The Chant of Savant

Saturday 23 January 2021

Hii Ndiyo Dawa ya Wanaohujumu Miundombinu Yetu

Kitendo cha baadhi ya wenzetu kuiba viti vya shule na kuviuza kama vyuma chakavu–––kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari hivi karibuni–––kinatia kinyaa. Pia kitendo cha wenzetu walioaminiwa ofisi za umma kuuibia umma ni mauaji, hujuma na unyama visivyo na kifani. Vinatia kinyaa. Rejea kufukuliwa kwa wizi wa madawa kwenye hospitali ya rufaa ya Muhimbili hivi karibuni. Je mchezo huu unafanyika Muhimbili tu au ni nchi nzima? Je umekuwa ukifanyika kwa muda gani na fedha kiasi gani tushapoteza kama taifa?  Japo wote tungependa tutajirike, vitendo kama hivi, ni zaidi ya ujambazi. Ni ujambazi, unyama na uuaji wa wazi.  Ni vya kikatili; na vinapaswa kupigwa vita kwa ukali wote. Je ni watu wangapi wasio na hatia wamepote za maisha tokana na ukatili huu utokanao ubinafsi, ulafi, upofu na upogo wa kutisha? Je kama taifa tunapaswa kufanya nini kupambana na ushetani huu ambao–––kama siyo kuigaiga na kuendekeza haki za binadamu zinazokinzana na za wengine–––wanaopatikana na hatia kama hizi ni wa kunyonga ili liwe mfano na somo kwa wengine wanaootea kuurudufu kwa kutaka kutimiza tamaa zao za utajiri.
            Tunapopata maskini na wajinga kama hawa, kamata, charaza bakora na toza faini eneo zima linapotokea tukio ili kila mmoja aonje madhara ya kuendekeza ujinga, umaskini na njaa.  Hivi kweli kuna haja ya kuiba vifaa vya umeme, mabomba ya maji, kutupa taka ma kuziba mifereji na kuchafua mito yetu, kuhujumu reli au barabara na mengine kama haya wakati serikali inaingia gharama kubwa kuviweka ili kuondoa kero kwa wale wale ambao miongoni mwao wanavihujumu? Kwa mfano, kama bomba la maji la kijiji limehujumiwa, wanakijiji wapewe fursa kwanza, kuwasaka au kuwataja wahusika. Wasipowapata, wote wawajibishwe kwa kuchangishwa fedha za kurejesha bomba au kitu husika.
            Adhabu pekee haitoshi kukomesha tatizo. Lazima serikali–––kwa  makusudi mazima–––itoe  elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa miundombinu kwa maisha na ustawi wao, gharama za kupatikana miundombinu na madhara kwa watu binafsi, jamii na taifa. Sambamba na umuhimu, elimu husika ieleze bayana madhara yatokanayo na hujuma hizi kwa mtu binafsi na jamii kwa ujumla. Katika kutekeleza hili, lazima kuwepo na usimamizi na ulinzi shirikishi ambapo kila mdau ana wajibu wa kulinda mali za umma akiwa ni sehemu ya umma. Lazima wananchi waambiwe kuwa wao ndiyo serikali na serikali siyo kiumbe cha ajabu tofauti na wao.
            Katika ulinzi wa pamoja, lazima kuwepo uwajibikaji wa pamoja kama ilivyo katika kufaidi au kukosa huduma husika. Hapa lazima kuunda mfumo wa kuripotiana na kutaarifiana pale wanajamii wanaozunguka eneo husika–––ambao kimsingi ndio wamilki wa miundombinu husika–––wanapohisi u kubaini kuna njama za kuhujumu mali yao, lazima wawe na mikakati yao wenyewe binafsi kama jamii ya kushughulikia kadhia husika na siyo kungoja serikali kana kwamba wao hawahusiki. Serikali wanayongoja hainywi maji toka bomba au kutumia umeme toka kwenye nyaya husika.
Lazima wananchi wafundishwe kuwa wao ni walinzi na wanufaikaji wa mali wanazohujumu kwa maslahi binafsi.  Wananchi wakitishwa jukumu la kulinda miundombinu na mali za umma, watavidumisha. Kwani, wanajuana kwa majina na sura ukiachia mbali shughuli wazifanyazo mbali na tabia za wenzao.  Mjenga na mbomoa nchi ni mwananchi na mnufaikaji kadhalika. Hili lazima walijue na kulikubali. Mfano, ofisini kama kutabainika matumizi mabaya ya maji au umeme, wanaotumia ofisi husika walipishwe bill wote bila kujali nani alihusika. Hii itajenga woga na utaratibu wa kuhimizana, kusimamiana hata kuchunguzana ili kuondokana na kadhia itokanayo na kuadhibiwa kwa kosa ambalo mtu hakutenda.
        Tumalizie kuwa wenzetu wa nchi za Magharibi hawakufikia hali ambayo hutufanya kuwahusudu kimiujiza bali ni kwa kubanana hadi wakazoea baada ya kuona manufaa ya kuwa na miundombinu endelevu na ya kudumu tokana na kuilinda vilivyo na kuitumia vizuri. Mwisho, piga marufuku biashara zinazopokea vitu kama vyuma chakavu na mengineyo.
            Ngoja tugusie jinai na kadhia ya uhujumu uchumi vitokanavyo ubinafsi na ulafi vya kutisha kwa ujumla. Tunapogundua jinai na kadhia kama hizi, tuangalie waliotenda ni nani na wamesukumwa na nini. Wapo wanaosukumwa na ujinga na umaskini vya kawaida. Mara nyingi, ujinga na umaskini vikichanganyikana, vinazalisha viumbe wa hovyo hata kuliko mbwa. Maana, mbwa mwenye akili zake, hawezi kumuibia anayemfuga kwa vile anajua wajibu wake. Je binadamu anayehujumu miundombinu na mali nyingine kama vile shule, mabomba ya maji, barabara, reli na mingi–––tena vyake–––siyo wa hovyo kuliko mbwa asiyemwibia anayemfuga? Mbwa ni hayawani. Lakini hayawani anayejua umuhimu wa amfugaye anaweza kuwa mwema na wa maana kuliko binadamu asiyejua umuhimu wa huduma apewazo na serikali yake tena kwa kodi kubwa za wengine.
            Ukiachia mbali jinai tajwa hapo juu kuwa unyama, ni  uhujumu wa nchi na uchumi. Tokana na hasira na machukizo jinai hizi zinasababisha, hata pale wahusika wanapokutwa na hatia, mojawapo ya adhabu iwe ni kuwachapa bakora za kutosha hadharani halafu mengine yafuatie. Kwanini taifa letu linaanza kugeuzwa la mahayawani kwa kutisha hivi? Yaani pamoja na juhudi za rais John Pombe Magufuli kuondoa nchi kwenye utegemezi na umaskini bado kuna viumbe wanaofanana na binadamu waliogoma kumuelewa! Inatisha na kusikitisha.
Chanzo: Nipashe Jpili.

No comments: