The Chant of Savant

Saturday 12 December 2015

Mlevi kuomba kukutana na rais







Baada ya kupiga kanywaji na tubangi kidogo kusherehekea ushindi wa ki-Tsunami wa Dk Kanywaji, nimepata wazo tena kubwa litakalosaidia kaya yetu. Ninapanga kuomba kukutana na Dk Kanywaji ili nimpe shule ya bure kuhusiana na utendaji wake na kipi afanye kuweza kufanikia. Kabla ya kusahau, kwanza, nampongeza Dk Kanywaji Makufuli kwa kuteua waziri mkuu toka nje ya mitandao ya kijambazi iliyotamalaki kwenye Chama Cha Maulaji (CCM). Baada ya kutoswa akina Makambale, Billy Lukuuvi, Mwiguu Michembe na walaji wengine na kuibuka na Katelephone Majaliwa, nilishehekea kama sina akili nzuri. Nani alitaka viraka na vibaraka wa utawala barakara uliopita? Nilisikia watu wakipiga domo kuwa njemba kama Lukuuvi anayetuhumiwa kughushi sifa za kisomi naye angeteuliwa. Mbona ningehamasisha walevi kuingia na kulala mitaani kuanzia ikulu hadi Kibaha. Hayo tuyaache.
Ngoja nijikite kwenye hoja. Nina sababu kibao za kutaka kukutana na lais Kanywaji.
Kwanza, nataka kumuonya aachane na tabia ya kuvamia maofisi akidhani wabangaizaji na wavivu watajirekebisha na kuchapa kazi. Je atatembelea ofisi ngapi kwenye kaya yenye utiriri wa wizara, mikoa, wilaya tena visivyo na tija kwa kaya?
Pili, namtaka abadili mfumo badala ya kungoja mfumo ujibadili au kumbadili. Ni simpo. Kama akitaka utendaji kazi uwe mzuri, awaite wa chini yake na kuwapa maagizo nao wawape wa chini yao hivyo hivyo hadi kwa mtu binafsi.
Tatu, unda serikali ndogo ya watu safi na wachapakazi uone mambo yatakavyokwenda. Badala ya kupoteza nguvu na muda kuvamia maofisi, wewe unda serikali ya hoja utaniambia. Pia katika kuunda serikali ndogo na chapakazi hakikisha makapi ya utawala habithi uliopita yanapigwa chini. Kuna damu mpya kwenye wigo wa kuteua mawaziri. Kama huwaoni nipige ofa ya gongo nikutajie kibao ninawajua na kuwaona.
Nne, chunguza mianya iliyokuwa ikitumia kuibia kaya. Mfano, angalia uchochoro wa wafanyakazi hewa, walioajiriwa kwa kujuana tunaowajua waliojazana kwenye balozi zetu, mahakama, kwenye bodi za ulaji za mashirika. Fanya kama ulivyochachafya Muhimbili.
Tano, jenga utaratibu wa wakuu wa vitengo, idara na wizara kutoa taarifa za kila mwezi za utendaji wa kazi wa maeneo yao baada ya kuanzisha utaratibu mwingine wa kuweka malengo ya muda mfupi na mrefu wa utendaji kwenye maeneo husika.
Sita, rekebisha mishahara huku zikitungwa sheria za kuwataka wafanyakazi wa umma kutangaza mali zao. Uanze wewe na bi mkubwa wako ndiposa wengine wafuate bila kuangalia nyani usoni. Wahenga walinena kuwa hisani huanzia nyumbani na jogoo aliwafundisha vifaranga kunya ndani.
Saba, Anza kutekeleza ahadi lukuki ulizotoa huku ukijikita kwenye vipaumbele ambavyo napendekeza iwe ni katiba mpya, kupambana na ufisadi, kurekebisha mikataba ya kijambazi ya uwekezaji ambao walevi wanaona ni kama uchukuaji na si uwekezaji na kufufua wizara ya Elimu kwa kufutilia mbali utaratibu wa sasa wa kizembe uliopunguza vitabu kwa ajili ya wanafuzi.
Nane, mulika sheria na utaratibu wa manunuzi wa vifaa vya umma. Huko ndiko ulaji uliopo ambapo wezi wenye madaraka huunda makampuni ya kuyapa tenda za usambazaji serikalini. Rejea kilichotokea kwenye TANESCO ambapo bosi wa zamani alikuwa akimpa tenda bi mkubwa wake na kulipwa kwa huduma mbovu au bila hata huduma.
Tisa, bana matumizi ya lisirikali. Kama ulivyopiga marufuku matanuzi ughaibuni, hakikisha unazuia manunuzi ya samani feki toka ughaibuni, ununuzi na matumizi ya mashangingi na hata ununuzi wa mafuta kwa magari ya serikali.
Naona kanywaji kameisha mezani. Acha nimuite muuza aniwekee vitu nifikiri jinsi ya kukusaidia kuwatawala wadanganyika wavivu na wasanii. 
Chanzo: Nipashe, Desemba 12, 2015.

No comments: