Kwa mara nyingine, Tanzania imepata msiba. Ni msiba wa mtoto wa baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Ni msiba wetu wote kama familia ya watanzania. Tokaa na kupendwa kwa familia ya baba wa taifa, wengi wataguswa na msiba huu wa binti yake. Kama marehemu baba yao, baba wa taifa, familia ya mwalimu Nyerere inapendwa tokana na uadilifu na usafi wa baba yao. Wao kadhalika, pamoja na kuwa watoto wa mtu mkubwa kama baba yao, walifuata nyayo za baba yao yaani kuishi maisha ya kawaida sawa na watanzania wengine. Kweli mtoto wa nyoka ni nyoka na wa njiwa ni njiwa! Nadhani kupendwa kwao si tukio la bahati, pamoja na kuchangiwa na ukoo wao hasa idhtibati ya marehemu baba yao, umechangiwa kikubwa na tabia yao ya kutopenda kutumia jina la ukoo wao kujinufaisha binafsi. Ukitaka kutafuta mabakia ya Ujamaa Tanzania, mahalil pazuri pa kuanzia ni Butiama kwenye familia ya Nyerere BONYEZA HAPA. Wanaomjua marehemu Rosemary wanashuhudia kuwa alikuwa mama wa kawaida tena maskini ambaye aliweza kumilki nyumba yake baada ya kulipwa kiinua mgongo cha kutumikia Bunge. Piga picha angekuwa ni binti wa marais wa zamani kama Kenyatta, Moi au Mobutu. Si angekuwa na maelfu ya maghorofa ndani na nje. Ukiachia mbali yeye, wapo wanaofahamika kama vile kaka zake ambao nao hawana makuu wala ukwasi wala kujisikia kama watoto wa baba wa taifa. Kwa bahati nzuri, nimetokea kumfahamu mmojawapo binafsi. Huyu si mwingine ni Madaraka G Nyerere. Kufahamiana kwangu naye kuna hadithi ndefu na mbovu kidogo ambapo niliwasiliana naye kuhusiana jambo fulani juu ya baba wa taifa wakati nikitafiti andiko langu kwa ajili ya shahada yangu ya uzamivu (PhD) akawa hana muda wa kunijibu kiasi cha kuudhika na kumsuta kinamna. Kutokana na unyenyekevu na welewa wake, aliniomba nimsamehe kwa vile alikuwa na majukumu mengi. Tuliwelewana na kuacha yaliyopita yapite na kusonga mbele kama marafiki na ndugu hadi leo. Tokea hapo tulikuwa marafiki na ndugu kiasi cha kuwasiliana kila tunapopata muda. Nachukua fursa hii kumpa rambirambi na makiwa kwa kufiwa na dada yake.
Kwa ujumla, ukiwalinganisha watoto wa Nyerere na wa wezi kama akina Mobutu, Bokassa na wengine waliotumia madaraka vibaya, wanatembea kifua mbele. Hivyo, msiba wa Rosemary si msiba wa familia ya Nyerere tu bali taifa zima.
PUMZIKA MAHALI PEMA PEPONI ROSE NA MUNGU AIFARIJI FAMILIA NA TAIFA KWA MSIBA WA MPENDWA WETU.
No comments:
Post a Comment