The Chant of Savant

Wednesday 13 June 2012

Badwill ni mfano wa ‘Wezimiwa’ wetu


BAADA ya Taasisi ya Tupo Kula na Kuipamba Rushuwa (TAKOKURU) kumtia mbaroni mwizimiwa Ommy Badwill kwa kutaka kupokea rushuwa, kijiwe kimekaa kama kamati kusukuti hali ikoje.
Awali kijiwe kilitaka kumjadili Ben Makapu aliyekuja na mpya kuwaambia mapaparazi mjini Arusha wamuache kwani ana matatizo yake. Hata hivyo badala yake Dk. Mpemba amekuja na mada nyingine ya wezimiwa wetu!
Akiwa amebeba nakala ya gazeti hili, analianzisha; “Yakhe mie nchi hii Wallahi yanshinda.”
Kabla ya kuelezea dukuduku lake, Dk. Mbwa Mwitu anaingilia: “Dk., mbona hueleweki, kwani nchi yakushinda kama ilivyomshinda NK miaka saba iliyopita?”
Dk. Mpemba anakatua mic: “Wala siongelei huyu, mie naongelea huyu mtuhumiwa mla rushwa aliyepewa kura kumbe ala rushwa.”
“Ala kumbe! kumbe unaongelea huyu mwezimiwa Ommy Badwill! Mbona wapo wengi sema mwizi ni yule akamatwaye kwenye tendo,” Dk. Mbwa Mwitu anatongoa.
Dk. Mipawa hataki kuachwa nyuma. Anakwanyua mic: “Nkwingwa kumbe hujui kuwa wengi wa waliojaa mjengoni ni wezi wa kawaida sema hawajakamatwa? Hivi wale walioghushi vyeti vya kitaaluma wadhani nini kama si wezi wa kawaida wanaotumia sifa wasizokuwa nazo kupewa mshiko?”
Profesa Dk. Mfilisofe anakwanyua mic kuweka mambo sawa kutokana na utata wa suala hili ambapo wengi wanaona kama ni gereshabwege kumkamata mwizimiwa.
“Usemayo Dokta Mipawa ni kweli. Wezi wako wengi kuliko huyu Badwill. Kosa lake ni kufichua mchezo mchafu ambao umekuwa ukiendelea kwa miaka mingi. Nyie mlidhani hii mikataba ya kijambazi inasainiwa bure? Wanaofanya hivyo si kwamba ni wajinga bali waroho ambao wamegeuka wapumbavu kutokana na kutumia matumbo kufikiri badala ya vichwa.”
Kabla ya kuendelea, Dk. Maneno anachapia: “Profesa Dokta Mfilosofe usiogope sema wanatumia masaburi kufikiri kama yule jamaa wa site anayetumia masaburi kufikiri hadi anaigawa Udau na mzee Mkaidi Lion.”
“Dk Mipawa hapa umetoa bonge la pwenti. Maana kama tutachunguza vipato vya hawa jamaa wengi wataishia gerezani kama siyo geresha ya Takokuru. Hivi mtu kama Ewassa analipwa marupurupu ya ustaafu upi wakati aliiingiza kaya kwenye balaa kutokana na Richmonduli yake?”
Tulisahau kuwajulisha kuwa kijiwe kimetembelewa na wageni toka mjengoni ambao ni Livingjiwe Lushindo aka Bwana Matusi, Sofi Lion. Tutajitahidi kila kikao tukaribishe baadhi ya watendaji au wahusika lau kwa dakika chache tusikie mawazo yao. Hivyo naona nao wanapaki mashangungu yao na kutia guu.
Baada ya kushuka na kukaa kwenye benchi, Profesa Dk. Mfilosofe anawapa brifingi ya kilichokuwa kikiendelea.
Anaanza: “Wapendwa wageni wetu wezimiwa na mafisi sorry mafisadi sorry mashufaa, tulikuwa tukijadili jinsi mwenzenu alivyonyakwa na Takokuru akivuta njuluku za rushuwa. Je, mna msimamo gani?”
Sofi anadaka mic hata kabla ya Profesa Dk. Mfilosofe hajamaliza: “Kwanza wewe huna adabu. Unawezaje kutuita sisi wezimiwa badala ya waheshimiwa, mafisi na mafisadi wakati ni viongozi wako?”
Kabla ya kuendelea, Lushindo anamwingilia: “Hawa ni matokeo ya makosa tuliyofanya kuwaruhusu kuwa na uhuru wa kusema. Ila mkiendelea hivi mjue askari magereza watawachanja chale kwenye makalio yenu ili mshike adabu. Hamtachanjwa kwa nia ya kugangwa bali kufundishwa adabu, na huko hakuna huruma ya profesa Maji Mafupi.”
Huku povu likimtoka anaendelea: “Wewe unayeitwa msomi usijifanye mtoto wa mjini. Hujui kitu. Sisi tumeishafanya kila kitu hapa mjini hadi magerezani. Tumeishafanyiwa kila mchezo mchafu amini.”
Akiwa anapokoma kila mtu anaanza kuguna kwa kinyaa na aibu kugundua kuwa jamaa ni mtoto si riziki anayekiri mwenyewe hadharani kufanyiwa mchezo mchafu.
Profesa Dk. Mgosi Machungi anaamua kuokoa jahazi.
“Wagosi tikubaiane. Timekuja hapa kuongeea wizi wa Badwill na Takokuru. Mambo ya mmeishafiwa astaghafiiai kawambie wake zenu, kama huna mke kwambie mwenzie Sofi Changubaka maana yeye ni open cheque.”
Baada ya Livingjiwe Lushindo na Sofi Changubaka Lion kuona mambo yamekuwa magumu waliamua kutoka mkuku kupanda mashumbwengu yao huku tukiwazomea na kuwarushia viatu.
Kama siyo Dk. Mpemba kuingilia kati, nilitaka niamke na kunyonga mtu hadharani. Bahati yao Dk. Mpemba alinizuia na ninamheshimu.
Baada ya hao wajalaana kuishia, tuliendelea na kijiwe kama kawa. Profesa Dk. Mfilosofe aliendelea kutoa dozi: “Nimewashika pabaya kiasi cha kuongea kimasaburisaburi.”
Anyway hayo tuyaache. Kimsingi, ni kwamba hiki kilichofanyika yaweza kuwa vita mitandao. Maana yake nini? Ni kwamba wengi japo si wote wanakula rushuwa na hawakamatwi kutokana na ukweli kuwa katika kaya hii hakuna walarushuwa kama Takokuru wenyewe.
Ukitaka kujua nimaanishacho kaangalie mimali waliyojirundikia. Kwani hatuwajui?”
Wakati tukiwa tunatafakari pwenti za Profesa Mfilosofe, Dk. Mchunguliaji ambaye alikuwa hajalonga muda mrefu alikwanyua mic.
“Mambo yote tisa, kumi ni pale Badwill angekuwa mbunge wa upingaji. Kile kijimama cha Makidamakida kingekuwa kimeishapitisha hukumu ya kumvua ubunge. Kwa vile kobe wote wana magamba, ni kobe gani atamvua gamba mwenzake wakati wote wanayo?
Hata hao vihiyo na vilaza waliojazana mjengoni wanalindwa na kuwa wanachama wa magamba. Wangekuwa wa magwanda wangeishatimuliwa zamani gani!”
“Hukusikia juzi Nepi Mapepe pale Janguani akiwafunga kamba watu kuwa watamshughulikia kwa vile amefichua siri kubwa ya chama cha magamba,” alidakia Dk. Meneno.
“Hapa hakuna cha kumshughulikia. Kama waliwashindwa akina Endelea Chenga, Mustaafu Mkulu na majambawazi wengine tunaowajua waliokwiba mabilioni huyu watakuwa wanamwonea kwa vile huenda yuko kwenye mtandao tofauti na wakuu,” aliongezea Dk. Mipawa.
Nami sikuona haja ya kujivunga, nilikwea mic na kusema: “Mnakumbuka Daudi Kafulia aliwaambia huyu jamaa na wenzake walivyo vibaka wakamtumia yule mtoto si---- so, Jimmy Kumbatia kutaka kumtimua ingawa naye alikuwa na tamaa zake za kisiasa?
Tukiwa tunaendelea kutongoa mistari si yule mara tukaona minjago inakuja kwetu kututimua wakidhani kuwa sisi ni wanauamsho. Tulikimbiaje?
Chanzo:Tanzania Daima Juni 13, 2012.

No comments: