How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Friday, 26 March 2021

Waraka wa Nkwazi kwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan (SSH)

Mpendwa Mama Rais,
Niruhusu kwa taadhima:
Kwanza nikupe pole binafsi kwa kufiwa na rais wako ambaye kufariki kwake, kumekulazimisha kupokea nafasi hiyo kwa majonzi–––kama ulisema baada ya kuapishwa kama itakavyo katiba ila siyo wewe–––kuwa umekula kiapo hiki tofauti na vingine vyote ukiwa na majonzi. Kimsingi, kiapo chako haikuwa sherehe bali msiba.
        Pili, wewe si mgeni katika uongozi japo si mwenyeji katika urais. Kuwa makamu wa rais na kuwa rais ni vitu viwili tofauti. Unayajua mengi kuliko sisi ingawa si yote. Nasi tunayo tunayoyaona na kuyajua ambayo unaweza kusahau baada ya kutwaa ukubwa.  Kwa unyenyekevu naomba univumilie na unisikilize. Chonde mama chama chako usikidharau wala kuruhusu wasaka ngawira wakirejeshe alikokitoa marehemu John Pombe Magufuli. Maana hakuna chama hakuna urais. Magufuli ameicha CCM pazuri. Zidi kuing’arisha. Magufuli–––licha ya kusafisha chama, alikitia adabu na kuacha kimeshikana–––jambo ambalo lilimpa amani ndani ya chama na kuweza kufanikisha mambo mengi kwa muda mfupi kiasi cha kuwapiku waliomtangulia kwa miaka mitano tu aliyokaa madarakani.
        Tatu, Mama Rais, tafadhali tekeleza si kutelekeza mema yote yaliyomfanya Magufuli awe Magufuli aliyependwa na kuheshimika dunia nzima. Sisemi ung’ang’anie timu yake au kila kitu. Ila unawajua mliokuwa mkifanya kazi nao. Unajua wabovu na wanaofaa. Muhimu, unajua kuwa kujiamini na kutoogopa lawana, kusema ukweli na uchapakazi ndiyo siri iliyomfanya marehemu ang’are Tanzania, Afrika na dunia nzima.
        Naomba nikukumbushe mambo yaliyompaisha marehemu Magufuli kama ifuatavyo:
        Mosi, kumbuka kupambana vilivyo na ufisadi bila kumuangalia nyani usoni. Mafanikio na uzoefu wa muda mfupi kama taifa, vilituletea matumaini na kujiamini kuwa kumbe tunaweza tukiamua. Katika hili, wewe ni shahidi sawa na waathirika na wanyonge ambao mrithi wako aliwapambania vilivyo na wazi. Nawe Mama usiruhusu ufisadi ushike kani kama zamani. Nakuomba chonde chonde. Jifunze kwenye baadhi zama ambapo nchi ilifanyiwa majaribio mbali mbali kubwa likiwa ruksa iliyoanzisha kila mwanya wa ufisadi ingawa mwanzilishi wake alikuwa na nia nzuri wakati ule.
        Pili, mtangulizi wako alikuwa mkweli na muwazi katika utawala wake. Unajua namna alivyofanya maamuzi bila kusitasita wala kumuongopa mtu hata kama siku zote hayakuwa sahihi. Hata mifano ya marehmu Magufuli inaonyesha kuwa walio wengi  wanapenda ukweli hata kama unawaudhi wachache wenye mamlaka
        Tatu, alisifika na kupendwa kwa kupigania haki za mwananchi wa chini huku akijitenga na magenge ya wafanyabiashara na wala na watoa rushwa. Wengi wataanza kukutafuta kwa udi na uvumba hasa sasa baada ya miaka mitano ya kubanwa kila kona.
        Nne hakikisha hutovumilia ubabaishaji, ufisadi, uharibufu wa fedha na mali vya umma, uzembe, wizi na mengine kama hayo. Wengi waliokumbwa na panga la Magufuli watakuwa wakisherehekea na kuandaa mikakati ya kurejea kwa kishindo. Usiwape nafasi.
        Tano, Magufuli alihakikisha kila mradi anaoanzisha unafanikiwa. Hapa siri ni rahisi. Kufuatilia kila jambo kwa ukaribu. Alitaka kuona thamani ya miradi kwa fedha aliyokuwa akilipa.  Hili nalo si gumu kama utaamua kuchapa kazi ukijua kuwa malipo si duniani bali huko mbinguni.
        Sita, usiue maono na visheni na kiu ya kujitegemea na kuionyesha dunia kuwa tunaweza hata bila ya wafadhili wawe halali au haramu. Ndiyo maana, tangia mtangulizi wako alipochaguliwa, hakuwahi kuonekana na makundi ya wafanyabiashara matapeli na wabaguzi tuliozoea huko nyuma wakiwazunguka viongozi wetu ingawa wengi hawakuchagua wala kuwa raia.
        Saba, hakuna jambo lilimpa sifa kama vile kubana matumizi akapiga maarufu sherehe,warsha na ziara visivyo na tija kwa taifa bali ulaji wa wahusika. Aliondoa uzururaji huu kwa fedha ya umma hasa ughaibuni ambao ulishakuwa donda ndugu. Maendeleo yako nyumbani na si ughaibuni. Fedha iliyookolewa iliekezwa kwenye miradi ya baadaye na kudumu ya kijamii kama barabara, madaraja na mengine mengi. Aliweza kupunguza hata mshahara wake. Simaanishi upunguze wako. Ila kama unataka kuendelea kuongoza baada ya ngwe hii, haya mambo ni muhimu kuyazingatia na kuyafanya. Hivyo,  si uwekeze tu kwenye mirand bali hakikisha unamalizia miradi aliyoanzisha marehemu huku ukipanga kubuni mipya.
        Nane, Magufuli hakuwa mwoga wala mnafiki. Alimtanguliza Mungu kwa kila alichofanya. Hivyo, mama inapokuja kupambana kwa ajili ya wanyonge, usiogope mtu wala lawama bali kutenda haki. Najua unaweza. Na kama utafanikisha hili, ile dhana kuwa akina mama hawawezi utakuwa umeipatia jawabu mujarabu. Siri moja, kama utafanikisha ahadi za Magufuli, sina shaka, utaongoza hadi 2035. Ni juu yako kuangalia karibu au mbali kulingana na ulivyoamua kuwa. Kimsingi, watanzania wanataka rais anayewapa matumaini na kuwainua wanyonge akijitenga na wale wanaowadharau au kuwadhulumu wanyonge walio wengi.
Kabla ya kumaliza ngoja tugusie mambo mengine ambayo, kwa kiwango fulani, marehemu hakuweza kuyafanya japo yanao umuhimu kwa taifa. 
        Mosi, taifa linahitaji katiba mpya ambayo itajenga mfumo unaojitegemea wa kuendesha nchi badala ya huu wa sasa unaotegemea nani yuko madarakani. Kimsingi, mema yote aliyofanya Magufuli yangekuwa kwenye katiba na mfumo wetu wa uendeshaji, usingekuwa na changamoto zinazokungojea baada ya kuapishwa. Tunahitaji mfumo wa kuwajibika unaojitegemea badala ya kutegemea rais pekee kama ilivyo sasa.
        Pili,Tanzania inahitaji mfumo unaomlazimisha kila mtanzania kutangaza na kutoa maelezo ya mapato yake kila mwaka. Hii ndiyo siri iliyozifanya nchi za magharibi kuendelea na kutajirika na kuepuka ufisadi wa kutisha. Kwani, mfumo huu wa kisheria unaomtaka kila mwananchi na mkazi atoe taarifa za mapato yake kila mwaka unaua motisha wowote wa watu kuingia kwenye jinai zinazowawezesha kupata utajiri wa haraka.
        Tumalizie kwa kukutakia kila la heri na fanaka katika kazi yako mpya.  Mungu akusimamie, akushauri na kukupa kila ujasiri na weledi unaohuitaji katika kutekeleza majukumu yako kama rais kwa mujibu wa viapo ulivyokula. Tunakuombea ufanye makubwa ili hata kwenye uchaguzi ujao chama chako kiweze kukupendekeza kugombea tena uweke rekodi nyingine. Kama ambavyo wanawake wameweza kuwazaa wanadamu wote, tuonyeshe kuwa wanaweza kuwaongoza. Akina Margaret Thatcher, Mary Robinson na  Angela Merkel huko Ulaya waliweza kulithibitisha hili bila shaka yoyote. Nakuomba mama Samia. Anzisha mchakato wa kutengeneza African Iron Ladies (AILs). Mama, natamani uwakosoe wale wanaosema mwanamke hawezi, uvunje hata rekodi ya Magufuli kama utaamua. Cha mno ni kuwa rafiki wa maskini hata kama matajiri watakuchukia kama ilivyokuwa kwa hayati Magufuli. Natanguliza shukrani. Kazi kwako.
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: