndege
yetu huko Kanada?
Chanzo: Tanzania Daime J'tano leo.
No comments:
Post a Comment