How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Sunday, 31 January 2021

Kuna Haja Kuchunguza Watumishi wa Maeneo Yote Yenye Mshiko

Wiki iliyopita, tuliahidi kudurusu kwa kina suala la kuchunguzana ili kubana wale wanaoibia umma kwenye nafasi walizopewa kuutumikia na si kuuhujumu au kuutumia. Leo tutaangazia baadhi maeneo yanayopaswa kutushughulisha katika kuchunguzana ili kubaini na kukomesha wizi ambao, kwa nchi nyingi za kiafrika, umekuwa kama desturi kama siyo mazoea tena mabaya ya kimfumo yanayoonekana kukubalika.
Tuanze na bandari. Hili ndilo lango kuu la kutolea na kuingizia bidhaa kwa taifa na mataifa jirani yasiyo na bandari  linalopaswa kuchangia pakubwa pato la taifa na si la watu binafsi wachache, yaani wafanyakazi na wateja wao wasio waaaminifu na wazalendo yaani wafanyabiashara wanaoshirikiana nao kuhujumu taifa. Hakuna ubishi. Watumishi wengi wa idara hii wana ukwasi usiolingana na kipato chao stahiki japo si wote. Ila ikilinganishwa na wengine si haba.
Ukiondoa bandari, ipo mamlaka ya mapato (TRA) ambayo nayo–––licha ya kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na bandari–––pia husimamia mapato yote ya taifa. Pia ina uhusiano wa moja kwa moja na wafanyabiashara wote nchini hivyo kuingiza wizara ya biashara.  Wafanyakazi wa idara hii nao ni wa kuchunguza sana tena mara kwa mara. Rejea mkutano wa rais John Magufuli na wafanyabiashara ikulu mwaka 2019 ambapo mfanyabiashara mmoja toka Mbeya alisema wazi kuwa wafanyabiashara wengi hutoa rushwa kutokana na baadhi ya maafisa wa TRA kujenga mazingira ya kufanya hivyo kwa kuwakadiria kodi kubwa kuliko stahiki. Sambamba na bandari ni idara ya biashara ambayo nayo ina ushawishi mkubwa katika kuingiza na kuuza bidhaa nje. Wafanyakazi wa idara hizi nao wana ukwasi fichi usio wa kawaida. Hivyo, nao ni wa kuwekwa kwenye kundi la kuchunguzwa vikali. Je mchezo huu umeacha? Je ni wangapi wameutumia kutajirika waliopo na waliokwishastaafu? Je hawa si wa kufuatilia na kuhakiki mali zao hata kama hawamo kazini tena?
Eneo jingine tunayopaswa kulitupia jicho kali ni ya Uhamiaji. Hii hughulika na utoaji vibali kwa wageni vya kazi na ukazi kwa wageni na pasi za kusafiria kwa watu wetu. Huku nako kuna kila aina ya ulaji ambao huikosesha serikali mapato. Kuna kipindi pasi zetu zilikuwa zikiuzwa kwa wageni na wahamiaji haramu kama njugu hadi baadhi ya nchi zikaiona pasi yetu kama karatasi isiyo na thamani. Sambamba ni hii ni vituo vya mipakani na viwanja vya ndege ambavyo vilisifika kwa kupitisha madawa na vitu vingine haramu kama ilivyowahi kutokea kupitisha twiga mzima kwenda ughaibuni. Sijui kesi hii imeishia wapi.
Ukiachana na uhamiaji na vituo vya mipakani, kunafuatia mbuga zetu za Wanyama utalii kwa ujumla. Rais Magufuli ni shahidi kuwa kuna watu wamekuwa wakitumia raslimali zetu kujineemesha wakati taifa likiendelea kuwa maskini. Rais aliwahi kuelezea hoteli moja inayotosha mamia ya dola kulala usiku mmoja ukiachia mbali vitalu vya uwindaji na ujangili ambavyo vina baraka za watumishi wa umma wanaovitumia kujineemesha binafsi.
Linalofuatia ni eneo linaloshughulikia madini. Nchi yetu imejaliwa wingi wa madini ambayo mchango wake ungekuwa mkubwa kwa uchumi wa taifa kama tungepambana na watumishi wabovu kwenye eneo hili na kuyatumia vizuri na vilivyo. Hapa hujagusia kwenye nishati ambapo ulanguzi wa umeme umekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya watu wetu. Wafanyakazi wa maeneo haya wanabidi kuchunguzwa bila huruma sawa na watajwa hapo juu. 
Maeneo mengine yanayopaswa kuchunguzwa bila huruma ni kuanzia Tume ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) mahakama, polisi, bohari kuu ya madawa na mahospitali yetu. Kuna haja ya rais kuunda kikosi cha siri ambacho kitakuwa kikiwachunguza hata wale tuliwaamini kuwachunguza wengine. 
Leo nimegusia maeneo husika kwa kuangalia uzoefu wangu hapa Kanada na nchi nyingine tunazoiita zilizoendelea ambazo hazina mchezo na mapato ya serikali na yale ya wananchi au wakazi wake kama sisi. Kila mwananchi na mkazi lazima ajaze taarifa za kodi na mapato yake kila mwaka kwa mujibu wa sheria na siyo utashi. Ukiwa na pesa zaidi ya kipato chako bila maelezo, inataifisha na unashitakiwa kwa makosa ya jinai. Hii ndiyo siri kubwa ya utajiri wa nchi husika pamoja na mengine.
Mwisho, serikali yetu inapaswa kuanzisha mfumo ambapo kodi yake nyingi hukusanywa toka kwenye bidhaa na huduma moja kwa moja. Kwa mfano, hapa Kanada kuna aina mbili kwenye bidhaa na huduma. Kodi ya serikali kuu na ile ya serikali ya mkoa. Unaponunua kitu au kupewa huduma, serikali hupata pesa yake hapo hapo. Kufanikisha hili, kila anayeuza au kutoa huduma lazima atoe risiti. Pia lazima awe na mashine ya kielektronikali (Electronic Fiscal Devices-EFDs) kwenye biashara yake. Kutoa EFDs si jibu kama hakutakuwa na mfumo endelevu,  Madhubuti na wa hukika wa kuhakikisha hazichezewi au kutotumika. Hivyo, lazima kuwe na sheria kali ya matumizi ya mashine hizi. Muhimu, kuwachunguza watumishi kwenye maeneo yanaoingiza au kuhusika na mshiko lazima kuwe endelevu. Wanaogundulika waadhibiwe vikali ili kuwaonya wengine. Kati ya yote, ni kubana fursa yoyote ya mtu kuwa na utajiri usio na maelezo.
Chanzo: Nipashe J'Pili.

No comments: