The Chant of Savant

Sunday 27 August 2017

Kutwaliwa ardhi ya Sumaye, je kuna unyakuzi wa ardhi?

Image result for photos of fredrick sumaye mashamba
          Baada ya waziri mkuu mstaafu wa awamu ya tatu Fredrick Sumaye kulalamika kunyang’anywa mashamba yake, wengi walishangaa. Hii ni baada ya kujua ukubwa wa mashamba husika na nafasi za mhusika alizowahi kushika hasa ikizingatiwa historia ya mhusika na namna suala la ardhi lilivyokuwa likichukuliwa tangu enzi za utawala wa awamu ya kwanza. Baada ya taarifa hizi kujulikana, wengi walijiuliza maswali mengi bila majibu mojawapo yakiwa; Je ni kweli Sumaye anamilki ardhi kubwa kiasi hiki? Je aliipata tokana na wadhifa wake au kwa kufuata sheria? Je ni vigogo wangapi kama Sumaye walitumia nyadhifa zao kunyakua na kumilki ardhi? Je ni wangapi na ukubwa wa ardhi wanayomilki ni kiasi gani? Je walipata ardhi husika kihalali na kisheria? Je nini kifanyike kuondokana na ubinafsi na unyakuzi huu?  Watanzania wana hamu sana ya kujua ni nani walinyakua; na nani hawakufanya hivyo ili kupima uadilifu na uhalali wao.
            Sumaye alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuhusiana na kutwaliwa mashamba yake yenye ukubwa wa zaidi ya hekari 300 ambazo ni nyingi kwa mtanzania wa kawaida asiye tajiri kulingana na kipato chake halali hata kama alikuwa kiongozi Sumaye alisema “Mimi sing’ang’anii hayo mashamba ninachokiomba haki itendeke lakini serikali imeingilia majukumu ya mahakama na kulitwaa shamba wakati kesi inaendelea mahakamani hili jambo siyo sahihi kabisa kwa nchi yenye kufuata utawala bora” Hapa kuna swali muhimu kumuuliza Sumaye. Je aliyapata mashamba husika kwa kuzingatia kanuni za utawala bora zinazomtaka mtumishi wa umma kutotumia mamlaka yake kujinufaisha binafsi kwa mali ya umma? Je Sumaye ameukumbuka utawala bora baada ya kuguswa?
            Kwa waliozaliwa na kukulia chini ya mfumo wa ujamaa wa awamu ya kwanza, watakuwa walistuka na kushuku; kuna mengi hayajajulikana; na yanapaswa kujulikana. Kwani tulizoea kusikia msamiati wa unyakuzi ardhi toka nchi jirani ambayo ilitupa msamiati huu pamoja na ukakasi wake. Japo si vibaya kwa mtanzania kumilkia ardhi kiasi anachoruhusiwa kisheria au kuhitaji, kwa wachache wenye mamlaka kunyakua ardhi yetu, tunapaswa kutokuwa na huruma nao bila kujali uhusiano au ukaribu wetu kwao. Nasema tusiwe na huruma nao hasa tukizingatia kuwa viongozi kama marehemu baba wa taifa Mwl Julius Nyerere alikufa akiwa anafanana na watanzania. Hata ukiangalia utajiri au mali alizoacha ambazo yenye thamani ni nyumba yake aliyojengewa na serikali, utakubaliana nami kwa hili. Inawezekana, ukimuondoa mwalimu, wengi wa viongozi wenye majumba ya kutisha na ya thamani, hawakuyapata kihalali kama tutakokotoa mishahara yao kwa muda wote waliotumikia au tuseme waliotumia umma kwa wale mafisadi kujitajirisha.
            Tokana na kufichuka ukweli huu wa vigogo, tunashauri yafuatayo:
            Mosi, Sumaye atendewe haki au kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria sawa na mwananchi yoyote bila kujali mafungamano yake ya kisiasa au msimamo na maoni yake.
            Pili, serikali ifanye ukaguzi kubaini ni vigogo wangapi walitumia mwanya wa kuwa kwenye utumishi wa umma kujineemesha kwa kunyakua ardhi ya watanzania ambayo kisheria iko chini ya serikali ili kuhakikisha na vizazi vijavyo vinafaidia nayo kwa kupewa sehemu yake.
            Sumaye, kama ameonewa kweli, aende mahakamani ili haki ijulikane. Na ikiwezekana, aeleze namna alivyopata ardhi husika ili kuwasaidia watanzania kubaini ukubwa wa tatizo.
            Tatu, kama hawezi kwenda mahakamani anyamaze; na kukubali yaishe.
            Nne, serikali itoe maelezo ya kina kuhusiana na sakata hili huku ikiepuka upendeleo katika kurejesha ardhi  ya umma. Mfano, baada ya kutwaliwa ardhi ya Sumaye, vyombo vya habari viliripoti kuwa rais mstaafu wa awamu ya pili anamilki ardhi kiasi cha hekali zaidi ya 1,000 bil ya yeye kukanusha.  Vyombo vya habari vilimkariri  mwenyekiti wa kijiji cha Wami-Luhindo, Apolinary Kahumba  akisema “Katika shamba la Mzee Mwinyi kuna ng’ombe na mbuzi wengi. Kuhusu ukubwa wa eneo la shamba hilo, sina uhakika sana lakini halipungui ekari elfu moja.Je aliipataje; na serikali ina mpango gani na ardhi hii? Lugha iliyotumika kutwaa ardhi iliyokuwa chini ya Sumaye ni kwamba hakuiendeleza. Kimsingi, kwa sheria za utumishi wa umma, hili lilipaswa kuwa la mwisho. Kwani, muhimu ni kujua namna alivyopata ardhi husika. Nasema hivi kwa kuzingatia kuwa, kama taifa, tutaruhusu kila mwenye mamlaka kuyatumia kupora na kunyakua ardhi ya umma, tutatengeneza bomu ambalo hatutaweza kulitegua huko tuendako. Kwani, wasio na mamlaka, ambao ni wengi nchini, watakosa ardhi baadaye na kuanzisha vurugu.
            Kama asemavyo rais John Magufuli, nitumie fursa hii kuchomekea. Wakati tukiwaandama wanyakuzi wa ardhi, tusiwasahau watuhumiwa wa ufisadi mwingine mkubwa unahohusisha fedha za umma kama vile kampuni ya Kagoda iliyodaiwa kuasisi na kunufaika na wizi wa fedha za EPA, kampuni ya Lugumi inayodaiwa kuibiwa umma mabilioni na utwaliwaji wa iliyokuwa Kampuni ya Usafiri Dar Es Salaam (UDA) iliyotwaliwa kijambazi mchana kweupe bila kusahau walioko nyuma ya jinai hii na wawezeshaji wake. Tukifanya hivi, tutatenda haki kwa taifa; na umma utatuheshimu kiasi cha kupembua pumba na mbegu baina ya malalamiko ya waathirika kama Sumaye na watakaofuatia.
Chanzo; Tanzania Daima J'pili leo.

No comments: