Baada ya rahis Joni Kanywaji Magufuli kuteua baraza lake la ulaji, kijiwe kimekaa kama kamati kuelezea kuudhiwa, kustushwa na kupinga uteuzi wa baadhi ya nyuso zilizoleta hasara kwa kaya hii. Si kawaida kijiwe kujadili uteuzi wa mkuu hasa ikizingatiwa kuwa ana mamlaka kisharia kumteua atakaye. Hata hivyo tokana na ukale na uhovyo wa katiba inayompa mkuu mamlaka yasiyo na kipimo, Kijiwe kinataka kuanzisha mkakati wa kumataka mkuu awe anatoa maelezo pale wanakaya wasiporidhika na uteuzi wake.
Mpemba anaingia akiwa hana raha. Anaamkua na kuendelea, “Yakhe nilidhani uteuzi wa hovyo wa kishikaji wa majizi na mafisadi ulikiwsha zama alipokitoa Njaa Kaya nsijue niliku naota nchana! Walahi baada ya kuona nyuso aloteua nkuu nimejihisi kama nasalitiwa walahi.”
“Ami nami sikuamini nilichoona kwenye runinga yangu siku mkuu alipotangaza walaji wenzake. Hakuna sehem ameniudhi kama kumrejesha Profwedheha Sossie Muongo. Sijui kama mkuu anao washauri wanaomtakia mema yeye na kaya yetu kusema ule ukweli,”
anajibu Mijjinga huku akiweka tai yake vizuri.
anajibu Mijjinga huku akiweka tai yake vizuri.
Naye Mgosi Machungi hajivungi, “Waahi hata sisi timeshangaa haya madudu anayoanza nayo mkuu. Hivi wana kaya wamekwisha hadi anatuetea makapi anayotaka kuyasafisha kwa majitaka au ndiyo seikai yenyewe ya majitaka?”
Kapenda anakwanyua mic, “Mi naona kama lisirikali lote ni la Njaa Kaya tofauti ni kwamba anayeongoza Dk Kanywaji. Huwezi kuamini katika mawaziri wote alioteua wake ni wawili tu. Hapa Njaa Kaya kweli hajaongoza kaya kwa mlango wa nyuma?”
Sofia Lion aka Kanungaembe anakula mic baada ya kuudhiwa na shutuma kwa Dk Kanywaji anayeonekana kumzimia kama alivyomzimii Njaa Kaya. Anachonga, “Hivi nyie mmeingiliwa na nini jamani! Mtu hata hajakaa hata miezi miwili mshaanza kumkosoa. Huyo Muongo mnayesema ni makapi mna ushahidi wa ufisadi dhidi yake jamani? Si mliambiwa kuwa yeyote unayemhishi kuwa fisadi upeleke ushahidi kwenye vyombo husika ili vichukue hatua za kisheria.”
Msomi Mkatatamaa hakubaliani na da Sofi. Anaamua kukwanyua mic. “Go tell it to the birds da Sofi. Kaya hii ni ya kupeleka ushahidi wakati ushahidi uko kila mahali. Kama hujui kuwa jamaa ni fisadi basi nawe ni fisadi wa kimawazo. Kwani kashfa ya Escrew ni ya uongo? Je wakati inatokea yeye alikuwa wapi? Mbona mura mwenzake Freddie Werema alitimliwa kama hakukuwa na namna? Nadhani kutakuwa na mafisadi wenye nguvu nyuma ya escrew sawa na wale walioasisi EPA ili kupata njuluku ya kuwahongea wachovu na kumchagua kilaza aliyenajisi kaya yetu kwa miaka kumi.”
Anapiga chafya na kuendelea, “Japo da Sofi hataki tumkosoa mkuu, akumbuke kuwa mkuu ni binadamu kama yeyote anayeweza kukosea hata kuchemsha ukiachia mbali kuweza kuingia majaribuni. Nijuavyo ni kwamba nyuma ya uteuzi wa mafisadi unaweza kuwa umeshinikizwa na chama. Nikiangalia vitegemezi vya vigogo kama vile Jan Makambale, Ninaye Mapepe na Dk Huss Muinyi naweza kujua nani wako nyuma ya zahama hii ya kutujazia viraka vya utawala mbovu uliopita.”
Mheshimiwa Bwege aliyekuwa akisoma gazeti anaamua kula mic, “Profesa Msomi nakubaliana nawe mia kwa mia. Kuna jamaa zangu wa usalama alinitonya kuwa kuchelewa kusuka hii baraza la ulaji kulisababishwa na mvutano baina ya Dk Kanywaji na wanene waliopita ambao walitaka afanye mambo watakavyo siyo atakavyo. Ngoja mtaona spidi yake itakavyoanza kupungua na hatimaye kusahaulika. Jamaa amenitonya kuwa ameshapigwa spidi gavana asitibue ulaji wa wenyewe kwa ushamba wake.”
Mipawa aliyekuwa anatupa kipisi cha sigara kali na kula mic, “Mheshimiwa Bwege usemayo ni kweli. Hata ukiangalia uso wa jamaa wakati akitaja jina la Muongo au hao vitegemezi na vihiyo kama Billy Lukuwi ungegundua kuwa jamaa hakuwa na raha.”
Mbwamwitu anaamua kumchomekea Mipawa hata kabla hajamaliza, “Kwanini atishwetishwe wakati ameishakabidhiwa rungu la ukuu. Si afanye kama Mutharika pale kwa mzee Banda kwa kuunda chata lake na kutosa chata la mafisadi. Kwani chata ni baba au mama yake?”
Msomi anakatua mic tena, “Mbwamwitu umeongea kana kwamba ulikuwa unasoma mawazo yangu. Ninakuunga mkono mia kwa mia kuwa anachopaswa kufanya mkuu kama jamaa wanamletea za kuleta eti awahifadhi awachonganishe na wanakaya waingie mitaani kumuunga mkono atakapoamua kukiaanga chata au kukihama na kuanzisha chata lake. Kwanza, akifanya hivyo hatakuwa na sababu ya kubanwa banwa aonekane kama anajipinga bali kuchanja mbuga huku kaya ikizidi kuneemeka.”
Mijjinga anarejea, “Kwa sisi tuliosoma na Dk Kanywaji hatuna shaka na unachosema Msomi. Ni suala la muda wale waliodhani kuwa jamaa angewakingia kifua watajilaumu huku wakilia na kusaga meno. Jamaa nimjuavyo vinginevyo wamkolimbe au kumsokoine. Na hili watakuwa wanajindanganya kwani umma hautawasamehe kutokana na sifa ambazo jamaa ameishajizolea.”
Kanji aliyekuwa akiongea na bibi kuba Bombei anaamua kutia guu, “Veve danganya nani? Nenda danganya nyani. Hapa kama yeye na Kolimba au Sokoine yeye hapana vatu naingia taani. Swahili iko oga sana. Kama kuba nafanya yoyote nataka yeye nakaa natoa machomacho kama haihusu yeye.”
Kijiwe kikiwa kinanoga likapita shangingi na Muongo tukalikimbiza kutaka tumpe kichapo cha mwizi. Bahati yake ndata walimuwahisha kabla hatujamfanyia kitu mbaya.
Chanzo: Tanzania Daima Desemba 16, 2015.
No comments:
Post a Comment