The Chant of Savant

Tuesday 30 March 2021

JE WAPO KAKOKO WANGAPI HAWAJANASWA?


Kwa waliofuatilia kashfa kwenye Bandari ya Dar Es Salaam, hawana shaka kuwa hatua alizochukua rais Samia Suluhu Hassan (SSH) zilipaswa kuchukuliwa miaka mingi iliyopita. Japo bandari zetu zimekuwa sehemu za upigaji fedha ya umma kwa muda mrefu, baadhi ya madudu yaliyofanyika chini ya utawala mkali na mfuatiliaji ya tano, yana utata. Leo tutagusia kashfa inayoendelea kutukuta ya ukwapuzi wa fedha uliisababishwa kusimamishwa kazi Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari (TPA) Deusdedit Kakoko–––kama ulivyoamuriwa na mheshimwa rais. Wanaokumbuka kashfa ya mwaka 2017. Kakoko alikaririwa na akisema kuwa “wapo wanasiasa wakubwa wakiwamo wabunge wananiambia kwamba vita ya flow mita kamwe sitaiweza, nawaambia sitaki kuingiliwa na mwanasiasa yoyote nitafanya kazi zangu kulingana na maagizo ya Rais John Magufuli, Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Mawasiliano (Profesa Makame Mbarawa).” Alisahau kuwa hata Makamu wa rais wakati ule ambaye ni rais wa sasa alikuwa sehemu ya watu ambao wangeweza kumpa maagizo ya nini cha kufanya. Wengi walishangaa kwanini Kakoko alikuwa akilalamika badala ya kuwataja wazi waliokuwa wakimkwamisha kama kweli aliyokuwa akifanya yalikuwa kwenye mamlaka yake?
Tukio jingine ambalo hata hivyo sijui lilivyomalizwa, lilihusu vichwa vya treni vilivyoingizwa nchini kinyemela. Hadi sasa hatujui waliokuwa nyuma ya kashfa hii iliyouawa kinamna sawa na ile iliyohusisha upigaji wa hali ya juu uliofanywa na kampuni ya Lugumi Enterprises iliyopewa tenda ya shilingi bilioni 37 kinyemela kufunga mashine za kutambua alama za vidole nchi zima bila kufanya hivyo.  Tuchukue nafasi hii kumkumbusha rais SSH kuwa na hili ni jipu analopaswa kutumbua ili kutoa onyo kwa waliodhani atakuwa legelege wakati anao uwezo kufanya makubwa hata zaidi ya mtangulizi wake tena bila kutuhumiwa kukandamiza haki za binadamu.
            Kwa vile Kakoko aliwahi kulalamikia wanasiasa waliokuwa wanamkwamisha kwenye suala la mita, ni wakati muafaka kutwambia liliishaje na huu ukwapuaji wa fedha za umma nao anamshutumu nani. Kwa namna serikali ya awamu ya tano ilivyokuwa ikifuatilia, tunashangaa ilikuwaje pesa husika ikakwapuliwa. Hata hivyo, wanaojua alikochomolewa Kakoko, hawashangai kwanini aliweza kupona na kuendelea na wadhifa alio nao wakati alionyesha wazi kupwaya tangu alipoteuliwa. Ama kweli, kila zama na kitabu chake. Aliwahi kusema ustaadh Ali Hassan Mwinyi.  
            Waliofuatilia tuhuma za Kakoko na namna zilivyomalizwa, kwa kuangalia kashfa inayomkabili, hawatashangaa. Kwani, alipotoa madai bila kuyathibitisha, alithibitisha utatanishi na kutoaminika. Kisheria, mtoa madai huwajibika kuthibitisha madai yake kwa kutoa ushahidi. Je hao waliomtishia Kakoko kutaka kulinda ufisadi kwenye mita za kupimia mafuta ni akina nani na ndio waliosababisha wizi wa hii fedha iliyosababisha asimamishwe kazi? Kakoko anapaswa kuwataja ili watanzania wawajue wanaotaka kuwakwamisha ukiachia mbali rais kuwajua na kuwatumbua haraka iwezekanavyo?
            Kwa vile sasa kashfa imegusa ulaji wake, Kakoko awataje haraka ili kuondoa mazoea ya baadhi ya wakubwa kutumia dhamana ya umma kutoa madai mazito juu ya mambo nyeti bila kutoa ushahidi; mbali kuokoa ulaji wake. Kipindi alichotoa madai husika sawa na wengine, yalianza kujengeka mazoea ya ajabu ambapo baadhi ya watu walijiona kama wasiogushwa. Bila kutoa maelezo na ushahidi, Kakoko anatukumbusha kilichotokea wakati fulani aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Paul Makonda alidai kutaka kuhongwa milioni 50 kwa mwezi ili aruhusu shisha liuzwe ukiachia. Mpaka anaondolewa ofisini, Makonda hakuwahi kuwataja waharifu waliotaka kumhonga; akashindwa kuwachulia hatua wakati sheria iko wazi: atoaye  na apoekeaye rushwa ametenda kosa la jinai; anapaswa kuchukuliwa hatua kisheria. Hata hivyo, kwa wanaojua watoa madai walivyofumbiwa macho kufikia kiasi cha kujisahau, hawashangai kwanini hakuchukuliwa hatua. 
            Mbali na Makonda, Waziri aliyeshughulikia  ardhi naye aliyewahi kutoa madai kama haya bila kutoa ushahidi kuwa kuna walanguzi wa ardhi walitaka kumhonga mabilioni ya shilingi bila ya wahusika kuwataja waliotaka kufanya hivyo. Kama Makonda, vyombo husika havikumbana mhusika kutoa ushahidi ili kuwashughulikia wahusika. Nadhani hili linapaswa kubadilika mara moja. Tuache kufanyia kazi mazoea wakati mambo yanaweza kubadilika wakati wowote kama ilivyotokea na kuanza kuonyesha.  Ni ajabu kuwa hata vyombo vinavyoshughulikia jinai kama hizi vilikaa kimya bila kutoa maelezo ni nini kilifuatia na nani walitaka kutenda makosa haya. Je hawa wakubwa waliotoa madai bila kutoa ushahidi si washirika wa wale waliowatuhumu hasa ikizingatiwa kuwa waliamua kuficha majina yao kwa faida wajuazo? Je ni vibaya kumkumbusha rais SSH kuwaangazia macho au kutowaweka au kuwabakiza kwenye serikali yake? 
            Je kuna akina Kakoko wangapi kwenye mashirika yetu ya umma ambao bado kashfa zao hazijafikishwa kwa mheshimiwa rais? Lazima tujulishwe wizi huu ulivyoweza kufanyika tangia lini na unahusisha akina nani hawa ambao ni wanjanja kiasi cha kuipiga chenga serikali iliyosifika kwa kupambana na ufisadi? Hili ni muhimu ili kujua mbinu na sababu zilizofanya wasichukuliwe hatua  mbali mbinu walizotumia. Je pamoja na ushupavu wake, kuna mahali ambapo serikali ya awamu ya tano ilikuwa ikizidiwa kete au kuna namna? Ilikuwaje akina Kakoko wakanusurika; na je wako wangapi na wameishalisababishia taifa hasara kubwa kiasi gani? Haya ndiyo maswali tunayopaswa kujiuliza na kujibu kwa usahihi haraka sana ili kuweza kufichua uoza mwingine ambao ulishindikana kwenye awamu iliyopita.
Kwa wanaokumbuka kashfa ya Chavda wakati wa utawala wa awamu ya pili, watakubaliana nasi kuwa kuna wakati mwingine kunakuwa na watu wachache wanaoweza kujihusisha na kashfa na kuwapiga chenga wakubwa wao. Tuchukue fursa kuionya awamu ya sita kujufunza tokana na kashfa kama hizi ili kuepuka kurudia makosa. Je hawa waliosababisha wizi wa mabilioni yanayodaiwa kuibiwa ni wale wanasiasa wakubwa ambao Kakoko aliwahi kuwatuhumu bila kuthibitisha madai yake ima kwa hiari au kwa kulamishwa na sheria? Je ilikuwaje alipotoa madai kama haya, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKURURU) ilizuiliwa na nani au nini kumhoji? Je bado TAKUKURU ambayo ilishindwa kumhoji Kakoko bado ina udhu na uwezo wa kumhoji na ikaufikia ukweli bila kupata kigugumizi kama ilivyokuwa pale alipotoa madai? Hili nalo rais anapaswa kuliangalia na kujua ni kwanini TAKUKURU ilishindwa kumhoji Kakoko ili awataje waharifu waliotaka kumkwamisha.
          Madai ya Kakoko, sawa na ya Waziri na Makonda, kwa wakati ule, yaliweza kuonekana kama poroja za kisiasa za kutafuta umaarufu. Maana, wahusika waliendelea na nyadhifa zao pamoja na kutoa madai mazito  ikiwamo kukalia taarifa nyeti ambazo zingeweza kusaidia mamlaka kupambana na ufisadi.  Tunaamini kuwa rais SSH anajua kadhia hizi vizuri ikizingatiwa alikuwa sehemu ya awamu ya tano ingawa hakuwa na mamlaka ya kuweza kuwashughulikia wahusika sawa na ambayo anayo sasa. Sijui kama rais au wasaidizi wake walisoma au wanakumbuka kashfa hii. Je kama wanaijua, watangoja au watazuiwa na nini kuchukua hatua ili kuepusha dhana ya kulindana? Sitaki niamini hivyo. Hata hivyo, tokana na unyeti wa kashfa husika, naamini wahusika wote watapata taarifa juu ya namna umma tunavyofanyia kazi madai yao. Haiingii akilini kwa watendaji wanaojua wazi kuwa walichoambiwa kufanya ni jinai kukaa kimya bila kuwa na maslahi binafsi au mapungufu kiutendaji. Hata kama wahusika walikuwa vipenzi na jamaa za waliowateua, wanapaswa kushughulikiwa ili kuuonyesha umma wenye watu wenye akili kuwa tunatenda haki kwa wote. Wahusika wanapaswa kujua umma wa wa-Tanzania si mazuzu wala wasahaulifu. Ndiyo maana makala kama hii inatoka ili kumpa fursa adimu rais kuyajua mawazo ya watu wake ambayo kuna kipindi hayakuwa na nafasi ya kusikika tokana na sababu mbali mbali.
            Tumalizie kwa kumuonga rais SSH kuzidi kupiga kurunzi ili awanase akina Kakoko wengine ambao wengine wamo kwenye ofisi yake mbali na wale walioko nje lakini wakiwa wamenufaika na fedha za umma kupitia rushwa au wizi kama ilivyowahi kudaiwa bila kutolewa ushahidi. Je wahusika walikatiwa chao wakaamua kunyamaza? Je walikuwa wakitafuta kiki? Je ilikuwa haki kufanya hivyo bila kuvunja sheria? Kwa vile kesi za jinai huwa hazifi, tunashauri wahusika wabanwe wawataje wahusika na waleze ni kwanini walishindwa kuwataja wakati wakijua fika walikuwa wakivunja sheria. Pia wachunguzwe utajiri walio nao kama unalingana na stahiki yao. Muhimu, tunamshauri rais awe mwepesi wa kuwatumbua watendaji ambao bado wako serikalini waliotoa tuhuma bila kuzithibitisha kwa vile inaonyesha walikatiwa kitu wakaamua yaishe. Pia kuna haja ya kuitaka TAKUKURU ijieleze ni kwanini haikushughulikia kashfa hizi wakati zilikuwa na harufu ya wazi ya rushwa na vitendo vya kibadhirifu. Inabidi, ikiwezekana tubadili sheria zetu ambazo zinaumiza vibaka huku zikiwaendekeza mibaka.  Wakati wa kuwashughulikia akina Kakoko wengine ni huu. Shime rais SSH. Tunakuamini.
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: