The Chant of Savant

Saturday 16 January 2021

Siku Trump Alipoivua Nguo, Kuihujumu na Kuidhalilisha Marekani

Zikiwa zimesalia wiki mbili kwa rais wa Marekani, Donald Trump anayemaliza muda wake, kuondoka Ikulu Jumba Jeupe (White House), hali lichacha na kuchafuka kweli kweli.  Mnamo Januari 6, 2021 ilikuwa “siku ya kiza” ( rais mteule Joe Biden) na simanzi katika historia ya Marekani. Kwani ni siku ambapo rais wa Marekani alianzisha maasi dhidi ya taifa hili lenye kujivunia mizizi ya kidemokrasia huku likijiteua kuwa polisi wa demokrasia duniani. Akiwa ameshindwa uchaguzi mkuu wa Novemba, 2020 na Biden, alikataa kumtambua, kumpongeza wala kukubali ushindi huu, Trump alimaua kufanya kile ambacho walatini huita sacriligo (sina tafsiri) au tuseme kilihataji kiasi fulani cha uchizi. Tokana na hili, Wamarekani walitaka Trump aondolewe ofisini haraka ili makamu wake wa rais Mike Pence amalizie ngwe yake.  Wengi wanajua namna Trump alivyohutubia mkutano wa hadhara muda mfupi kabla ya kuwahimiza  wahuni na wabuguzi wa kimarekani kuvamia jengo la Bunge la Marekani la Capitol Hill  na ‘kuirejesha nchi yao nchi yao’ wakati wabunge na maseneta wakiwa kwenye vikao vya kuhakiki na kupitisha ushindi wa Biden.  Katika uvamizi huu, mtu mmoja alipigwa risasi na kufariki huku askari polisi akijeruhiwa na kufa baadaye hospitalini mbali na wengine wanne waliiofariki kutokana na kukosa huduma za matibabu. Wahuni hawa walijitokeza wakiwa na bendera ya kibaguzi na ya ile yenye maandishi ya Trump.
         Baada ya shambulizi hili la aibu na hatari, maseneta na wabunge walirejea Capitol Hill na kumaliza kupitisha ushindi wa Biden. Walivamia wakiwa chini ya uenyekiti wa makamu wa rais Pence huku usalama wake, familia yake na wabunge ukiwa hatarini. Kituko ni kwamba, askari wa jiji la Washington na wengine wa vyombo vya usalama hawakuonekana kama walivyofanya wakati wa maandamano ya amani ya watu weusi ya Black Lives Matter kabla ambapo walijazana na kuwasambaratisha kwa mabomu ya machozi na pilipili na risasi za mpira. Hili–––licha ya kuonyesha ubaguzi wa kimfumo–––limewaacha wachambuzi wengi hoi. Baada ya kwisha kwa kadhia hii, hadi makala hii inaandikwa, Trump hakuwa amewasiliana na Pence ambaye waandamanaji walikuwa wakisema anyongwe kwa kumsaliti mpendwa na kiongozi wao Trump. Je ilikuwaje Trump akawahadaa Wamarekani kiasi cha kupata umaarufu na nguvu hivi? Profesa Makau Mutua anasema kuwa watu wanapenda sana kusema na kusikia uongo (Daily Nation, 10 Januari, 2021). Hivyo, msidhani ni waswahili tu wanaohadaiwa na kuchezewa na wanasiasa bali hata watasha. Binadamu ni binadamu tu.
          Chanzo kikuu cha Trump kufanya machukizo na makufuru ni kupinga kushindwa katika uchaguzi aliosema uliibiwa ilhali serikali yake ndiyo uliyouandaa na kusimamia. Katika kupinga ushindi wa Biden, Trump alifungua kesi zaidi ya 60 mahakamani na kushindwa zote––––tena nyingine zikisikilizwa na majaji aliowateua mwenyewe.
            Kwa mara ya kwanza, rais wa Marekani aliamua kushambulia taasisi muhimu ya kidemokrasia yaani mhimili mmojawapo wa dola. Kitendo kilichowaudhi na kuwadhalilisha wamarekeni kiasi cha kuona kama ule ushafaa wao duniani kuhatarishwa na mtu ambaye alihadaa wakamchagua kulinda taasisi husika akaishia kuzishambulia na kuzidhalilisha. Wengi tunajiuliza: 1) Jinai aliyotenda Trump ingetendwa na mtawala yeyote wa kiafrika hali ingekuwaje? 2) Je mashambulizi ya kigaidi dhidi ya jengo la Bunge yangefanywa na watu weusi wa Marekani, hali ingekuwaje? 3) Je Marekani inaendelea kuwa mwalimu na polisi wa demokrasia duniani wakati taasisi zake zinatia shaka kiasi hiki? 4) Je Marekani itafanya nini–––ikiwemo kumtia adabu Trump na wabaguzi wenzake­­­–––ili kurejesha heshima yake? 5)Je ugaidi huu ambao­­­–––kipindi hiki umefanywa na wazungu­­­–––unaifundisha nini dunia hasa mashabiki wa Marekani? 6)Je Marekani imejifunza nini na itakuja na utetezi gani?
            Marekani, mkosoaji mkubwa wa wegine, kipindi hiki, imeshikwa pabaya. Taifa ambalo lilianzisha vita dhidi ya ugaidi ili kuwakomesha maadui zake sasa linazizima na mchezo lililoasisi. Taifa ambalo linasifika kuwapindua viongozi shupavu duniani wasiokubali kuwekwa mfukoni sasa linaonja shubiri ya dawa lililobuni lenyewe. Hii ni kutokana na uoza na uhovyo wa mfumo wa Marekani ambayo, kimsingi, ilianzishwa kwa misingi ya kikandamizaji na kinyonyaji. Rejea taifa hili lilivyoneemeka na utumwa ambao uliwahusisha mamilioni ya Waafrika kwa miaka zaidi ya 400. Rejea kuendelea kuendeshwa na mfumo wa kibaguzi ambao uliwadhalilisha watu weusi hadi miaka ya 70. Rejea ubaguzi wa chini chini wa kimfumo unaoendelea kwenye taifa hili sawa takribani karibu nchi zote za kimagharibi. Ukiishi kwa upanga, unakufa kwa upanga, wahenga walinena.
            Trump, mfanyabiashara mwenye kutia shaka amefanikisha kitu kimoja, yaani kuufichua na kuutumia udhaifu wa kimfumo kuiadabisha Marekani kiasi cha kuumbuka tena ndani ya masaa 24. Kama ni kipigo, hiki ni kikubwa cha muda mfupi kuwahi kulikumba taifa lolote. Hakika, tarehe 6 januari, 2021 ibaki kuwa siku ambayo Marekani ilivuliwa nguo na kuhujumiwa na rais wake mwenyewe. Ama kweli mjenga na mbomoa nchi ni mwananchi mwenyewe–––saa nyingine anaweza kuwa rais wake–––kama ilivyotokea Marekani.
        Baada ya Trump kuchochea kile ambacho wachambuzi hata viongozi wengi wa Marekani, akiwamo Rais Mteule Biden, walikiita jaribio la mapinduzi, maasi, ugaidi wa ndani, ujambazi, uhuni na kila aina ya majina, wapo wanaodhani kuwa ni wakati mwafaka kumtimua Trump toka madarakani hata kama amebakiza siku chache muda wake kikatiba kuisha. Kimsingi, Trump ameichafua Marekani kiasi cha kuiumiza vibaya–––taifa linalojiona kama mhimili, mshitiri na mwalimu mkuu wa demokrasia duniani hata kama misingi na sera zake vinatia shaka. Kitendo cha Trump, licha ya kutia aibu taifa la Marekani, kimefichua uoza wa kimfumo ambao ulimwezesha mtu anayesifika kwa uongo na majigambo kuchaguliwa kuwa rais wakati alionyesha wazi kutofaa kuongoza hata mkoa achia mbali nchi. Wengi walidanganywa na utajiri wake wa kutia shaka na uongo.
Chanzo: Nipashe Jpili.

No comments: