The Chant of Savant

Monday 29 March 2021

Bashiru, Heri Kunyamaza Ule Vinono Kimya Kimya

Kitendo cha Mheshimiwa rais  hayati Dkt John Pombe Magufuli kumpata mtu wa kuziba nafasi ambayo kilikuwa kikimnyima usingizi kwa kumteua Balozi Dkt Bashiru Ally tena muda mfupi, kama alivyokiri Marehemu.  Hii inaonyesha namna mteuliwa anavyofaa au kuaminiwa na mamlaka husika. Japo kuteua na kutengua uteuzi ni wajibu wa kawaida wa Rais, nafasi husika siyo lelelmama tukizingatia umuhimu wake kwa taifa hasa kumuunganisha Rais na kila anayetaka kuonana naye. Kimsingi, nafasi hii ni dirisha au mlango wa kuingilia Ikulu. Hii ni nafasi inayohitaji mtu makini na mwaminifu ambaye anaweza kusema hata hapana kwa mtu ambaye hukumtegemea. Inahitaji mtu anayejua kupima mambo na kutoa majibu kwa kuzingatia mizania ya haki.
         Tukiangalia aliyeteuliwa kushika wadhifa huu mzito na kuvaa viatu vikubwa vilivyoachwa na marehemu Balozi John William Kijazi–––ambaye aliutosha vilivyo wadhifa huu kiasi cha kuwa vigumu kupata wa kumrithi hadi kifo kinamchukua–––kinaonyesha namna Magufuli alivyomuamin Balozi Ally. Maana viatu alivyovishwa ni vikubwa mno kwa mtu ambaye hana historia kubwa ya utumishi wa umma. Isitoshe, wengi walidhani Balozi Ally angekataa uteuzi huu kama tutamkumbusha nadhiri yake mbali na kutokuwa na uzoefu ingawa hakufanya hivyo. Hata hivyo, kwa sasa anaweza kujiengua ili aendelee kuaminika kwa watanzania kama kiongozi wa umma. Tunajua, huenda alilazimika kukubali cheo hicho tokana na woga wake kwa hayati Magufuli. Ndiyo maana, tunamshauri afikiri mara mbili chini ya rais Samia Suluhu Hassan (SSH) ili kulinda heshima yake na ya rais. Ni ushauri tu tena wenye nia nzuri toka kwa mwananchi wa kawaida ambaye anaweza kuwakilisha namna wanavyomuona wananchi wengine wa kawaida.
Hata hivyo, tangu alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Ally ameonyesha ujasiri na umakini wa hali ya juu kiasi cha kujizolea sifa hadi Rais Magufuli kumpandisha cheo kwa kumteua kuwa Balozi na Katibu Mkuu kiongozi. Hivyo, Balozi Ally aliteuliwa kunaziba nafasi ambayo  Rais alisikika wakati wa maombolezo ya Balozi Kijazi akikiri kuwa alitaka kumteua mtu mwingine baada ya  Balozi Kijazi kufikia umri wa kustaafu lakini hakumpata hivyo kumuongezea muda Marehemu Kijazi.
Kama alivyomueleza Rais, Balozi Kijazi hakuwa mpayukaji wala mtu wa kujisemea bali kuchapa kazi kimya kimya kwa kuzingatia viwango. Alikjuwa simba mla nyama na siyo mbwekaji. Kwa kukopa maneno ya Mheshimiwa Jaji Mkuu, Profesa  Ibrahim Hamis Juma, Balozi Kijazi alikuwa ni mtu wa kufuatilia hata mambo madogo madogo ambayo mtu asingeyapa umuhimu asijue ni ya muhimu. Jaji Mkuu alisema kuwa alipomwambia kwa kiingereza kuwa the devil is in the details yaani shetani yuko kwenye vitu vidogo vidogo, Balozi Kijazi alisema God is in the details akimaanisha kuwa hata kwenye mambo tunayoona si muhimu kwa Mungu yanaweza kuwa makubwa na muhimu. Mbali na hiyo, Rais Magufuli alifichua siri kuwa alipomfahamu Balozi Kijazi, aligundua kuwa alikuwa mtu mwaminifu na mwenye kujua namna ya kuwasimamia wa chini yake na fedha za umma. Hizo ni tunu ambazo Balozi Ally anapaswa kuanza kuzifanyia kazi. Kwa kuzingatia umakini na sifa za Balozi Kijazi–––kama mrithi wake ataamua kuzifanyia kazi–––hana haja ya kupewa pole bali hongera. Hivyo, hapa sijui nimpe hongera au pole. Sijui. Ngoja tuone utendaji wake.
Najua Balozi Ally siyo Balozi Kijazi hasa nikizingatia historia za utendaji wao. Utendaji wa Balozi Kijazi ulielezwa vizuri na Rais pamoja na Jaji Mkuu. Utendaji wa Balozi Ally mbali na ule uliotajwa kwa kutukuka hapo juu, unaelezewa na yeye mwenyewe. Kwa mfano, alipo teuliwa kuwa Katiba Mkuu wa CCM, Balozi Ally alisikika akiutangazia umma kuwa katu hangegombea au kukubali uteuzi wowote. Alisema “cheo hiki ni kikubwa mno [Ukatibu Mkuu]heshima hii niliyopewa ni kubwa mno. Ndiyo nafasi yangu ya kwanza na ya mwisho katika uongozi wa nchi hii. Sitagombea  nafasi yoyote na sitakubali uteuzi wowote baada ya nafasi hii. Huu ndiyo utamaduni wa CCM.” https://www.youtube.com/watch?v=qiI_bAVXrec 
        Ushahidi wa maneno haya umejaa kwenye mitandao baada ya kurushwa punde tu alipotangazwa kuteuliwa kuwa Katibu Kiongozi. Hatujui kama Balozi Ally alijisemea kwa utani au kwa sababu ya furaha ya kupata nafasi ambayo hakuwahi hata kuifikiria wala kuipigania. Kimsingi, Balozi Ally alisahau kuwa Rais ana mamlaka ya kumteua au kumtuma yeyote wakati wowote katika kazi yoyote kwa mujibu wa sheria.  Hata hivyo, kauli hii inamuweka pabaya linapokuja suala la kuaminiwa na umma tena tokana na maneno yake mwenyewe bila kulazimishwa na yeyote. Kama mhusika hayuko tayari kama alivyowahi kuapa, basi, kistaarabu anaukataa uteuzi. Je hapa mhusika alijesemea, kupitiwa, ‘kupayuka’ au kuonyesha uanagezi na kutokujua kwake? Je atakaposoma makala hii atakuwa tayari kutoa ufafanuzi wa kutangua nadhiri yake au kujinyamazia ili kufunika kombe? Je hii inamuonyesha kama kiongozi wa aina gani mbele ya jamii? Je hii inatoa taswira gani kwa vijana wetu ambao ni warithi wetu karibu katika kitu ukiwemo uongozi? Je tumejifunza nini?
        Hata hivyo, Balozi Ally ni binadamu tena mwanasiasa japo hataki kuitwa au kujulikana kama mwanasiasa asijue kuwa kila mwanadamu ni mwanasiasa ima kwa kutaka au kulazimika. Kimsingi, Balozi Ally  hakujua kuwa alikuwa akijipalia mkaa na kuingia kwenye anga ambazo, kimsingi na uzoefu, hazikuwa zake. Ndiyo maana tunamkumbusha maneno yake na kumtaka ajiwajibishe ili kulinda ithibati yake kama kiongozi wa umma.  Aliuambia umma wazi wazi kuwa siyo sifa ya CCM kuwa wala kukubali wala kutamani vyeo vingi. Hapa lazima Balozi Ally akubali kuonja adha ya kuramba matapishi yake baada ya kujisemea kana kwamba angekufa kesho yake. Wakati mwingine, ni bora kujinyamazia na kula vinono kimya kimya kuliko kupiga kelele au kukufuru usijue ya kesho. 
        Wahenga wetu walituasa: Hujafa hujaumbika. Ombaomba hata machinga anaweza kuwa lolote hata mteule.  Licha ya nadhiri tanguliwa za Balozi Ally kuwa somo na onyo kwake asijisemee tena, ni somo kwa walio wengi ambao hufanya au kusema mambo bila kuangalia kesho. Balozi Ally si wa kwanza wala wa mwisho katika kadhia hii. Rais Yoweri Museveni wa Uganda, mwaka 1986 akiingia madarakani alisema kuwa tatizo la Afrika siyo wananchi bali viongozi wanaong’ang’ania madarakani. Miaka karibia 40 tangu aseme haya, muulize hali ikoje. Kila mtu anajua pia hata mhusika.
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: