The Chant of Savant

Wednesday 17 March 2021

Je ni Manispaa na Halmashauri Ngapi Zina Madudu Kama Temeke? HILI NI AGIZO KATI YA MAWILI YA MWISHO ALIYOTOA MAGUFULI

Kuna clip ya video iliyozagaa mtandaoni ikimuonyesha Rais John Pombe Magufuli akisikiliza ombi na baadaye aki’mtandika’ Mbunge wa Temeke Dorothy Kilave baada ya kumuomba serikali yake iilipie Manispaa hiyo deni la shilingi bilioni 19 ilizokopa toka Benki ya CRDB kwa ajili ya kulipa mafao ya wale waliobomolewa maeneo yao ili kupisha miradi ya maendeleo ambayo Mbunge hakutaja. Hata hivyo, pamoja na kum’tandika’ Mbunge huyu,  Rais alimtetea kuwa yeye hakuwa sehemu ya ufisadi huu wa kutisha na wa kijinga. Hivi unachukuaje fedha kwenye taasisi binafsi kufanya shughuli za umma bila kufuata taratibu husika halafu unataka Serikali ikulipie kana kwamba ndo ilifanya haya madudu? Maana kama Manispaa ya Temeke ingefuata utaratibu, Serikali ingekuwa na taarifa ya deni husika. Je huku siyo kukiuka taratibu na sheria ukiachia mbali kuwa uchochoro mzuri wa ufisadi? Je miradi inayodaiwa kutekelezwa ni mingapi na inalinga na fedha tajwa?
        Jambo la kufurahisha ni kwamba, kwa ukali na uwazi wake, Rais alisema Serikali katu haikuhusika kwenye kutafuta na kupata mkopo husika. Hivyo, haina sababu za kulilipa bila kujua namna lilivyopatikana, kutumika na mengine kama haya. Mbali na msimamo wa Serikali, Rais alisema wazi kuwa anadhani kuna ulaji hasa ule utokanao na kuwekeana aslimia fulani kwenye mkopo au almaarufu cha juu. Tokana na mashaka haya, Rais alitaka miradi inayodaiwa kujengwa kwa fedha husika ikaguliwe kuona kama ina thamani ya fedha tajwa au kuna upigaji. Tokana na uzoefu wake, Rais alisema kuwa pia kuna haja ya kujua waliolipwa fidia ni akina nani, wangapi isijekuwa nao waliongea na Manispaa ili kufanikisha ulaji huu. 
        Katika kuonyesha Rais alivyo tayari kuwasaidia Manispaa ya Temeke kujua namna ya fedha ilivyotumika, alisema anachoweza  kuwasaidia ni kutuma wakaguzi wa mahesabu ili wawasaidie kufichua madudu ambayo ni dhahiri yatakuwapo tena mengi na makubwa. Kwa wanaomjua Rais Magufuli, hawatashangaa kusikia wale wote waliohusika wakipambana na kesi za uhujumu taifa ambazo ni stahiki yao. Maana, kama alivyoahidi rais wakati akiingia madarakani, zama za Tanzania kuwa Shamba la Bibi kwa kila Bwege kujiibia zilikwisha zamani.
        Sakata la Manispaa ya Temeke na deni lake lina maswali mengi zaidi ya majibu. Mfano, je Serikali ingelipaje  deni wakati haikutumia fedha husika wala haikuombwa lau ushauri wakati wa kuchukua mkopo huu wa kipigaji? Eti Manispaa ya Temeke imekuwa ikilipa shilingi bilioni nne kila mwaka na bado, kwa mujibu wa Mbunge, deni ni zaidi ya bilioni 12.195. Je walikuwa wakilipa nini hadi deni halipungui? Je waliingia lini kwenye mkataba wa deni na ulipaji wake? Je Manispaa ya Temeke wanatozwa riba kiasi gani? Na je riba husika ni stahiki na inangia akilini kiutaratibu? Je masharti ya mkopo husika yanaingia akilini?
        Si vibaya kusema kuwa Manispaa ya Temeke hawamheshimu hata Rais wao. Ilikuwaje na kwanini wahusika walitaka kumuingiza mkenge? Ni kwanini hawakulichelea hili kuwa mtu yeyote mwenye akili angehoji mantiki ya Serikali kulipia deni bila kuhusika na kulitafuta wala kutumia fedha husika? Je ni Manispaa na Hmashauri ngapi zinayo madudu kama haya ambayo hayajafichuka? Je Manispaa na Halmashauri kama hizi zimejifunza nini tokana na kujilipua kwa Manispaa ya Temeke japo haikujua kuwa ilikuwa ikifanya hivyo? Je mamlaka husika yatachukua hatua gani mujarabu ili kutoa somo kwa wengine? Je ni mbalioni kiasi gani ya fedha za umma yameishatafunwa namna hii na kwa muda gani? Je hili halitoi somo kuwa Serikali zichunguze mamlaka zote za halmashauri nchi nzima kubaini madudu hata kama yamefanyika miaka 20 iliyopita ili wahusika warejeshe chumo hili la wizi na kushughulikiwa kisheria ili haki itendeke na liwe somo kwa wezi wengine?
        Kutokana na kukithiri kwa ufisadi kiasi cha walioushiriki kutaka hata kuiingiza Serikali mkenge, tunashauri Rais aamuru Manispaa na Halmashauri zote  nchini zinazodaiwa fedha za mikopo toka kwenye taasisi binafsi zifanyiwe uchunguzi na ukaguzi ili kujua kilichoko nyuma ya pazia ambacho wengi hawakijui. Hii, licha ya kutoa onyo kwa wahusika, itaokoa fedha nyingi za umma ukiachia mbali kunasa mapapa wengi wa mchezo huu. Uchunguzi huu usiishie kwa wakopeshwaji bali hata wakopeshaji. Hii itasaidia kuona kama kweli wanafuata sheria za mikopo na kufanya biashara na taasisi za umma. Madudu ya namna hii yamekuwa donda ndugu kwenye Nchi za kiafrika ambacho ndicho chanzo kizuri cha umaskini wa nchi nyingi ambazo zimekosa umakini katika kuyatokomeza. Juzi, Nchini Kenya, kulitoka taarifa ya mtu aliyepewa tenda ya mabilioni na mtu ambaye hata hawakujuana ilmradi mhusika amtumie kuliibia Taifa. Haya mambo yapo na ni mengi kuliko unavyoweza kufikiri.
Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: