The Chant of Savant

Monday 15 March 2021

WAPINZANI WANAPO MMISS MAGUFULI!

 


Kuna usemi maarufu kuwa siasa ni mchezo mchafu. Kuucheza vizuri, wakati mwingine, inahitaji kila mbinu za uchafu na uchafuzi kama ilivyojibainisha hivi karibuni. Gazeti la the Daily Nation la Kenya limekuwa likimnukuu naibu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu anayeishi Ubelgiji akitoa madai na taarifa hata bila ya hata chembe ya ushahidi kuwa rais John Pombe Magufuli yu mahututi na alikuwa amelazwa nchini Kenya na baadaye India kabla ya kupelekwa Ujerumani. Hata kuku na ubongo wake mdogo, hawezi kukubali kusema eti Magufuli alipelekwa Kenya nchi ambayo tuna ugomvi nayo kibiashara ukiachia mbali kutumiwa na mabeberu tangu uhuru. Hili la India linachekesha. Magufuli ambaye amekuwa akipiga kelele na kuhakikisha anajenga mahospitali ili kupunguza gharama na kashfa ya kupeleka wagonjwa India aende India? Kwanini hakumpeleka mkewe au mama yake wala dada yake walipoumwa. Hawa inaonekana hawamjui Magufuli vizuri.  Japo kuugua ni jambo la kawaida kwa binadamu na rais kutoonekana hadharani, kwanini sasa Lissu ameamua kumtambua Magufuli ambaye aliapa hatamtambua baada ya kumbwaga kwenye uchaguzi? 
            Kwanini Magufuli amekuwa lulu kwa Lissu na washitili wake kipindi hiki ambapo tunaambiwa na wasaidizi wake kuwa ni buheri wa afya? Marais kutoonekana hadharani ni jambo la kawaida. Wapo wanaoshindwa kuonekana hadharani kwa sababu ya kuumwa. Wengine hufanya hivyo kupima imani ya wananchi kwao. Wengine huwa wako kwenye shughuli binafsi mbali na utawala ambazo, hata hivyo, haziwazuii kuongoza nchi kikatiba.
            Kutoonekana kwa Magufuli kwa takriban wiki moja mbona si mara ya kwanza? Mwanzoni wa mwaka jana alijichimbia kijijini kwake kwa kitambo na watu wakaanza kuzusha kama kawaida. Rais wala hakujitokeza hadi muda wa kufanya hivyo ulipowadia. Hata ukimya na kutoonekan kwa sasa kwa Magufuli kusiwasumbue bure wapinzani. Ataibuka wakati ukifika na kuwafanya watafute jingine la kushikilia. Muhimu, nawashauri akiibuka basi akina Lissu wafanye uungwana, wamtambue kwa vile kwa sasa wanaonekana kummiss. Kama kweli anauma, akipona au lolote kutokea, kwani kuna atakayeishi milele? Tumuombee apone kama anaumwa na kama ni mzima basi tumuombee ila ukimya nao unachosha. Hapo ndipo wapinzani wana hoja kuwa rais si binadamu bali rais ambaye ni mali ya kila raia.

No comments: