How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Sunday 13 December 2015

Motisha na kuzawadia wafichua uovu


            Hakuna ubishi kuwa juhudi za rais John Pombe Magufuli (JPM) za kusafisha taifa toka kwenye mfumo na mazoea ya uozo zinaweza kubadili taifa letu toka kwenye ujambazi na ufisadi unaohujumu na kukwamisha umma wa walio wengi.
            Hata hivyo, hatua hizi haziwezi kufanikiwa bila kuwapo na taarifa zihusianazo na uovu, wapi ulipofanyika, upi na wa lini. Kufanikisha juhudi hizi ambazo ni za aina yake kwa taifa letu, lazima kuwapo na mfumo na utaratibu wa kuwapa motisha watu wema wanaoweka maisha yao rehani kwa kufichua uovu husika. Ni jambo linalotaka kujitoa mhanga kuuchukia na kuufichua uovu. Ili kufichua uovu wowote –tena uhaohusisha mabilioni ya fedha ya watanzania –lazima kuwepo vitu vikubwa viwili yaani mapenzi kwa taifa au uzalendo na kuwa tayari kulipa gharama unapogunduliwa. Kwa maana hiyo basi, wanatoa taarifa za uovu sehemu mbali mbali kwenye taasisi za umma na binafsi –licha ya kuzawadiwa na kupewa motisha –wapewe ulinzi wa uhakika ili kuwapa motisha wengine wanaojua maovu yanayofanyika au ambayo yameishafanyika kwenye taasisi husika.
            Japo lengo la serikali ya awamu ya tano ni jema tu, si wote wanaoliunga mkono wala kulipenda ukiachia mbali wengi wa wahalifu waliokuwa wakinufaika na mfumo wa kujihomolea kufanya kila mbinu kulikwamisha.  Uzoefu unaonyesha kuwa uzawadiaji watoa taarifa huleta mafanikio. Mfano wa karibuni ni pale Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) ulipotoa zawadi kwa yeyote ambaye angetoa taarifa za alipokuwa akijificha kiongozi wa kundi la ugaidi la Al Qaeda. Baada ya kufanya hivyo, mtego ulimnasa mhusika na kumalizwa haraka sana iwezekanavyo.
            Upelelezi au uchunguzi wowote wa kisayansi hutegemea sana taarifa ambazo mara nyingi hutolewa na watu wa ndani ya taasisi husika kutokana na ima kutaka kuukomesha uovu, kupata zawadi, hata kujitolea kwa mapenzi ya taifa lao.
            Tunashauri serikali ya awamu ya tano kujenga utaratibu wa kuwazawadia wahusika japo fedha kidogo tokana na kiasi cha fedha zitakazookolewa. Mfano, waliofichua uovu wa kutoroshwa kwa makontena zaidi ya 300 ambao ungelisababishia taifa kukosa shilingi bilioni 80 lau wangepewa asilimia kuanzia moja hadi kumi ili kuwapa motisha wengine wenye taarifa nyeti kama hizi.
            Kwa sasa tunajua. Wezi wengi –tena wakubwa tu –watakuwa wakihaha kuficha mali walizopata kinyume cha sharia. Hivyo, serikali ikitoa motisha kwa watoa taarifa za kufichua uovu, uwezekano wa kuwazidi wezi hawa kete ni mkubwa. Hapa lazima serikali iwe makini kuhakikisha inalinda watoa taarifa kwa kutotoa majina, picha au habari zinazoweza kuwatambulisha.  Namna hii, hata wezi wenyewe wataogopa kwa vile hawawezi kujua nani atatoa taarifa zipi linin a wapi. Wahenga walihusia kuwa penye udhia penyeza rupia. Lazima serikali ya awamu ya tano ipange fungu litakalotokana na fedha zitakazookolewa kwenda kwa wafichua uovu wenye taarifa sahihi na nia nzuri zitakazowezesha vyombo vya dola kuwakamata na kuwashughulikia waovu.
            Pia serikali isikubali maelezo ya baadhi ya watuhumiwa wanaojisafisha kwa kuwatoa kafara wenzao. Mfano wa hivi karibuni ni mfanyabiashara mmoja wa Kariakoo ambaye anahusika na ukwepaji wa kodi. Jamaa huyu alisikika akisikitikia eti jina lake. Ana jina gani wakati ni mharifu wa kawaida tu? Ni ajabu kwa mhusika kusikitikia jina lake na si taifa.  Kuna haja ya kuwachunguza wahalifu hawa kuanzia hata siku walipoanza kufanya biashara zao haramu za ukwepaji kodi.
            Tanzania ni taifa letu. Hata hivyo, ina raia wa aina mbili. Wapo wenye mapenzi mema na taifa lao na wapo wanaoitumia kama shamba la bibi kuchuma na kutorokea wanakodhani ndiyo kwao. Kuna haja ya kuwamulika maafisa wa serikali walio kwenye kitanda kimoja na mafisadi wanaohujumu maisha ya watanzania.  Na kufanya hivyo, ni kuhakikisha hakuna mtu anayecheza na mfumo wetu wa sheria wala upelelezi wala anayejihisi yuko salama kwenye kutenda uovo kama ilivyokuwa kwenye tawala tatu zilizopita. Ni wakati muafaka kutangaza kiama cha ujambazi na wizi wa fedha za umma kama wenzetu wa Rwanda walivyofanya na kubaki wakitucheka kwa kukalia raslimali na mali nyingi hivi lakini tukawa taifa la ombaomba wakati fedha yetu inaibiwa na majambazi wachache.
            Tumalizie kwa kuihimiza serikali hasa rais Magufuli kuweka mtandao mpana wa kupambana na wizi wa mali na fedha za umma kwa kuhakikisha wanatakaokuwa tayari kujitolea  kutoa habari za uovu wanazawadiwa kulindwa na kumotishwa ili wengi wenye taarifa nyeti na muhimu wajitokeze na kulikwamua taifa lao. Watanzania wanaweza kuishi maisha bora na halali hata bila kutenda uovu kama kila mmoja –kwa wakati na namna yake –atatimiza wajibu wake kwa uwajibikaji na uaminifu mkubwa kwa taifa lake.
Chanzo: Tanzania Daima Desemba 13, 2015.

No comments: