The Chant of Savant

Tuesday 11 August 2020

Lissu hana hoja hapa eti Magufuli kajenga uwanja wa ndege kwao!

Opposition leader Tundu Lissu returns to challenge Magufuli, after ... 

Kitendo cha serikali ya awamu ya tano kujenga uwanja wa ndege mkoani Geita kinaonekana kuwakera baadhi ya watanzania hasa wapinzani wa serikali. Mmojawapo aliyeshupalia na kuvalia njuga uwanja huu pamoja na mbuga ya wanayama aliyoinzisha mkoani Geita si mwingine bali mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu ambaye hivi karibuni alisikika majukwaani akiligeuza hili kuwa sera. Jamani, kama hamna cha kumpinga rais John Magufuli heri mjinyamazie kuliko kujiaibisha. Lissu anasema hii ni aibu na watanzania si wajinga. Ni kweli. Watanzania si wajinga kiasi cha kuamini ujinga wake. Hivi kwanini haulizi vigezo vilivyotumika kujenga uwanja husika huko Chato mkoani Geita? Je Lissu hajui kuwa kwa sasa madini ya dhahabu ambayo yanapatikana sana mkoani humo ni ya pili kwa kuchangia pato la taifa? Je hajui kuwa wachambaji wengi wa dhahabu huko Geita licha ya kampuni kubwa kuliko zote ya Geita Gold Mine Ltd (GGML) wako Geita? Je hajui kuwa wachimbaji wengi ni matajiri wanaotaka usafiri haraka? Je kama mkoa wenye kuzalisha dhahabu nyingi kiasi hiki kosa liko wapi kuwa na uwanja wa ndege wa kimataifa?

Mbali na Chato kuwa strategic kwa usalama wa nchi na alternative kwa ndege zinapokuwa na dharura si Tanzania bali hata nchi jirani, Geita ina vivutio kama vile mbuga ya wanyama ya Burigi Chato ambavyo vinahitaji watalii na usafiri wa haraka. Lissu hajui kuwa mbuga anayolalamikia ni ya tatu kwa ukubwa baada ya Ruaha na Serengeti. Je alitaka hii mbuga iendelee kuwa vitalu vya uwindaji wa kifisadi kama zilivyokuwa nyingine alizoanzisha hivi karibuni? Mbona Lissu halalamikii mbuga nyingine zilizoanzishwa sambamba na mbuga hii wala viwanja vya ndege vilivyojengwa sambamba na hiki kinachomnyima uzingizi?

Kwanini Lissu na CHADEMA wasifanye japo homework kidogo wajiulize ni kwanini Geita inayoingiza mabilioni ya shilingi kwenye uchumi wa taifa isiwe na uwanja wa ndege lakini Zanzibar ambayo pato inaloiingiza haliwezi kulingana na Geita iwe na uwanja wa ndege wa kimataifa? Kwanini halalamikii Mbeya kuwa na uwanja wa kimataifa wa ndege wala Mwanza? Hata angepanua uwanja wa ndege wa Mwanza na kuacha kujenga wa Chato bado wangesema anapendelea Kanda ya Ziwa. Haya ndiyo mawazo ya watu wanaoshindwa kufikiri sawa sawa na kuhukumu mambo kama yalivyo baada ya kufanya hivyo kwa kusukumwa na hasira na kutaka umaarufu rahisi na kulipiza kisasi. Wanaobeza juhudi za Magufuli wanapaswa kuwa na busara japo kidogo.

Siku moja nilimsikia profesa mmoja wa lugha mstaafu aking’aka eti watu wanasifia barabara, madaraja, ndege na reli. Anataka wasifie umaskini tulio kuwa nao hadi tukazidiwa na viinchi kama Kenya visivyo na raslimali hata nusu yetu? Profesa huyu wa CHADEM alisikika akimnukuu na kumsingizia Marehemu baba wa taifa Mwl Julius Nyerere kuwa alisema kuwa maendeleo lazima yawe ya watu. Ama! Kwani hizo barabara, madaraja, ndege na reli vimejengwa visafirishe Wanyama au majini? Si hawa hawa wanaopiga kelele watakuwa wa kwanza kuvitumia?

Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni jamani. Wapo waliowahi kusema kuwa hata makaburu wa Afrika ya Kusini walijenga hiyo miundombinu. Kwanini hawajiulizi hao makaburu walimjengea nani kama siyo weupe tu waliokuwa wamewezeshwa kufaidi vitu hivyo kwa jasho la Mswahili? Ajabu ya maajabu hao hao wanaomzodoa na kumlaani Magufuli kwa kujenga vitu ‘badala ya utu’ ni wale wale waliokuwa wakisafiri toka kwao kupitia wengine Uganda na wengine Kenya kwenda Dar es Salaam. Yaani tumekuwa wepesi wa kusahau hivi kiasi cha kujigeuza kwa makusudi wezi wa fadhila? Walitaka Magufuli ajenge nini zaidi ya miundombinu ili kufanya mageuzi ya uchumi wa kisasa? Hao hao wakienda Ulaya wakapanda vipandwa wanavyolalamikia wakija huku wanaanza kusema kwanini hatuwi kama Ulaya? Tukitaka kuwa kama Ulaya wanayoiabudia, tena wanaanza nongwa. Hii ni tabia ya kitoto. Mtoto ukimpa mpira achezee akaupoteza anakulaumu. Ukimnyima asiuchezee ili asiupoteze anakulaumu. Ama kweli hawa ni akina Siwema.

Bila kusema mengi, wanaotaka kumpinga Magufuli watafute na kujenga hoja zenye mashiko badala ya uzushi na siasa za maji taka kwa kukopa toka kwa marehemu Samuel Sitta. Tuache siasa chafu. Watanzania si wajinga hivyo. Watanzania si wasahaulifu hivyo. Wala watanzania si vipofu na viziwi jamani.

Serikali ya awamu ya tano sasa iko mbiyoni kujenga hospitali za rufaa mikoani. Kesho utasikia Magufuli kajenga hospitali ya rufaa kwao. Je kwao hawaugui? Je kwao si watanzania sawa na wengine wanaohitaji huduma hii? Je Geita––kumzaa Magufuli­­––inapoteza haki zinazopewa mikoa mingine? Ni ajabu kumsikia Lissu akisema eti Geita hakuna biashara ya kuhitaji ndege. Ama! Mbona Arusha na Kilimanjaro kuna uwanja wa ndege wa kimataifa? Juzi Lissu alisikika akisema eti uwanja wa ndege wa Chato hauna kazi bali kutumika kumsafirisha Magufuli na mama yake. Haya ni matusi ya nguoni. Anasema eti Nyerere hakujenga uwanja wa ndege kwao. Angejengaje wakati ule vipaumbele vilikuwa ni siasa za ukombozi na si ukombozi wa kiuchumi? Angejengaje wakati hata barabara zenyewe hazikuwa zimejengwa tokana na jukumu la Tanzania kumpiga nduli Idi Amin na kuongoza mapambano Kusini mwa Afrika? Nina hakika hata Nyerere angekuwa hai leo, angemwambia Magufuli akachape kazi kama ambavyo mzee Ali Hassan Mwinyi na Marehemu Benjamin Mkapa walichagiza si mara moja wala mbili.

Kwa leo itoshe kuwasaidia wenzetu kufikiri kuwa kinachoendelea Tanzania, si kwa faida ya Tanzania tu bali hata majirani zetu hasa nchi zisizokuwa na bandari kama vile Rwanda, Uganda, Zambia na DRC. Cha msingi ni kukubali na kuelewa kuwa ndege zitazidi kununuliwa, barabara na madaraja kujengwa na mbuga mpya za Wanyama penya Wanyama kuanzishwa kwa faida ya watanzania watake wasitake. Na hakika huku ndiko kushindwa hata kabla ya kuanza uchaguzi.

Nkwazi Mhango masomoni Kanada

 

No comments: