The Chant of Savant

Thursday 25 March 2021

DARASA TOKA KWA HAYATI JOHN POMBE MAGUFULI

Japo si mara ya kwanza kwa Tanzania kupoteza kiongozi wake, kifo cha rais hayati Dk John Pombe Joseph Magufuli kina masomo mengi ambayo ni nadra kuyadurusu kwa makala moja au kitabu kimoja. Mara ya kwanza, tulipata msiba wa baba wa taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere (1922––1999). Msiba huu ulivunja rekodi kwa waombolezaji. Hii ni kutokana na mchango aliotoa kwa taifa letu ukiachilia mbali uadilifu, uchangamfu, uchapakazi, ushupavu na weledi wake. Kwa waliokuwapo kipindi kile wanakumbuka mitaa jiji la Dar Es Salaam ilivyofurika watu wakati wa kuuaga mwili wake. Mara ya pili, taifa lilimpoteza rais wa awamu ya tatu hayati Benjamin Wiliam Mkapa (1938––2020). Majonzi yalikuwa makubwa japo si kwa kiwango cha Mwl Nyerere. Miezi michache, ilikuja funga kazi alipofariki ghafla rais Magufuli (1959––2021).
Pamoja na kuwa rais aliyewahi kutawala kwa kipindi kifupi nchini, Magufuli atakumbukwa kama rais aliyefanya mambo mengi katika kipindi hicho kifupi huku taaswira yake itambaa taifa zima na dunia nzima. Umati wake umevunja rekodi. Kwani, ilikuwa mara ya kwanza kuona akina mama wakitandika khanga na vitenge vyao barabarani ukiachia mbali akina baba kutandika T-shirts na masharti yao barabarani ili gari lililobeba mwili wake lipite juu yake kama alama ya heshima, kumbukizi na upendo kwa Magufuli.
Yafuatayo ni masomo muhimu yatokanayo na maisha na urais wa Magufuli ambayo, kimsingi, yanamtofautisha na watangulizi wake:
Mosi, kama nilivyodokeza hapo juu,  Magufuli aliweza kufanya mambo makubwa na mengi yaliyowagusa watanzania wote ndani ya kipindi kifupi cha miaka mitano kiasi cha miradi aliyoanzisha ima kuzidi au kuwa karibu sawa na yale yaliyofanywa na watangulizi wake, kwa pamoja. Mfano, rais Magufuli atakumbukwa kwa kujenga miundombinu mingi nchini kuanzia barabara, reli ya kisasa  (SGR), madaraja, flyovers mijini, meli, kununua ndege mpya 11, kulifufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), kufumua na kufuta mikataba ya uwekezaji ya kinyonyaji, kupambana na ufisadi, kutimua walioghushi vyeti vya kitaaluma, kupanua bandari, mashule, hospitali, zahanati, viwanda, kuongeza bajeti za afya na elimu na maendeleo na mengine mengi. Hii ni mojawapo na mambo yaliyofanya apendwe na kuheshimika sana. Kwani, kila mwananchi alimuona kama mwenzake na mkombozi wake. Akina mama waliokuwa wakijifungulia barabarani walijengewa zahanati karibu nchi nzima huku watoto wao wakijengewe mashule na elimu kutolewa bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari.
Pili, Magufuli alikuwa mfuatiliaji si kawaida. Katika muda mfupi, nadhani aliweza kutembelea nchi karibu kuliko rais yeyote. Ili kufanikisha hili, Magufuli aligoma kusafiri nje ya Afrika kwa kipindi chake chote. Alikuwa akitumia muda wake kutatua matatizo ya raia hata yaliyokuwa madogo. Umma utamkumbuka alivyokuwa akiwapa fedha maskini waliomlilia shida huku akiamuru wasaidizi wake kushughulikia matatizo ambayo asingeweza kupatia ufumbuzi pale pale. Ni kutokana na ufuatiliaji wake, Magufuli alikuwa mgeni kila sehemu Tanzania kila alipopata fursa ya kufanya hivyo ima kwenda kusikiliza matatizo ya wananchi au kufuatilia ahadi zake.
Tatu, Magufuli alikuwa na sifa ya kutopenda makuu. Aliwasumbua sana wasaidizi mara kwa mara akishuka kwenye gari lake kwenda kujiunga na wananchi ima kucheza nao, kutembea nao, kusalimiana nao au kuwasikiliza hata pale ambapo waandaji wa ziara zake walithubutu kuwaficha wasimfikie kumueleza matatizo yao. Ndiyo maana akapewa jina la Mtetezi wa Wanyonge. Na hakika. Alikuwa Mtetezi wa Wanyonge. Magufuli alikuwa mnyenyekevu wa kweli si kwa maneno tu hata matendo.
Nne, Magufuli alijaliwa kipaji cha kujieleza. Kila aliposimama kujieleza, alitumia lugha rahisi na kuhakikisha ujumbe wake unamfikia yule aliyemlenga. Mbali na kuzungumza lugha iliyoeleweka kwa wananchi, Magufuli alikuwa na matendo yaliyowateka watanzania. Mojawapo yalikuwa ule ujasiri wa kufukuza wasaidizi wake walizembea; kukamata mafisadi; kukemea hata wakubwa mbele ya wadogo huku akisisitiza kuwa kazi ya serikali haikuwa kuwatumia wananchi bali kuwatumikia. Alihakikisha kura alizopigiwa zinaleta matumaini na kukidhi matarajio ya wapiga kura na wananchi kwa ujumla. Katika kuthibitisha alivyokuwa amejitenga na umangimenza, Magufuli alisifika kwa mtindo wake wa kutumbua majipu ambao wakubwa wengi serikali hawakuupenda kwa vile ulikuwa unawanyang’anya tonge mdomoni.
Tano, Magufuli alikuwa akisema mara nyingi kuwa alikuwa amejitoa kafara na sadaka kwa Tanzania. Hivyo, hakuogopa kufa au kuuawa. Mara zote alikuwa akisema hili huku akimtanguliza Mungu kwa kila kitu. Na aliishi kana kwamba atakufa kesho huku akifanya mema na uwekezaji kana kwamba ataishi milele. Hakuwa muongo wala mbinafsi na mchoyo wala mlevi wa madaraka. Hakika, Magufuli aliishi kile alichohubiri na kuhubiri kile alichoishi. Katika kuonyesha kuwa kweli alikuwa kafara, hakusita kufanya maamuzi hatarishi na magumu kama vile kuzuia kuendelea kujengwa bandari ya Bagamoyo ambayo mtangulizi wake alikuwa ameithinisha wakati mradi wenyewe haukuwa na maslahi kwa taifa. Kila mtu anajua nguvu ya taifa la China kwa sasa. Ni Magufuli pekee aliyelitolea nje wazi wazi akisema kuwa ule mradi usingeweza kupitishwa hata na mwendawazimu.
Sita, Magufuli alikuwa mchapakazi hakuna mfano. Rais Samia Suluhu Hassan aliyemrithi alisema kuwa masaa 24 hayakuwa yakimtosha. Alisema kuwa Magufuli alifanya kazi sana hadi wasaidizi wake wakawa na hofu kuwa angeweza kudhuru afya yake. Pamoja na ushauri wa kupumzika, mara nyingi alikataa akaendelea kuchapa kazi. Hivyo, aliposema Hapa Kazi Tu, aliishi kauli mbiu hii ambayo ilimfanya akubalike kwa watanzania aliowahimiza kuchapa kazi na kujitenga na njia ya mkato katika maisha hasa akizingatia alikotoka kuwa mwalimu wa kawaida wa sekondari hadi akawa rais wa nchi.
Mwisho, kama nilivyoanza, si rahisi makala moja wala kitabu kimoja kuelezea mambo aliyofanya Magufuli ndani ya miaka mitano na miezi miwili ya urais wake. Tokana na staili yake ya uongozi, wapo wanaosema kwa kukata tamaa kuwa viongozi kama hawa hutokea mara chache katika nchi. Kuna ukweli japo wasemayo haya wanaonyesha hofu na wasiwasi kuwa hakuna wa kuvaa viatu vyake vikubwa. Kumbuka marehemu Thomas Isdore Sankara wa Burkinabe au Samora Moses Machel wa Msumbiji? Kwa hiyo, tusianze kuomba na kungoja atokee Magufuli mwingine Tanzania bali tujifunze masomo aliyotoa ili tuyarudufu katika kulikomboa taifa letu na bara letu. LALA MAHALI PEMA DK JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI rais wa awamu ya tano aliyetutoka.
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: