How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Monday 28 December 2015

Magufuli amefika wakati muafaka ila anahitaji nguvu ya kimfumo


            Ujio wa rais John Pombe Magufuli una somo moja kubwa. Amefika wakati muafaka. Wengi –baada ya taifa letu kutekwa na mafisadi –walifikia mahali kukata tamaa wakihoji kama kuna mtanzania atajitokeza na kuondosha mfumo huu fisadi na mchafu wasijue kilio chao kilikuwa kimesikika. Hata hivyo, pamoja na ujio wa Magufuli ulioonyesha aina mpya ya utawala ambao taifa liliukosa baada ya kung’atuka baba wa taifa marehemu Mwl Julius Nyerere, ujio huu hautakuwa na maana kama utaendelea kuwa kile ambacho waingereza huita one man show yaani utawala wa mtu mmoja na si taasisi. Kuondokana na hofu na kuweza kuwa na mfumo endelevu, lazima rais Magufuli ajikite kwenye kubadili mfumo kwa kuufumua na kuufuma upya ili uweze kuwa endelevu na unaojitegemea. Nchi za magharibi zimetuzidi kwa hili. Kwani, nchi hizi zimefanikiwa kutokana na kuendeshwa na mfumo wa kitaasisi badala ya kutegemea busara na juhudi za mtu mmoja.
            Kufumua na kufuma mfumo kuna faida nyingi mojawapo zikiwa:
            Mosi, mfumo mpya endelevu na unaojitegemea utawezesha kuondoa utegemezi wa mawazo ya mtu mmoja ambayo wakati mwingine yanaweza kutokidhi mahitaji na matarajio ya umma.
            Pili, mfumo wa kitaasisi endelevu hupunguza motisha kwa wale wanaoathiriwa na sera za mhusika kiasi cha kutaka kumdhulu. Ukiwa na mfumo uliojengeka kitaasisi, hakuna mtu mwenye akili anaweza kupoteza muda wake kutaka kumuondoa au kumuua kiongozi wa mfumo kwa vile anajua kuwa hata mhusika asipokuwepo mfumo utajiendesha. Hapa ndipo umuhimu na ulazima wa kurejesha rasimu ya Katiba Mpya ya jaji Joseph Warioba iliyouawa na utawala kidhabi uliopita unapojitokeza.
            Tatu, unapokuwa na mfumo endelevu na toshelezi, hata kiongozi wa nchi akimaliza muda wake au hata kufariki, mfumo bado utajiendesha na kufikia malengo yaliyotarajiwa na kudhamiriwa.
            Nne, unapokuwa na mfumo endelevu na wajibika wa kitaasisi, hata vishawishi kwa watu wachache wanaotaka kuutimia mfumo kujineemesha kwa kuhujumu wengine inatoweka. Mfano, nani anaweza kuotea kupindua serikali za Marekani, Kanada, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani? Kutokana na kuwa na ithibati ya kitaasisi, hakuna mtu anayeweza kuota mchana akapanga kupindua serikali za namna hii. Mfumo huu huondoa hata utegemezi wa jeshi jambo ambalo hutoa mwanya wa ufisadi kwa wakubwa wa kijeshi kwa vile wanajua wanaogopewa wanaweza kuondosha serikali.
            Tano, mfumo endelevu hautegemei sera za chama bali misingi iliyowekwa kimfumo ambao hulazimisha vyama vya siasa kushindana kuongoza nchi na kutekeleza mahitajio na maelekezo ya mfumo.
            Je kwanini wenzetu waliamua kujenga mfumo badala ya watu? Jibu ni rahisi kuwa walitaka kuepuka utegemezi wa mtu mmoja ambaye anaweza kuchoka, kuugua hata kufariki wakati nchi haifi wala kuugua.
            Kwa kuzingatia umuhimu wa kuufumua (deconstruction) wa mfumo na kuufuma upya (reconstruction) tunahisi kuwa ni rahisi kuurekebisha na kuuboresha mfumo mbovu kama wetu. Kifalsafa unachofanya ni kufanya mambo kinyume na mfumo mbovu uliopo. Kwa kiingereza anaweza kusema, you just turn the current system upside down. Kama tatizo –kwa mfano –ni ukubwa wa serikali, unaunda serikali ndogo. Kama tatizo ni ukosefu wa maadili, unarejesha maadili huku ukizidi kusambaza mamlaka kwenda kwa umma. Mfano wa hivi karibuni ni vipengele vilivyotaka wabunge na viongozi wengine wa umma watakaoshindwa kukidhi matarajio ya waliowachagua kuwawakilisha kuondolewa kwenye nafasi husika. Huu utaratibu licha ya kuwa wa kiwajibika, ungechochea utendaji wa hali ya juu kwa wahusika kwa vile wanajua wasipofanya hivyo wataondoshwa bila kungoja wafikie ukomo wa mamlaka yao kama ilivyo sasa. Kimsingi, dhana hii ni ya kimapinduzi inayomuweka jaji Warioba mbele ya wakati wake.
            Hivyo, kusisitiza ni kwamba bila kufufua mjadala wa Rasimu ya Katiba Mpya, rais Magufuli atakuwa anatwanga maji kiasi cha kuwapa cha kusema wakosoaji wake kuwa anatafuta umaarufu na kujenga utawala wa muungu mtu jambo ambalo si kweli.
            Kuna haja ya kujifunza toka kwenye nchi zinazosumbuka na kutegemea utawala wa mtu mmoja kiasi cha hata kubadili katiba ili kumpa nafasi ya kuendelea kuongoza kinyume cha sheria kana kwamba hatakufa wala kuishiwa. Kwa vile rais Magufuli amekuja na staili ya kinyenyekevu ya kufanya mambo bila mbwembwe, tunamshauri afufue mchakato wa Katiba mpya. Tutamaliza kwa kunukuu maneno ya aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Kukusanya maoni ya wananchi jaji Warioba aliyekaririwa hivi karibuni akisema, “Huwezi kuwa na mabadiliko kama hauna maadili kwenye katiba, lazima kuwa na separation of power (kutenganisha madaraka) naamini na kanuni hizi zitaingia kwenye katiba mpya.” Asemayo Warioba ni kweli kuwa huwezi kuwa na mfumo wa uwajibikaji bila kuwa na maadili kwenye katiba ambayo hukupa nguvu na uhalali wa kuchukua hatua. Bila kuwa na miiko na maadili kwenye katiba, itakuwa vigumu hata kuwashitaki watuhumiwa –kwa mfano –wa uhujumu wa taifa.
Chanzo: Dira Desemba, 2015.

No comments: