The Chant of Savant

Tuesday 23 March 2021

Waraka wa Nkwazi kwa Watanzania na Wanyonge Dunia Nzima


Ndugu watanzania, wapendwa, kwanza nitoe salamu za rambi rambi kwa familia ya marehemu Rais John Pombe Magufuli aliyetutoka hivi karibuni na taifa kwa ujumla. Hakuna ubishi. Hiki ni kipindi kigumu na cha pekee kwetu kama jamii na taifa. Tuna changamoto nyingi kubwa ikiwa ni kama kweli mema yote aliyotenda yataendelezwa ikiwamo miradi mikubwa na utetezi madhubuti wa wanyonge.  Pia ni mara ya kwanza kwa taifa letu kupoteza kiongozi wake akiwa ofisini ingawa sisi si wa kwanza kupata balaa hili. Tunayo mifano ya mataifa jirani kama vile Kenya alipofariki mwanzilishi wake Jomo Kenyatta mwaka 1978, Zambia ambapo rais wake wawili, Levy Mwanawasa, 2008 na Michael Satta, 2014 na  Malawi ambapo rais Bingu wa Mutharika alifia madarakini 2012, makamu wao walichukua madaraka. Nchini Msumbiji, alipokufa Samora Machel, mwanzilishi wa taifa hilo, waziri wake wa mambo ya nje Joachim Chisssano aliapishwa kushika madaraka. Pamoja na wote, ni mwanamke pekee aliyechukua nafasi ya urais aliyekuwa makamu wa rais. Huyu si mwingine bali Joyce Banda ambaye alimalizia kipindi cha mtangulizi wake lakini akashindwa kujijengea ushawishi wa kuchaguliwa alipogombea baada ya kumaliza kipindi husika. Mwingine aliyeshindwa kufua dafu ni Rupia Banda pale nchini Zambia. Naye aliongoza baada ya kifo cha Mwanawasa akakimaliza na kushindwa katika uchaguzi uliofuata.
            Je hili linatufundisha nini? Ni mambo mengi kubwa likiwa onyo kwa rais wetu mama Samia Suluhu Hassani aliyerithi nafasi ya hayati Magufuli. Naamini na kumpa angalizo kuwa kama atataka kwenda mbali zaidi ambayo ni haki yake na anastahili, ahakikishe anavaa viatu vya marehemu na kutimiza yale waliyokuwa wakiyafanya pamoja hasa kuipeleka nchi kwenye uchumi wa viwanda. Hili linahitaji kujitoa mhanga na kupambana kweli kweli. Hivyo, tumsaidi atufikishe huko. La pili, kama wananchi, tuhakikishe tunachapa kazi na kudumisha mshikamano wa kitaifa ili taifa letu liendelee kuwa kisiwa cha amani. Tukifanya hivi, hatutajiletea maendeleo tu bali tutamuenzi hayati Magufuli ambaye wanyonge wengi walimpenda kutokana na kuwapa matumaini na wengine kuwainua kwa kuhakikisha wanatendewa haki.
            Kama taifa, nawaomba tumpe ushirikiano kiongozi wetu mpya kuhakikisha tunashikamana na kushirikiana katika kumuenzi rais Magufuli aliyetokea kupendwa hata zaidi  baba wa taifa Mwl Julius Nyerere. Sipigi chuku. Ukiangalia umati uliofurika kumuanga Magufuli ukalinganisha na ule uliomuaga Nyerere na namna vilio vilivyotawala, utajua nisemacho. Sijui kama hata waliompokea Yesu kule Jerusalem walivunja rekodi hii. Mapenzi yetu tuyaonyeshe kwa mrithi wake na kuhakikisha tunamkumbusha pale anapotokea kusahau jambo bila ya kulazimika kuleta vurugu.
            Kama taifa, nawaomba na kuwasihi tuhakikishe kasi ya kupambana na ufisadi inaongezeka. Kama taifa hasa umma wa wanyonge, tusikubali kuona miradi ya maana aliyoanzisha Magufuli kama vile ufufuaji wa Shirika la Ndege Tanzania kwa kununua ndege mpya kwa kutumia fedha yetu, kujenga reli ya kisasa ya SGR, kupanua bandari zetu, kujenga meli na barabara na mingine mingi vinauawa.  Naomba nieleweke kuwa sina maana kuwa vitu hivi vitakufa. Ila ikitokea kukawa na dalili za kufanya hivyo, tusiogope lolote bali kuhakikisha tunavisimamia na tunavitunza kwa uaminifu mkubwa.
            Kama taifa, naowamba mhakikishe mali na raslimali zenu zinawanufaisha wote na si wachache. Kimsingi, hakuna miujiza aliyotenda hayati Magufuli ila kusimamia mali na raslimali za umma kwa uadilifu na usawa. Kama jamii, lazima hili mhakikishe linafanyika ili kuondoa mianya ya kunyonyana na kuweza kusababisha ukosefu wa amani na haki. Hili si jambo la kuomba au kupewa kama hisani. Hayati Magufuli alilionyesha hili kwa vitendo. Hivyo, kila mtu asimamie haki si kwa ajili yake tu bali hata wengine hasa wanyonge ambao ndiyo walio wengi. 
Magufuli alikuwa rais wa wanyonge duniani
             Japo alichaguliwa na kuongoza watanzania bila hata kwenda nje kuzurura, hayati John Pombe Magufuli hakuwa rais wa Tanzania tu. Kisheria alikuwa rais wa Tanzania. Kimsimamo, alikuwa rais wa Afrika nzima. Ukizingatia nchi Jirani zilivyompa heshima ya kwa kutangaza siku za maombolezo, haijawahi kutokea. Uganda wametangaza wiki mbili za maombolezo, rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Felix Tshekedi alisitisha kila kitu na kuhutubia taifa kulitaarifa siku tatu za maombolezo. Magufuli ameombolezwa karibu dunia nzima kwa namna tofauti. Mfano, wapo watu waliotoka sehemu mbali mbali duniani kuja kuungana na watanzania katika msiba huu mzito.
            Kwa watanzania na dunia nzima, mambo aliyoweza kuyafanya kwa muda wa miaka mitano–––kama angekuwa sawa na wahubiri matapeli wanaotangaza kufanya miujiza wakati ni utapeli–––basi angeweza kuyaita miujiza. Hakuna kitu kilichomfanya Magufuli kukubalika na kuheshimika duniani kama kuwajali wanyonge, kupambana wazi wazi na ufisadi, kujiamini, uzalendo na uchapakazi usio na mfano. Aligusa maisha na nyoyo za wengi duniani hasa watu wa tabaka la kawaida. Nakumbuka rafiki yangu kiongozi wa kata alipokaribishwa ikulu kukutana na rais, aliniambia kuwa alitoa machozi na si yeye pekee bali wengi wa kada yake. Kwani, kwa maisha yao yote, hawakuwahi hata kuota kuwa wangeingia ikulu achia mbali kuwa kikao na chakula na rais wa nchi. Lakini Magufuli–––mtoto wa mkulima ambaye hakusahau alikotoka–––aliweza kuwafanya watu wa chini kama hawa kukaa ikulu na kuongea na rais bila woga wala kusumbuliwa. Nadhani, hakuna rais aliyewahi kuipeleka ikulu kwa wananchi kama Magufuli. Hakuna rais zaidi yake aliyewahi kushuka kwenye gari na kwenda kuwasikiliza wasiojiweza tena akikaa nao kwenye mavumbi na kuwasikiliza kama Magufuli. Hakuwa mtu wa makuu wala majivuno zaidi ya ubinadamu na unyenyekevu. Ndiyo maana akapendwa duniani nzima has ana wanyonge.
            Mie na mzee Pius Msekwa, Spika mstaafu wa Bunge la Muungano, tuliandika kitabu kinachoweza kutafsiriwa kama Umagufuli, nadharia inayoweza kueleza msatakabali wa Afrika na Magufuli afanyaye mambo kutokea au kwa kimombo Magufulification, the Concept That Will Define the Future of Africa and the Man Who Makes Things Happen ambacho kilitoka mwezi mmoja kabla ya mauti kumfika.
            Baada ya kutangazwa msiba wake, pamoja na mstuko na ngoa, niliweza kutumia muda kwenye mtandao nikidurusu namna dunia ilivyoupokea. Nilisika maneno yaliyoelezewa kama makufuru ya msanii mmoja aliyeamua kumtukana Mungu kwa vile alimuombea sana marehemu neema lakini akamchukua. Nilisikia mshairi toka Afrika Kusini, mama aliyetoka Kenya kuja kuomboleza na wananchi mbali mbali wa mipakani ukiachia mbali marafiki zangu toka pande zote za dunia walionipa salamu za rambirambi na kuelezea namna walivyomkubali Magufuli. Nilisomakwenye mitandao wasiwasi juu ya kutekelezwa miradi aliyoanzisha Magufuli na kuendeleza mema na staili yake ya kutawala hasa ukweli, uwazi, upendo na kutoogopa ukiachia mbali utabiri wake juu ya kifo chake. Kwani, mara nyingi alikuwa akiwaandaa watanzania kuishi baada ya yeye kuondoka duniani kana kwamba alijua kifo chake.

            Kwa ufupi ni kwamba rais Magufuli hakuwa wenu peke yenu bali dunia nzima. Ndiyo maana msiba wake ni wa dunia nzima hasa ikizingatiwa alionyesha njia ambayo­­­–––kama Afrika kweli inataka kujikomboa–––kila nchi ikizurudufu, inaweza kusonga mbele ndani ya muda mfupi. Namaliza kwa kuwaomba viongozi wetu wasituangushe wala kumuangusha Magufuli kama alivyopenda kusema mara nyingi kila alipohutubia taifa. LALA PEMA SHUJAA WETU JOHN POMBE MAGUFULI.
Chanzo: Raia Mwema leo

No comments: