The Chant of Savant

Friday 1 June 2012

Rais anafaidikaje na jinai hii?





Hii ni mara ya pili kuandika barua ya wazi kwa rais. Sifanyi hivyo ili kutafuta ujiko au kuwa karibu naye ili nipewe ukuu wa wilaya au hata wa mkoa huko tuendako. Sina shida na ukuu wowote zaidi ya kuwa na shida moja-kumkubusha ndugu rais awanusuru watu wetu na taifa letu toka kwenye kadhia na jinai vinavyozidi kubarikiwa na kuhalalishwa wakati ni janga kwa taifa.
Nakumbuka mwaka 2006 rais Jakaya Kikwete aliwaambia umma wa watanzania kuwa ana orodha ya wauza unga, majambazi, wala rushwa, hata wezi wa bandarini kutaja wachache. Hii ikiunganishwa na ahadi yake aliyotoa ya maisha bora kwa watanzania wote, kwa rais makini na mkweli, unapata jibu kuwa kweli kuna maisha bora yaliyoahidiwa. Lakini kwa upande mwingine ukijumlisha ahadi za rais na kutotimiza hata moja, unapata jibu japo chungu kuwa maisha bora kwa watanzania ilikuwa ni changa la macho kama wasemavyo watoto wa mjini.
Leo kwa mara nyingine naandika barua hii kwa rais ingawa ni ya wazi. Naandika kumkumbusha jambo moja kati ya mengi anayopaswa kukumbushwa. Naandika kumkumbushia kuwashughulikia wauza unga ambao kwa sasa umekuwa balaa la kitaifa. Ingawa wachache, tena viongozi wakubwa kama alivyodai mchungaji mmoja hivi karibuni, wanapata utajiri wa haraka na wa kutisha, taifa linaangamia. Sijui ni rais gani anataka kuongoza taifa linaloangamia au kuacha historia kuwa alifanikisha biashara ya mihadarati? je rais ananufaika vipi na biashara ya mihadarati kiasi cha kuendelea kuifumbia macho wakati ana orodha ya wauzaji?
Kwa maneno mengine, ukimya wa rais unafanya watu waanze kujenga dhana potofu kuwa kuna jinsi rais au watu wake wanafaidika na biashara hii hatari. Ni juzi juzi tuliambiwa kuwa ulikamatwa unga kule Mtwara ukiwa unasafirishwa na mtoto wa Amatus Liyumba aliyewahi kufanya kazi benki kuu na kuishia kusababisha upotevu wa mabilioni. Kesi hiyo imefikia wapi? Haisikiki tena. Juzi juzi alikamatwa mdogo wa mfanyabiashara tata Rostam Aziz aitwaye Abdulrasul. Ajabu kesi yake ilikimbizwa kama gari la wagonjwa na kuachiwa haraka huku akiacha walalahoi wakiteketea na mambo yakaishia hapo kana kwamba kilichofanyika ni kitu cha kawaida! Je tutapigana na vita ya mihadarati kwa kukangalia umwenzetu na urafiki au kuna faida nyuma ya pazia wakuu wanapata kama alivyodai mchungaji? Je namna hii mnamdanganya na kumfanya mpumbavu nani?
Kutokana na kesi ya hii ya mdogo wake Rostam imefikia mahali watanzania wamejenga dhana kuwa huyu jamaa ana hisa kwenye serikali ya Kikwete kutokana na mkono wake kuwa karibu kila mahali. Nenda Kagoda, utaambiwa Rostam. Nenda Richmond, yupo Rostam. Na sasa mihadarati, Rostam anatajwa. Na ushahidi zaidi ni kwamba kila uchafu unaofanywa na Rostam hashughulikiwi mtu kutokan ana ukaribu wake na ushirika na rais.
ingawa wasiojua sheria na jinsi ufisadi na jinai hii vinavyolindwa wanawalauma majaji kwa kutoa hukumu iliyoonekana kumpendelea ndugu yake Rostam, ukweli ni kwamba mfumo wetu ndiyo unawezesha haya na rais analijua hili. si siri kuwa, kisheria, ukitaka kumsaidia mharifu unamfungulia mashitaka chini ya vifungu visivyo kisheria na jaji anatupilia mbali shitaka au kutoa haki kwa mhusika hata kama hakustahili. Kinachofanya wakubwa walaumiwe kwa uchafu huu, ni ile hali ya kutumia udhaifu huu kupitisha na kusaidia watu wao. Hakuna ubishi kuwa hukumu iliyomwachia mdogo wake Rostam ni pigo kwa mapambano dhidi ya mihadarati. Kinachogomba ni ukweli kuwa kumbe rais anawajua wauza unga lakini hawashughulikii. Hata wachovyo na mafisi fulani wakitumia vifungu vya sheria vibaya kuwaachia hakuna anayejali. Mbona, kwa mfano, katibu mkuu kiongozi wa zamani Philemon Luhanjo alipomrejesha ofisini kinyume cha sheria katibu mkuu wa zamani wa wizara David Jairo rais aliingilia kati? je kama hakuna namna mbona Kikwete haingilii kati kwenye suala zima la kuachiwa huru kwa mdogo wake Rostam? ni kwa sababu ni mdogo wake Rostam mshirika wa Kikwete na mwezeshaji mkuu katika kutunisha mtaji binafsi?
Itakuwa ni utoto wa ajabu kwa watanzania kuendelea kuamini kuwa Kikwete anaweza kupambana na wauza unga iwapo watu wake wa karibu wanaachiwa hivi hivi nan aye anajifanya kutojua.
Umefika wakati wa kumbana Kikwete ashughulikie wauza unga aliodai ana orodha yao. Maana miaka inazidi kuyoyoma nasi tunapewa matumaini ya kitoto ya kesho kesho. Wahenga walisema kesho huwa haipo na ukitaka deni njoo kesho kwa maana ya kuwa hutapewa mkopo. Kwanini tumeligeuza taifa letu kuwa la waharifu na jinai? Ajabu ya maajabu tunaendelea kuwaheshimu waharifu eti kwa vile wana pesa au wako karibu na wakubwa. Rais Kikwete tafadhali shughulikia wauza unga kabla ya kuondoka ofisini. Kama utaamua kunyamaza kama kawaida yako, uje siku moja utakuja kuulizwa na namna utakavyoulizwa haitakuwa ya kufurahisha kwako binafsi na taifa. na isitoshe, wafanyabiashara wenye pesa itokanayo na uchafu huu watakuabudia leo kwa vile uko madarakani. Ukishaachia madaraka watakukimbia na hata kutoa ushahidi dhid yako. Mungu epusha mbali hili lisikutokee ingawa laweza kutokea kama hatua madhubuti kupambanana jinai hii hazitachukuliwa mapema.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 30, 2012.

No comments: