Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda si mgeni katika vituko. Baada ya kumshambulia mzee Joseph Warioba, hapo tarehe 2 Novemba 2014 rais mstaafu Jakaya Kikwete aliishangaza dunia kwa kumteua Makonda kuwa mkuu wa wilaya. Hatua hii ilifafsiriwa kama onyo kwa Warioba na wale wote waliokuwa wakipigania Katiba Mpya kuwa wangekomeshwa na mgenge ya wahuni. Wapo waliotafsiri uteuzi wa Makonda kama kulipa fadhila kwa kazi aliyokuwa ametumwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake ikiongozwa na Kikwete. Wengi walihoji busara ya uteuzi huu ambao ulikuwa ni udhalilishaji wa moja kwa moja kwa mzee Warioba.
Wahenga walisema: Mchovya asali hachovyi mara moja; na ukimtukana mzee mmoja utawatukana na wengine. Baada ya Makonda kujihisi kuwa hawezi kuguswa, aliendelea kutembeza ubabe hasa ikizingatiwa kuwa ndiyo zana na nyenzo iliyomfikisha hapo alipo kama tulivyoeleza kwenye sakata la kumshambulia, kumtisha na kumdhalilisha mzee Warioba. Kama vile ilikuwa imepangwa, Makonda aliteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Kinondoni anamoishi mzee Warioba.
Kimsingi, Makonda alizoea siasa za kibabe na kihuni kiasi cha kuzigeuza kuwa ndiyo kanuni ya mchezo wenyewe asijue mambo yamebadilika. Gazeti moja liliandika “Ikumbukwe DC ndiye Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na DSO akiwa katibu wake, sasa mtu kama Makonda ambaye yupo tayari kufanya vurugu yoyote kutetea maslahi ya CCM leo kupewa u-DC wa Kinondoni tutegemee nini uchaguzi mkuu wa Oct 2015?” Kwa vile rais John Pombe Magufuli amepania kurejesha heshima ya taifa na uwajibikaji vya kweli, ni wakati muafaka kumtaka aondoe watu kama Makonda toka kwenye ofisi za umma. Maana, kuwapo kwao madarakani –licha ya kupingana na dhana nzima ya kuwakomboa watanzania –kunazidhalilisha ofisi za umma na kunapingana na hali halisi hasa ikizingatiwa kuwa wengi wa aina hii waliteuliwa kama njia ya kulipana fadhila bila kuzingatia uwezo na sifa za kushika nafasi hizo.
Kuendelea kuwa na watu kama Makonda kutaanzisha vurugu. Chukulia mfano wa hivi karibuni ambapo Makonda aliamuru mbunge wa Ubungo, mheshimiwa Said Kubenea (CHADEMA) kukamatwa kwa vile walipishana lugha na kurushiana matusi. Huu ni ushahidi kuwa Makonda hajui thamani na mipaka ya madaraka yake. Kimsingi, ukuu wa wilaya siyo cheo cha majaribio wala kujaza wahuni na kusababisha kuvunjika kwa Amani. Makonda alikaririwa akimwambia Kubenea, “Unajua mimi ni nani?” Naye Kubenea alikiri kumjibu, “Wewe ni kibaka tu.” Inakuwaje mkuu wa wilaya mzima anakosa adamu na uvumilivu ili kufuata njia zinazohusika kisheria anapovunjiwa heshima? Kama tunakuwa wakweli, nani ni nani kati ya mbunge ambaye ni mwakilishi wa kuchaguliwa na wananchi na mkuu wa wilaya ambaye anateuliwa na mtu mmoja kumwakilisha na si umma? Je wananchi wa Kinondoni wakiamua kusimama na mbunge wao –kama serikali itaendelea kumkingia kifua –je Kinondoni kutakalika? Kwanini Makonda hakuyapima yote haya? Sijui sifa za kitaaluma za Makonda. Hata hivyo , matendo yake yanamuonyesha kama mtu mbumbumbu asiyejua thamani na uzito wa mamlaka yake. Kimsingi, nukuu ya hapo juu kuwa unapompa Makonda ukuu wa wilaya tutegemee nini zaidi ya fujo ina mashiko. Kimsingi, alipopewa ukuu wa wilaya baada ya kumdhalilisha mzee Warioba, Makonda imekuwa ni sawa na chizi kupewa rungu jambo ambalo matokeo yake yanajulikana hata kwa kuku mwenye ubongo mdogo.
Tunafahamu kuwa kuna wakuu wengi wa wilaya na mikoa walioteuliwa ‘kinamna’ wakati hawana sifa wala uwezo wa kushikilia madaraka haya makubwa. Hivyo, rais Magufuli atuondolee aibu na vurugu kwa kuwawajibisha mara moja watu wa namna hii ambao wanajulikana licha ya wao kujijua. Tulizoea kushangaa rais alipokuwa akitangaza uteuzi wa wakuu wa mikoa, wilaya, mabalozi hata baadhi ya majaji wasiofaa. Tulizoea kusikia wananchi wakisema, “Hata na fulani naye kateuliwa!” Ama kweli, ukishangaa ya Warioba utaona ya Kubenea kuhusiana na ubabe wa Makonda ulivyo!
Hatupendi tuonekane tunamsakama Makonda. Ndani ya miezi miwili ameishaonyesha udhaifu usiokifani kuhusiana na nafasi na utendaji wa mkuu wa wilaya. Ni vizuri Makonda akafahamishwa kuwa siasa za kutukana na kutishana au kufanyiana uhuni zimeishapitwa na wakati hasa wakati huu ambapo uchaguzi mkuu umekwisha. Makonda na wenzake walizoea kutumia matusi kuwatukana wapinzani kama mtaji wao bila kujua wananchi wanataka nini. Kubenea amechaguliwa na wananchi. Hivyo –kama mbunge wao halali –anapaswa kuheshimiwa na kulindwa. Inashangaza hata kitendo cha polisi kumkamata na kumweka ndani kwa amri ya mkuu wa wilaya bila kuangalia haki zake kama mwakilishi wa wananchi. Je Kubenea angekuwa mbunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) angekamatwa na kuvunjiwa heshima yake kwa amri ya mkuu wa wilaya anayejulikana kwa sifa na tabia zake za vurugu kama tulivyooneysha hapo juu? Kama Makonda amefikia kuwadhalilisha nguli waliochangia ustawi wa taifa hili kama mzee Warioba, atashindwa kuwadhalilisha wabunge wa upinzani? Je Magufuli anaridhika na siasa za majitaka kama hizi wakati kauli mbiu yake ni kazi tu na kutumbua majipu? Basi tunamuomba rais Magufuli chonde chonde, tumbua jipu hili Makonda.
Chanzo: Mawio Desemba 18, 2015.
No comments:
Post a Comment