The Chant of Savant

Saturday 2 January 2021

CHADEMA Igeni mfano wa ACT-Wazalendo


Uchaguzi mkuu uliopita ulijaa vimbwanga, visasi, visingizio hata vitisho hasa baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilishinda kwa kishindo kwa aslimia 84 urais na kuzoa viti karibu vyote huku upinzani ukiambua  viti viwili tu upande wa Bara jambo ambalo halijawahi kutokea tangu kuingia mfumo wa vyama vingi. Japo ni nje ya mada ya leo, washindi wa viti viwili tu vya upinzani Bara ni wanawake mmoja mmoja toka CHADEMA na mwingine toka CUF. Hivyo, unaweza kusema kuwa uchaguzi wa mwaka huu umeutia ufa mfumo dume na imani kuwa akina mama hawawezi siasa za ushindani wakati wanaziweza kama walivyodhihirisha. Kwani, kwenye bunge lililoanza hivi karibuni, upinzani kwa upande wa Bara hautakuwa na mwanamme hata mmoja. Ushindi wa akina mama hawa ambapo wanaume wote walishindwa uwahamasishe akina mama wengi kushiriki nafasi za kuchaguliwa na kuachana na kutegemea nafasi za viti maalumu ambazo sasa ziko zinawagombanisha wao kwa wao na vyama vyao kwa baadhi ya vyama. Kimsingi, viti hivi viwili vinakomesha matusi na upuuzi kuwa akina mama siyo thabiti kisiasa kiasi cha kutegemea viti vya dezo.  Kama akina mama wameweza kumzaa kila mmoja wa binadamu wote duniani, watashindwa nini kumuongoza? Nayapongeza majimbo yaliyowachagua hawa akina mama wawili waliovunja rekodi ya kuwachakaza wanaume waliotoka kapa kiasi cha sasa kuanza hata kuwawekea mizengo kwenye viti walivyoshinda kihalali na kwa kuvuja jasho.
     Sasa uchaguzi ni historia baada ya viongozi wote kuapishwa na kushika nafasi zao. Baada ya uchaguzi kutangazwa, mfano, mgombea wa upinzani aliyeambulia aslimia 13, kwanza, hakutambua matokeo wala kumpongeza mshindi. Pili alitimkia ughaibuni alikokuwa kabla akidai maisha yake yalikuwa hatarini ilhali kwenye kipindi chote cha  kampeni ambako alikuwa akichanganyikana kirahisi na kiholela maisha yake hayakuwa kwenye hatari jambo ambalo linatia shaka au kuzua maswali mengi kuliko majibu.
    Hata hivyo, pamoja na upinzani kusimama kidete pamoja kupinga matokeo, wapo waliofanya kile ambacho waingereza huita Road to Damascus kwenye kisa cha biblia ambapo hasidi mkubwa wa Yesu aliyekuwa akiua wanafunzi wake Paulo au Sauli ‘alitokewa na sauti ya Bwana’ akaamua kuslimu na kujiunga na kumfuata Yesu. Samamba na hili, hawa si wengine bali chama cha ACT-Wazalendo ambacho kilikuwa kimekamia kususia matokeo lakini kisijue kuwa mbali ni kuwa agizo la katiba kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), kugomea ulaji ni kukufuru hasa kwa walioshindwa vibaya. Tunakipongeza kwa ujarisi wake wa kuachana na msimamo ambao ulikuwa hasi hasa pale kilipokaribishwa kujiunga na SUK Visiwani kikaanza kugoma goma na mwisho wake kikaamua kuingia hasa ikizingatiwa kuwa kama si Katiba ya Zanzibar kukibeba, hapakuwa na namna au stahiki ambapo chama kilichoshindwa kingeingia kwenye serikali.
     Kimsingi, kilichofanyika Zanzibar ni kuheshimu Katiba ambayo inatamka wazi kuwa chama kitakachokuwa cha pili kitapewa nafasi ya Umakamu wa kwanza wa Rais na viti kwenye baraza la mawaziri kulingana na aslimia ya ushindi wa chama husika. Hivyo, kitendo cha awali cha ACT-Wazalendo kukataa mwaliko wa kujiunga na SUK ilikuwa ni kinyume na Katiba. Sasa ACT-Wazalendo wamo ndani, hakuna tena ubishi kuwa wametekeleza matakwa na maagizo ya Katiba ya Zanzibar. Pamoja na yote, tunawapongeza kwa hili. Maana hakuna mgogoro usio na mwisho hasa muamuzi mwenyewe wanapokuwa ni wananchi walioamua kuichagua CCM.
    Hata hivyo, kwa upande wa Bara ambapo Katiba ni tofauti na Visiwani iko wazi kuwa chama kitakachoshinda kitaunda serikali bila kulazimika kikatiba na kisheria kuwashirikisha walioshindwa, hali ni tofauti. Kama tulivyoeleza kwenye utangulizi, upinzani, pamoja na kushindwa wazi wazi, bado haujaitambua serikali ya CCM ambacho kilishinda uchaguzi kihalali.
     Wakati ACT-Wazalendo iliyochukua nafasi ya pili Visiwani ishapeleka wateuliwa na wachaguliwa wake, Bara ambako nafasi ya pili ilishikiliwa na CHADEMA, bado wahusika wanavutana. Hadi tunaandika wabunge 19 wa viti maalum waliochaguliwa na Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA), licha ya kuamriwa na chama wasishiriki bunge, walitimliwa uanachama kwa kukubali kuapisha na Spika wa Bunge kwa mujibu wa sheria. Hii maana yake ni kwamba CHADEMA wameamua kupinga Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inayotamka wazi kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu ndiye ataunda serikali bila kulazimaka kuwakaribisha wapinzani tena walioshindwa kama ilivyo Visiwani ambako Katiba ilifanya hivyo tokana na mazingira ya huko na migogoro isiyo na mwisho iliyowahi kuleta maafa kule.
       Japo kususa kutuma wawakilishi wake ambao wanaona hawakufuata utaratibu ni haki yao kama chama, ila si haki yao kudharau maagizo ya Katiba kama wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na taasisi ya umma ambayo uhalali wake unatoka kwenye Katiba ile ile wanayopinga maelekezo yake kama watashikilia msimamo wa kutotuma watu wake bungeni. Pamoja na kuwapo wanaoona kama kilichotokea Visiwani ni matokeo ya siasa za sura badala ya sera na mvuto wa ulaji kwa wahusika, bado tunawapongeza kwa kukubali maelekezo ya katiba.  Kwani nani asiyetaka ulaji tena kama ni wa dezo kwa mtu au chama kilichoshindwa vibaya?
      Tumalizie kwa kuwataka CHADEMA wafikiri upya hasa ikizingatiwa kuwa kushiriki bunge ni amri ya kikatiba na si ya utashi. Wamalize gogoro na akina mama wao watoe mchango kwenye uendeshaji wa nchi kwa mujibu wa Sheria na Katiba.
Chanzo: Nipashe J'pili leo.

No comments: