INAONEKANA kuna jambo limetokea. Maana Mgosi Machungi anavyoingia kijiweni kwa furaha si bure. Isitoshe tangu siku hizi zimtembelee, haachi kununua gazeti lau akifika nyumbani bi mkubwa ampokee bwana mkubwa aliyetoka kwenye misheni bab kubwa. Anyway, hayo ndiyo maisha ya Bongo ambayo wengi ni misheni tauni.
Mbwa Mwitu hangoji. Anamvamia Mgosi akisema; “Mgosi kunani leo mbona umechangamka utadhani umeshinda bahati nasibu?”
Mgosi anajibu: “Mgosi hata huamkui! Hiyo bahati nasibu tishinde sisi? Huwa sishiiki wizi wa matamasha na mashindano ya umaskini kama yanavyoendeshwa na baadhi ya makampuni ya telephone yanayowaibia wachovu kila siku na kuwaletea kiini macho cha jishindie mifedha.”
Mbwa Mwitu anazidi kujifanya mtabiri: “Au ni kwa vile mwezi mtukufu umepita na sasa unaweza kujichana ulabu na makandokando yake?”
Mgosi anachukia na kusema; “We kafii mkubwa. Kumbe ulikuwa umefunga Amadhani tu.
Wakati Mgosi na Mbwa Mwitu wakiendelea kuchambuana anaingia Msomi Mkatatamaa. Leo inaonekana ni fasheni ya kununua magazeti. Maana naye analo. Anatuamkua na kumwaga stori.
Anaanza: “Wazee mmeona mzee mwenzetu wa viwango alivyofufuka na kuja na hoja za maana kwa kaya?”
Anafunua gazeti na kuonyesha habari inayomkariri mzee Sam Six akisema kuwa ubunge wa msukule ni mzigo kwa kaya. Hivyo, katiba mpya ihakikishe inaupiga stop.
Kabla hata ya kuendelea Mgosi anakwanyua mic: “Mgosi umenikuna kwei kwei.”
Mzee Maneno anachomekea: “Amekukuna wapi na vipi?”
Mgosi hamkawizi: “Mzee Maneno tiheshimiane. Tatizo la nyinyi ni kufikii kichinichini. Ndiyo maana wabunge msukule wanaupata ulaji tena wengi kwa kutumia sera za chini chini. Wangekuwa na sera za juu juu tungewaona kwenye kampeni juu juu kwenye majukwaa wakitoana jasho na wenzao hata kama wote hawana maana.”
Anajifuta jasho na kuendelea: “Msomi umegusa hapo hapo palipofanya nifuahi hadi nilipoingia watu wakajua nina fuaha leo. Hakuna kitu kilikuwa kinaudhi na kunichefua kama huu ubunge maalumu ambao kimsingi ni mzigo kwa kodi zetu. Hawa huwakilisha matumbo yao na mambo yao ajabu tunawalipa!”
Kabla ya kumaliza mzee Mipawa anachomekea: “Beng’we hapa mami Six ametoa bonge la pointi. Namuona kama anafaa kuwa rais japo yuko kwenye chata la hovyo, mizengwe na mafisadi.”
Kanji anamkata mzee Mipawa jicho la chuki. Huyu ni mwanakijiwe wetu ambaye alikuwa zake likizo India na Uingereza alikokwenda kutumia baada ya kuchuma huku kwenye shamba la bibi.
Anasema: “Veve Pava ovyo sana. Kwanini sema chata ya Six ovyo. Hovyo hovyo mama yako. Veve hapana ona hii amani vatu yote nafaidi au pinzani wewe.”
Mzee Mipawa anakuja juu: “Mami usinichefuege nikakufanyiaga kitu mbaya. Hiyo amani waiona wewe unayeweza kuchuma hapa na kwenda kulia kwenu. Huna tofauti na hao waishiwa msukule wanaowakilisha matumbo yao. Nakushauri unyamazage nisije fanyaga kitu mbaya.” Baada ya Kanji kuona Mipawa anakuja juu, anaamua kushusha hasira yake na kumtania: “Veve Sukuma ya vapi isiyopenda tani?” Anasema huku akicheka. Anamwambia muuza kahawa: “Veve uza gahawa. Hebu Tia yeye moja.”
Mipawa kuona hivyo anaamka kutaka kumkaribili Kanji. Anasema: “We inaonekana hunijuagi. Kama unadhani mie ni mtu wa kuhongwa kashata na kahawa kama Msukuma yule mjinga Mzee wa Vijenti umenoa. Kawahonge hao vyangudoa wa kisiasa, lakini si mimi Ng’wana Jilala wa Danga Nkulu wa Maduhu wa Ng’wana Kang’wa wa Sheta wa Shikome.”
Anasimama ili kumkabili Kanji akisema: “Ngoja nilikong’otege linijuage. Beng’we!”
Kuona maji yanaanza kuzidi unga, mimi na msomi tuliamua kuingilia kusuluhisha sintofahamu hii.
Msomi alisema: “Nkwingwa huna haja ya kupigana. Aisifiaye mvua jua imemnyea. Kanji hawezi kuona upande wa pili iwapo anakula na vipofu tena vichaa. Nadhani unanielewa. Haya tuyaache. Tujadili hoja ya viti vya uishiwa wa dezo aka msukule. Kanji ni mtu mdogo na saa nyingine maskini kama wewe sema hujui. Si kila Mhindi ni tajiri au fisadi. Lazima tuwe fea kidogo jamani hata kama kuna mambo madogo madogo kama ubaguzi utokanao na ujinga na historia ya kubaguliwa. Enewei, haya tuyaache.”
Kanji anaonekana kunywea kama mbwa aliyenyeshewa mvua. Anatabasamu asijue la kusema.
Msomi anaamua kuunganishia humo. Anasema: “Kwa mara ya kwanza tangu afanyiwe mizengwe, brother Six ameni-impress sana. Methinks I’ve to meet with him and accord him my appreciations.”
Kabla ya kuendelea Mpemba anaingilia kati. “Yakhe huo Ukameruni sasa tuu machi. Yakhe ongea Kiswahili japo nasi tuelewe wallahi.”
Msomi anatabasamu na kusema: “Samahani. Huwa nikifurahi au kuchukia Ukameruni huwa unakuja tu. Anyways, kwa ufupi, nilikuwa namuona brother Six kama mchumia tumbo aliyewekewa mizengwe kwenye uspika akaogopa kuhama chama chake cha mizengwe. Kumbe jamaa ameamua kupigana kutokea ndani japo kwa chama chake si salama.”
“Naona jamaa ameamua kuwaharibia wenzake wanaotaka kumwekea mzengwe mwingine. Naamini mara hii hatakubali kuendelea kukaa kwenye chama chenye mizengwe. Utaniambia,” anasema Kapende ambaye alikuwa kimya muda wote akisoma habari za misukule.
Mzee Kidevu naye anaamua kuvunja ukimya. “Mie simwamini Mbongo. Anaweza kujifanya kusema mambo ya maana ila ukifika wakati wa kufanya kweli ukashangaa ukasikia amenywea kama alivyofanya pale bwana Richmonduli alipoamua kumnyang’anya uspika na kumsimika yule mama. Kama anamaanisha kujitofautisha na mafisadi aamue kujiondoka mara moja vinginevyo ni michosho yao.”
“Kwei pesa ya dezo ni ya dezo. Muiona jinsi waishiwa wa msukule wanavyoshindana kufungua foundations za uongo na ukwei. Wana shida gani iwapo pesa yenyewe wanaipata dezo? Utasikia Katheine Foundation mara Njusi Foundation muadi ulaji mtupu. Sasa tutawaona,” anasema Mgosi huku akikwanyua kombe lake na kulibusu.
Mbwa Mwitu naye anaamua kutia timu: “Una habari tusiposhupalia viti maalumu kuna siku vitaanzishwa viti maalumu kwa ajili ya wanaume wanaodundwa na wake zao.” Anamalizia akimkazia macho mzee Kidevu ambaye tulizinyaka kuwa bi mkubwa huwa anamtia adabu.
Mzee Kidevu anakuja juu: “Mbona wanitolea mimacho?”
Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga si likaja shangingi la muishiwa maalumu. Kwa hasira za kuibiwa kodi zetu tulilimwagia kahawa na kutawanyika.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 14, 2013.
|
|
4 comments:
Sita mwenyewe amekanusha kauli yake hiyo. "Ni maadui wake wa kisiasa", amedai.
Basi nami ni adui wake wa kisiasa kwa vile nimeeleza ukweli wa kile alichosema. Kama ukisoma maneno haya, "Mzee Kidevu naye anaamua kuvunja ukimya. “Mie simwamini Mbongo. Anaweza kujifanya kusema mambo ya maana ila ukifika wakati wa kufanya kweli ukashangaa ukasikia amenywea kama alivyofanya pale bwana Richmonduli alipoamua kumnyang’anya uspika na kumsimika yule mama. Kama anamaanisha kujitofautisha na mafisadi aamue kujiondoka mara moja vinginevyo ni michosho yao.”
Sitta ni mnafiki, maneno mengi tu!
Heri Sitta angekuwa mnafiki. Ni mpuuzi na mchumia tumbo na changu wa kisiasa anayepaswa kudharauliwa na kuzodolewa kwa woga na kutapatapa kwake. Shame on Sitta!
Post a Comment