How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 17 March 2021

TANGULIA MAGUFULI, DAIMA TUTAKUENZI




Kifo hakina rufani, pia hakina huruma,
Kimempoka kundini, Rais mwenye heshima,
bado ali ujanani, mudawe umesimama,
Daima tutakuenzi, Tangulia Magufuli

Kifo hakina rufani, kwa kila mja lazima,
Kwa uchungu na huzuni, natakabari Karima,
Mjao yu mikononi, Dunia ameihama,
Tanzania takumbuka, maisha ya Magufuli.

Alikuwa muumini, wa ukweli kuusema,
Wengi aliwaudhini, hakuongopa daima,
Kipenzi cha maskini, utamlilia umma,
Tanzania takumbuka, mchango wa Magufuli.

Uoza ukibaini, ukweli uliusema.
Hukuwa na ya sirini, uliuambia umma,
Bila nani wala nini, daima ulisimama,
Daima tutakuenzi, tangulia Magufuli

Liwapiga marhuni, wakakiona kiama,
Hata huko mautini, jinale litasimama,
Akiwa mja makini, aliyejaa heshima,
Tanzania takumbuka, kipindi cha Magufuli.

Rais aliyewini, ulimkubali umma,
Jabari kimakwelini, imara alisimama,
Na amefia kazini, akipigania mema,
Pengo aliloliacha, pengo kubwa kweli kweli.

Baba nenda kwa Amani, tutaonana kiama,
Wala haumithiliki, kazi yako kazi njema,
Tunalia kwa huzuni, Mungu na akupe mema,
Tanzania bila wewe, inahitaji hekima.

Mudao madarakani, umefanya mambo mema,
Kapumzike peponi, ulikuwa mja mwema,
Umetuacha njiani, tukiwa tumesimama,
Tanzania takumbuka, tunu zako Magufuli.

Maisha ya mja nini, ayajuaye Karima,
Matunda yamesheheni, kwa uliyofanya mema,
Nenda baba umewini, jinalo litasimama,
Tanzania takumbuka, mipango ya Magufuli.

Wezi uliwabaini, wakakionja kiama,
Yajayo tupo kizani, roho zinatutetema,
Mungu aliyetupeni, amechukua mapema,
Kwa akili zao waja, bado hatujakubali.

Jabari u kitandani, dunia umeihama,
Tutakuweka nyoyoni, hadi siku ya kiama,
Tunatoa shukrani, kwa yale tuliyochuma,
Mungu akupe amani, tangulia Magufuli.

No comments: