Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Saturday 26 December 2015

Mlevi kushitaki sirikali The Hague


            Waraka huu ni ujumbe kwa rais Dk Kanywaji Makufuli kuwa nina mpango wa kuishitaki sirikali yake kwa kuua mjengo wangu niliokuwa nimeshusha bondeni Uswekeni. Kwanini sirikali haitaki kufumua siri kali yote iliyoko nyuma ya sisi wachovu kujenga mabondeni au ni kwa vile tulipouziwa haya mabonde tuliwafukuza vyura ambao juzi walikuwa wakituzomea kwa kurejeshewa makazi yao? Juzi niliangusha jozi baada ya kuona –hata kunguru –walikuwa maghorofani –sorry –kwenye miti wakinicheka kwa kuumbuka tena siku chache baada ya kutoa kura yangu ya kula nisujue nami ningeliwa kinamna.
            Katika hati ya kiapo nitakayowakilisha The Hague kwa bi mkubwa Fatou Bensuda nitataka sirikali inilipe fidia, kuniomba msamaha na kunipa kiwanja kwa wanene ili nami niwe mnene. Pia nitaomba mahakama iamuru sirikali kufumua siri kali ya wale ambao walituruhusu kukaa mabondeni huku wao wakitanua uneneni. Wanadhani tulipenda kukaa mabondeni kama mamba kenge na vyura siyo? Wasingetunyonya na kuvuruga mfumo wetu unadhani tungekuwa tunanyanyasika hivi kana kwamba hatuna kwetu? Hebu Dokta Kanywaji tafadhali, angalia namna ya kutusaidia bila kuwaacha waliotuchuuza wakitanua kwenye ofisi za umma ili zoezi lipoe wawakaange wengine. Heri ungewabana na kuwafilisi na njuluku utakayopata itusaidie sisi wahanga wa ufisadi na uroho na ufisi wao.
            Katika hati nyingine ya kiapo nitaomba ICC iamrishe lisirikali lieleze lilikuwa wapi hadi tunajenga, kuishi, kuzaa hadi kujukuu.  Nitawasilisha ankara zangu za malipo ya umeme, maji na kodi ya mjengo ambayo nilikuwa natozwa kila mwezi. Hapa bado sijaonyesha kitambulisho changu walichonipa kwa anwani yangu ya bondeni ukiachia mbali karatasi ya kupigia kura ya kula kwenye kituo chetu cha Jangwani Bondeni.
            Pia nitaomba jaji aamuru wote waliotuchuuza tukachuuzika nao waadhibiwe kwa kufilisiwa njuluku waliyotutoa kwa miaka yote hii walipokuwa wakiuza viwanja vya mabondeni. Hakuna kilichoniuma kuona wale wale waliotuibia kwa kutupimia viwanja mabondeni kusimamia zoezi la kutudhalilisha. Lazima niiambie mahakama iamuru wataifishwe mali zote walizochuma kwa kutuibia ili njuluku hii itutunze wahanga wakati huu tukijipanga kuanza maisha upya.
            Pia nitaiomba mahakama iamuru na mahekalu ya wanene yaliyojengwa kwenye viwanja vya wazi na maeneo yasiyokubalika kule beach nayo yaporomoshwe huku wakifilisiwa.
Kwanini wanataka kuniadhibu wachovu peke yetu wakati wanene waliokuwa madarakani waliniacha nikaendelea kutesa huku wakichukua njuluku zangu. Sasa nateseka peke yangu wao wakinicheka utadhani hawahusiki.
            Katika hati ya kiapo ya dharura nitaomba mahakama iamuru lisirikali linipangishie kwenye hoteli ya kitalii na kutulipa fidia mimi na bi mkubwa kwa kutunyima usingizi kwa kulala tumekaa kwenye vifusi na penu za wengine. Pia nitaomba mahakama iamuru lisirikali linilipe fidia kwa kunidhalilisha, kunisababishia mateso ya kisaikolojia kama kuchekwa, kuzomewa, kupigwa picha na waandishi wa umbea, kupiga picha vyombo vyangu na vyupi, kutoa picha zangu magazetini na kusomeka dunia nzima bila kusahau kunipunguzia heshima mbele ya walevi. Siwezi kuvumilia udhalilishaji huu. Nilishangaa eti wale wakota walipokuja kuua mjengo wangu waliniuliza hati. Mbona mijengo ya lisirikali haina hati na haibomolewi au kufungisha virago lisirikali lenyewe? Mbona Chama Cha Maulaji (CCM) kina miradi mingi ya kuegesha magari kwenye viwanja vya kuvamia vya umma au hatujui? Ngoja nikusanye nauli niende The Hague. Nitaomba mahakama pia iamuru CCM kuondoka kwenye maneo ya umma ambako imekuwa ikijiingizia mabilioni ya njuluku kwa miaka zaidi ya 30. Nitaomba naye ifilisiwe na wakubwa zake wawekwe sero moja na Chaz Taylor na Laurent Badboys kwa kuwadhalilisha walevi.
            Si haki kutuvunjia mijengo na kutuacha tukilala nje wakati CCM ikiendelea kuingiza mabilioni kwa mchezo ule ule wa kuvamia maeneo ya wazi.  Tena kabla sijasahau, mna habari pale bondeni kwetu tulikuwa na matawi mengi ya vyama vya siasa? Sijui navyo vilivamia kama sisi au ni kujifanya miungu watu na kuwaonea wenzao.
            Hoja nitakazotumia kwenye kesi ya msingi ni:
Mosi, tulipovamia lisirikali lilikuwa wapi? Kwanini halikutuchukulia hatua? Tulipovuta umeme lisirikali lilikuwa wapi? Mbona halikutunyima umeme? Kwanza, walituibia. Umeme wenyewe wa mgao na kulanguana. Hapa lazima walipe fidia tena si madafu bali dolari za kwa Joji Kichaka.
            Pili, nitachezesha mikanda niliyowarekodia wasaka kura wakisema kuwa tusingebughudhiwa.
            Tatu, nitaomba mahakama  izuie lisirikali kuchukua hatua zaidi ili kumaliza kesi ya msingi.
            Ili kunogesha mambo, nitaomba ICC iamuru Dk Kanywaji na Njaa Kaya wafike mahakamani na kuwekwa ndani bila dhamana kwa vile wao–chini ya vicarious liability –wanawakilisha chama na lisirikali.
            Ngoja nitumie fursa hii kuwataka waje wanione mara moja kabla sijakwenda zangu The Hague na kuwakatishia ulaji wao. Wasiniogope. Mie silipizi visasi kama Njaa Kaya aliyemlipizia kisasi mzee Jose Waryuba. Wakija wakaongea vizuri tunaweza kuyamaliza  kiasi cha mimi kuchukua changu na kuacha walevi waendelee kuadhirika.
Ala! Kumbe ni ndoto!  Hata hivyo, jamani jifunze kuheshimu na kufuata sheria. Sasa kazi tu!           
Chanzo: Nipashe, Desemba 26, 2015.

No comments: