Baada
ya kaka Dk Kanywaji kuja juu na kubomoa majumba yaliyojengwa uswekeni,
wanakijiwe wamepokea uamuzi huu kwa shingo upande.
Mpemba anaingia akiwa na ndita
usoni. Baada ya kuamkua anasema, “Yakhe mmepata simu ya Mgosi Machungi?”
Kabla
ya kuendelea, Mbwamwitu anadakia, “Kwani simu yake imepotea au amekupigia?
Unamaanshani Ami?”
Mpemba
anajibu, “Mgosi Wallahi kanpigia simu na kusema eti nyumbaake yabomolewa kesho.
Hivo, anaomba yoyote mwenyeweza kumhifadhi afanye hivo.”
Kapenda
anachukua kirongaronga chake na kumtwangia Mgosi. Mara simu inapokelea. Tunasikia “Hao hamijambo huko?”
Kapende
anajibu, “Sie wazima vipi huko Mgosi? Maana habari tulizopata si nzuri hasa
kuhusiana na ubomoaji wa mjengo wako.”
Mgosi
anajibu, “Ni kwei sote tiiojenga mabondeni timeambiwa tibomoe kabua hawajaja
kubomoa wenyewe.”
“Pole
sana Mgosi,” anajibu Kapende na kukata simu. Baada ya kukata simu kijiwe
kinaanza kujadili zali zima.
Msomi
Mkatatamaa anakuwa wa kwanza kutongoa, “Japo naunga mkono mpango mzima wa
kubomoa majumba yaliyojengwa kinyume cha sheria, lazima niseme wazi,
sikubaliani na kuwaadhibu wahanga peke yao huku waliowasababishia madhira haya
wakisimamia zoezi la ubomoaji.”
Mijjinga
anakula mic, “Hapa Profesa Msomi umenena. Haiwezekani wale waliowaacha watu
wakajenga wasiadhibiwe nao. Maana ukiangalia majengo haya ambayo hayakuota
kimiujiza, unagundua kuwa serikali iliona kila kitu ikajinyamazia bila kutimiza
wajibu wake kwa watu wake.”
Mipawa
anakula mic, “Wewe unaongelea la kuzembea kuwazuia wananchi kujenga mabondeni!
Nani angemzuia nani wakati wazito nao walikuwa kazini wakijipa viwanja na
kuvamia vya umma?”
Mheshimiwa
Bwege anakwanyua mic, “Unadhani sababu ni hiyo tu? Ilikuwaje wahusika wakapewa
maji, umeme na wengine kutozwa kodi za viwanja na majengo kama serikali
haihusiki na balaa hili?”
Msomi
anarejea, “Serikali inahusika japo si awamu ya dokta Kanywaji. Hata hivyo, kuna
haja ya kumtaka Dk Kanywaji kuwapa hifadhi wahanga hasa ikizingatiwa kuwa
makosa ni ya pande mbili. Nadhani jambo la muhimu kufanya ni kuchunguza wote
walioruhusu balaa hili tangu mchezo mzima ulipoanza na kuwachukulia hatua za
kisheria.”
Kanji
anakula mic, “Somi sema juli sana. Ila veve nasahau kuwa mingi ya vatu nakula
juuku likwisa staafu au kufa. Sasa kama nachunguza tasitaki vatu yote nastaafu
au kufa?”
“Wewe
unaonaje?” Msomi anamuuliza Kanji huku akikwanyua kombe lake la kahawa na kubwia
kabla ya kuendelea kuongea bila kungoja Kanji ajibu.
Anakohoa
na kudema, “Tunafahamu wengi wameishastaafu hata kufa. Je mali walizochuma
tokana na jinai hizi nazo zinastaafu au kufariki? Tungeshauri wahusika wasakwe,
wafilisiwe na wengine kufungwa. Maana huu ndiyo ufisadi wenyewe na majipu
ambayo Dk Kanywaji anapania kuyatumbua bila mzaha. Haiwezekani kaya yetu
ikaendelea kuwa shamba la chizi.”
Da
Sofia Lion aka Kanungaembe ambaye alikuwa ameshika tama anaamua kula mic,
“Mwenzenu hata mimi naona kuna namna. Kwani hata mjomba wangu naye amebololewa
nyumba yake aliyojenga zaidi ya miaka 30 iliyopita. Mtu mwenyewe anaumwa vibaya
sana ukiachia mbali kuwa alishafiwa na mkewe. Mzigo wote tumetupiwa sisi. Kweli
nakubaliana nanyi. Kuna haja ya kutenda haki hasa kwa wahanga wa zoezi hili
linalotokana na utawala mbaya.”
Kapende
anakula mic, “Kumbe nawe dada Sofi umeanza kuona mwanga! Siku zote tulipokuwa
tunasema kuwa serikali zilizopita zilikuwa fisadi , ulikuwa ukituona wazushi
usijue kuwa yakikugusa utastuka.”
Mzee
Maneno anakwanyua mic, “Ama kweli hujafa hujaumbika. Nadhani Sofi siku zote
ametetea chama bila kujua nyuma yake kunani. Sasa uchaguzi ndiyo umeishakwisha
na wenye kupeta wamepeta mnadhani kuna atayesikia la mwazini au mchota maji
hapa?”
Mijjinga
naye anaamua kurejea, “Jamani tuwe wakweli. Tuseme ukweli kama alivyosema Dk
Kanywaji kuwa msemakweli ni mpenzi wa Mungu. Watu wetu walizidi sana kiasi cha
kusahau kuwa kuna sheria. Nadhani hapa tujadili jinsi ya kuwasaidia wahanga
binafsi badala ya kuipa mzigo serikali ingawa chama chake kilihusika kwa
asilimia kubwa. Nashauri –kama serikali itatusikiliza –ikamate waliosababisha
maafa haya na kuwafilisi na hiyo fedha iwatunze wahanga wakati wakitafuta namna
ya kusonga mbele.”
“Nadhani
sasa watu watajifunza kuheshimu sheria na kuzifuata huku na mamlaka nayo
yakipaswa kutoacha watu wajenge ndipo yaje kubomoa. Tunatiana hasara na
kuumizana tokana na kutofuata sheria. Somo kubwa nadhani hapa ni kwa wachovu
kujifunza kutii na kufuata sheria badala ya kupenda vya mteremko. Nashauri
tupitishe mchango kwa ajili ya Mgosi na da Sofi lau wapate pa kuanzia wakati
kijiwe kikitafuta namna ya kuibana serikali isiwatupe watu wake iliyowadanganya
kwa muda mrefu nao wakadanganyika.”
Kijiwe
kikiwa kinanoga si akapita meya wa zamani wa Jiji ambaye ni shikaji wake da
Sofi. Acha tumtoe mkuku kabla ya ndata hawajamuokoa. Maana hawa ndiyo chanzo
cha mabalaa yote haya. Na shauri yao. Tukiwakamata watu kama hawa wanaokalia
madaraka bila kufanya kazi tutawafanyia kitu mbaya.
Chanzo: Tanzania Daima Desemba 23, 2015.
No comments:
Post a Comment