How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday 8 December 2015

Akina Makonda waache uhuni na kuvunja sheria

  •  
Hakuna ubishi. Staili ya kutawala ya rais John Pombe Magufuli (JPM) imewastua –licha ya kuwazindua wengi –waliokuwa wamezoea kutegea, kubia, na kufuja mali za umma. Baada ya kuapishwa na kuingia kazini kwa staili ya namna yake, tunaanza kuona walioko chini yake wakiwajibika.
Baada ya Magufuli kutangaza wazi wazi kuwa sasa mazoea basi, tumesikia baadhi ya watendaji kama vile mkuu wa Wilaya ya Kinondo –aliyeuliwa kwa mizengwe – wakihamanika na kuanza kufanya mambo mengine ambayo ni kinyume cha sheria ukiachia mblai kuonyesha kutojua kinachoendelea. Hivi karibuni vyombo vya habari vilikariri habari ambapo Makonda aliamuru maafisa 20 wa ardhi kuwekwa ndani kwa masaa sita kwa kuchelewa kuhudhuria kikao jambo ambalo sijui kama limefuata misingi ya sheria hasa ikizingatiwa kuwa mhusika (hakimu wa kujipachika) hana mamlaka kisheria kumtia mtu yeyote hatiani achilia mbali kuamuru aswekwe ndani. Makonda alikaririwa akisema, “Nina imani saa sita hizo waliozokaa ndani zitakuwa somo kwa watumishi wengine wa umma kujali muda.” Wapo wanaojiuliza ni kwanini Makonda amechukua hatua hizi na si tangu alipoteuliwa. Sina haja ya kuwatetea waathirika wa uhuni wa Makonda ila.  Wapo pia wanaoona kuwa sasa unaanza utawala usioheshimu sheria na kanuni kiasi cha kuanza kuwa vurugu. Pia wapo wanaoona kuwa watendaji wasiojali wala kujua sheria kama Makonda wanaweza kutia doa juhudi za Magufuli za kutokomeza ubangaizaji, uzembe, wizi na uhujumu kwa umma. Lazima tufuate sheria kama ilivyo na si kukurupuka na kutaka sifa jambo ambalo laweza kuligharimu taifa hasa wahusika watakapokwenda mbele ya sharia na kukuta waliadhibiwa kinyume cha sharia. Alijuaje kuwa kosa waliolotenda wahusika lilistahili adhabu husika? Kwa nijuavyo, kila kosa liwe la madai au jinai huwa na vifungu vyake vya sharia. Sijuia Makonda ametumia kanuni zipi za adhabu kufikia hitimisho na uamuzi alivyochukua jambo ambalo ni kinyume cha sharia. Katika nchi yetu ni hakimu au jaji pekee wanaoweza kumkuta au kutomkuta mtu na hatia na kuto aadhabu kali kama hiyo. Ni vizuri basi tukawaonya watendaji kama Makonda kuacha uhuni wa kujiamria mambo bila kufuata sheria.
 Pia tullisikia Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro, aifanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha afya Kambarage mjini Shinyanga ili kujionea hali halisi jinsi huduma zinavyotolewa kwa wananchi siku moja tu baada ya muuguzi wa kituo hicho kukamatwa kwa tuhuma ya kuiba dawa za serikali. Wapo wanaohoji: Je alikuwa wapi wakati kila uchao tunasikia malalamiko mengi tu toka kwa wananchi?  Japo ni jambo jema kwa Mkuu wa Wilaya kwenda kujionea mwenyewe kadhia ya kuhujumu taifa, kwanini waanze sasa? Je watafanya hivyo hadi lini? Je wanafanya hivyo kwa uchapakazi au hofu ya Magufuli ukiachia mbali kutaka waonekane wanachapa kazi?
Kila mtanzania angependa kuona mambo yakibadilika huku serikali na mfumo mzima vikirebishwa kukidhi mahitaji na matarajio yao. Lakini lazima mambo haya yafanywe kwa kufuata na kuheshimu sheria na si kutumia ujinga, uhuni hasira na kutaka sifa.  Haiwezekani watu waanze kujifanyia mambo ya hovyo watakavyo kwa kisingizio cha kutekeleza sera za rais. Tunadhani –ili kuonyesha mfano na namna anavyojali utawala bora na wa sheria –rais Magufuli atamchukulia hatua Makonda hasa ikizingatiwa kuwa uteuzi wake ulijaa utata licha ya kutokuwa na sifa za kushikilia nafasi hiyo adhimu. Pia, lazima kuwepo na utaratibu unaoeleweka wa kufanya mambo. Maana, kwa kutumia kisingizio cha kutelekeza sera za rais, wapo watendaji wanaoweza kuwakomoa wabaya wao ukiachia mbali kujigeuza miungu watu kana kwamba wao wako juu ya sheria. Makonda amewaadhibu maafisa husika bila kufuata sheria na taratibu, je wahusika watagwaya na kuendelea kuumia kimya kimya? Nadhani asasi za kupigania uwajibikaji, haki na haki za binadamu wanapaswa angalau kulaani uvunjwaji huu wa sheria na haki za binadamu. Tunapendekeza hili lifanyike kwa kuhofia kujikuta kwenye hali ambapo waathirika watakwenda kudai haki mahakamani na kulipwa fidia toka kwenye fedha ya walipa kodi ambao wanajifanya kuwatetea kwa kuvunja sheria. Kuna msemo wa Kiingereza kuwaTwo wrongs don’t make a right yaani makosa mawili hayawezi kuhalalisha jambo. Tunaunga mkono harakati za rais za kuhakikisha kila mfanyakazi anawajibika au kuwajibishwa asipofuata sheria. Lakini yote haya yafanywe kwa kufuata na kuzingatia kanuni na sheria ili kuogopa kupoteza fedha na muda kwenye kesi zinazoweza kuepukika.
Hivyo, tumalizie kwa kuwataka watendaji wenye pupa, ua wasiojua wala kuheshimu sheria kama Makonda kuacha kumuaibisha rais kwa kisingizio cha kutekeleza maelekezo au sera zake. Wananchi kwa pamoja au mmoja mmoja wasiruhusu walevi wa madaraka kuwanyanyasa kwa kisingizio cha kutekeleza sera za rais. Tunadhani wananchi wa Manispaa ya Kinondoni waliotiwa aibu na huyu mkuu wa wilaya wa kupachikwa wana haki ya kuandamana wakimtaka rais awateulie mkuu wa Wilaya anayejua na kuheshimu sheria na haki za binadamu. Haiwezekani kuwa na watendaji wasiojua hata mipaka ya mamlaka yao wala mambo ya kawaida kama utawala bora na wa sheria.
Chanzo: Tanzania Daima Desemba, 6, 2015.

No comments: