Magufulification: Concept That Will Define Africa's Future and the Man Who Makes Things Happen

Magufulification: Concept That Will Define Africa's Future and the Man Who Makes Things Happen

Saturday, 19 December 2015

Mlevi aunda baraza lake la mawaziri mbadala


             Baada ya kuupiga na kusoma sura zilizoko kwenye baraza la ulaji aliloteua mkuu JMP, nami nimeamua kuunda baraza langu ili kuonyesha alivyokosea katika kuunda lake. Nafanya hivi kuonyesha nilivyo na hasira jinsi alivyoacha nje wachapakazi ambao kama angewateua hii kaya ingepaa kama Airbus 380 kwa kusheheni maendeleo.
             Baada ya kutupa kipisi cha msokoto nakohoa kidogo na kuwapigia simu waandishi wa umbea waje kuzinyaka ili wawafikishie walevi. Punde si punde ofisi yangu imesheheni waandishi wa umbea na makanjanja.
            Kwa mikogo natoka chumbani tayari to face the press kama wasemavyo wakameruni wa kwa mama. Nakohoa kidogo na kuwaamkua waandishi na makanjanja tayari kuanza shughuli.
            Naanza, ndugu waandishi wa umbea na makanjanja. Kwanza leo hakuna mshiko na mwenye kiu anaweza kwenda kwenye bomba akanywa maji bili nitalipa mimi.
            Bila kuwachelewesha nataka nitangaze baraza langu la ulaji litakalonisaidia kusafisha kaya hii iliyonajisiwa na mbu na mapanya wa Njaa Kaya. Pia nataka niuleze umma wa walevi kuwa awamu yangu ni sasa kula tu. Hivyo, lazima kuunda baraza la gendaeka wanaojuka kukatua. Bila kupoteza muda wafuatao ndiyo watakuwa wasaidizi wangu katika kuendesha ulaji wa kaya hii tukutu.
Waziri mkuu na himaya tawala Jan Makambale.  Huyu atasimamie himaya tukufu akisaidiana na vitegemezi vya wazito vilivyojazana Bell of Tembo (BoT) kuhakikisha maslahi ya wanene hayachezewi na toboa toboa na panya wasio vitegemezi vya vigogo.
Waziri wa uwekezaji, uchukuaji na Kagoda na EPA Roast tamu Aziz. Huyu atasaidiwa na naibu waziri Mohmood Deweji. Tokana na umahiri wao wa kutumia kaya kuwa mabilionea, naamini wanene wote hadi namaliza ngwe yangu watakuwa mabilionea wa kunuka.
            Napiga chafya na kuendelea, Waziri wa njuluku, fedha na fedheha escrow na utoroshaji mitaji Setii Singasinga. Huyu atasaidiwa na manaibu wake Sada Mkuyati na Mwiguu Michemba. Kutokana na kazi pevu waliyoifanya kwenye utawala uliopita ambapo mapato ya kaya yalikuwa kiduchu kutokana na kuruhusu miradi na biashara za wanene zisiguswe lazima niwaongezee ulaji ili wazidi kuongeza pato la wanene.  Anayefuata ni Waziri wa nishati na madini, Escrow na uwezeshaji wa madili Profwesa Sossie Muongo huyu ahitaji naibu kwani akisaidiana na akina Setii na Rugemalayer wanaweza kupata makampuni ya kigeni ya kupewa tenda ya kuendesha wizara yake kwa mafanikio kama alivyofanya kwenye Escrow kiasi cha kuwaacha wengi vinywa wazi.
            Natoa leso mfukoni na kujifuta jasho na kuendelea, anayefuatia ni Waziri wa uchukuzi na utoaji takrima Jimmy Rugemalayer ambaye atasaidiwa na Bishop Kilaini ambaye nimemteua kuwa mbunge na sasa nimemteua kuwa naibu waziri.  Huyu vitu vyake vinafahamika hasa alivyoweza kukuza uchumi wake na wa Tanesco kwa haraka sana kiasi cha kuongeza mgao wa umeme ambao ni mzuri kwa utunzaji wa mazingira. Anayefuatia ni Waziri wa mambo ya nchi za nje Jake Kiquette ambaye naibu wake atakuwa mkewe na Mwidini Misupu. Huyu anajulikana anavyoijua kila pembe ya dunia. Hivyo, kutokana na sifa yake ya uvasco da Gama, ataleta sifa kubwa kwa kaya yetu.
            Natabasamu kidogo na kuendelea na kusuka baraza la ulaji. Anayefuatia ni Waziri wa mambo ya ndani, Umar Mahita aka Ngunguri atasaidiwa na Lajabu Hadadi.
Waziri wa afya na vifo Dokta Hussain Muinyi aka Ruxa bin Loliyondo. Anayefuatia ni Waziri wa nyumba makazi na fukwe Yussie Manji atasaidiwa na yule ponjoro mwenye majengo mauaji ya mitaa ya Udosini yaliyolishinda lisirikali lililopita. Anayefuatia katika ulaji huu mtukufu ni Waziri wa ilm, ujinga, kughushi na shahada za dezo Dk Shukuruni Kawa-dog ambaye atasaidiwa na Makorongo Muhanga, na Didias Makalio.
            Natoa msokoto wa ganja na kuuwasha na kuendelea na kutangaza majina mengine. Anayefuatia ni Waziri wa utalii na usafirishaji wanyama Razier Nyalandu   na naibu wake atakuwa Mwidini Ndongara.Waziri wa jinsia na jinsi za kitoto Sofia Lion na naibu wake atakuwa Aisha Kikalio.
Waziri wa kilimo na baa la njaa Steve Wahasira ambaye atasaidiwa na naibu waziri Bill Lukuvi. Baraza la ulaji haliwezi kukamilika bila kutangaza atakayechukua wizara ya kuua katiba mpya. Waziri atakuwa mheshimiwa Sam Sixx ambate atasaidiwa na manaibu  mawaziri Anna Makidamakida na Jobless Nduguy. Anayefuatia ni Waziri wa ardhi na unyakuzi wa viwanja Anna Kajuamlo Tiba-ijuka naibu waziri Gettie Rwakatarehe na Dan son of Jonah. Waziri wa viwanda na ulaji atakuwa mlangira Niziro Kadamage. Na Gavana wa benki kuu atakuwa Prof Benny Ndururu huku mwanasheria mkuu wa lisirikali na mpayukaji atakuwa mura Freddie Werema.

            Wizara za nyeti zilizobaki bado nazitafutia wa kuzikalia wakati wengine wakiendelea kuhomola. Mungu ibariki Danganyika. Wabariki walevi na wadanganyika. Kumbe ninaota siyo!
Chanzo: Nipashe, Desemba 19,2015.

No comments: