Baadhi ya wateja wa Airtel wakijichana futari iliyoandaliwa na kampuni hiyo.
MIMI huwa sipendi unafiki. Wasiojua kitu huita hali hii uswahili japo ni makosa. Nakipenda Kiswahili ila sitaki kinipende hata kama sitakiponda kikitumika vibaya”.
Mzee mzima naingia nikilalamika. Naongeza: “Mbu mbwa wanajua Kiswahili. Mbu aliyezoea mosquito coil ukimpulizia doom anasema nyooo hunipati.
Wajua hata kunguru wanajua Kiswahili. Paka ndiyo usiseme. Hata kufuru ya mzee Idd Lion na Elieza Fenesi wajua pia.”
Mbwamwitu tuliyekuwa tumeongozana kuelekea kijiweni akinisikiliza aliamua kuniunga mkono kwa kukwanyua mic. “Siku hizi hata vyangudoa wanaongea Kiingereza ili wawapate watasha, siyo kajamba nani, mavi matupu.
Nasikia na watasha wenyewe wengi ni ape alolo huko kwao. Utamsikia changua akisema: “Me, my milk is standing,” akimaanisha kuwa “manyonyo bado mchomo”.
Sina mbavu kwa jinsi anavyoonyesha ishara ya manyonyo tena akionyeshea kifuani mwake.
Kumpa tafu naendelea. “Hata wahishimiwa mjengoni hawamalizi vikao bila kubukanya na kuvuruga ung’eng’e. Utamsikia mtu akiongea kiswangilish kisicholeta maana lakini akatoka anajiona kuwa wameipata kuwa yu msomi wakati alighushi. Huu nao unafiki pia. Nadhani ndiyo maana wengi wa walioghushi wanaendelea kuula na kutupuuzia.”
Mgosi Machungi aliyekuwa nyuma yetu akinyata bila sisi kujua anachomekea: “Tate nane tane hei wangeongea kishambaa wakaeeweka kuiko kutichanganya”.
Huku tukicheka kwa jinsi alivyotupata Mbwamwitu anakula mic, “Mgosi umetufumania kweli kweli.”
Mbwamwitu anazidi kulikoleza akikandia Kiswahili, “Kiswahili kina mipaka. Kama unaenda majuu ishia Kipawa. Kama unaelekea Kenya ishia Namanga au Horohoro. Kama unaingia kwa M7 ishia Mutukula hata kama hujala”.
Naamua kumuunga mkono: “Hata Bongo kwenyewe kuna sehemu ukiingia ukachonga Uswa wako watu wanakutolea mimacho utadhani si Waswahili. Ifikie kipindi tukubaliane kuwa dunia imechenchi.
Hekaya za Abunwasi siku hizi hazina dili. “Karudi baba mmoja” siku hizi haionekani si darasani, mtaani wala duka la vitabu liwe la ubaoni hata maktaba.
Siku hizi watu wanaongea digatali. Ukifungua kompyuta ni Kiingereza. Jamani biashara ya kimataifa si nazi na ubuyu.”
Mgosi anaonekana kutokubaliana nasi: “Mimi sikubaiani nanyi. Kwanini kwa mfano, wahishiwa wasiokijua kimombo wakiazimishe wakati wae wanaowawakiisha mjengoni hawaujui huo umombo kama siyo uimbukeni?”
Mjadala wetu ulikatishwa nasi kufika kijiweni na kumkuta msomi Mkatatamaa, Mpemba, Kapende, Mipawa, Mzee Kidevu na Maneno na Mchunguliaji wakitungoja.
Baada ya kuamkiana tunapewa miniti ya mkutano wa siku hiyo ambao ni juu ya ujambazi wa Mwanasharia mkuu wa li siri kali aliyekula rushua na kuharibu kesi ya Idd Lion yule mwizi maarufu aliyeachiwa hivi karibuni.
“Huu ndiyo unafiki nisioutaka mimi. Kama afisa wa lisirika anashirikiana na mibaka yako wapi mantiki ya kuwa na ofisi tena kubwa kama hiyo?” Nachomekea tena.
Mpemba analianzisha: “Hivi huyu nzee Idd Lion naye ana dini au tapeli? Je, naye amefunga mwezi ntukufu?”
Msomi anauliza: “Mpemba kufunga kwa Idd Lion Mwizi kusikuhangaishe iwapo anaweza kuibia wachovu. Hivi siku hizi hujui wapo wanaofunga kinafiki na mazoea? Umemuona bi Mkubwa Salmae Kikwekwe akijifanya kufuturisha wachovu akiwa na kidosho wa Bulair ambaye alikuwa ameulamba kikafiri na jamaa zetu wasihoji?
“Unafiki mkubwa. Ukisikia ukafiri ndiyo huu japo wengi hawataki kuulaani. Nani ahoji wakati wote ni waganga njaa? Huoni makampuni yanayowaibia yanavyoshindana kufuturisha wakati hayana dini? Alaye na kutoa futari kama hii naye kafiri. Kwanini mwezi mtukufu unajisiwe na majizi kwa vile eti wana pesa?
“Hivi haya makampuni, kwa mfano ya virongaronga, yanayotubamiza mkenge kila uchao yana dini kweli au ni kuzidi kuwaingiza mkenge wachovu?”
“Nsomi usitake mie nkufuru Wallahi. Juzi nilimpigia simu nke wangu kule Peemba na kuambiwa eti simu ninayopiga haipo wakati ipo? Nilipong’ang’ania nikaambwa sina salio wakati nilikuwa nimetoka kuweka elfu tano. Eti hawa nao wafuturisha au wakufurisha?” Mpemba anaongea kwa uchungu.
“Mie hakuna watu nachukia kama wale wapandishao bei za vyakula na bidhaa nyingine mwenzi wa Ramadhani halafu wajidai nao wana dini. Hawa dini yao pesa siyo nyingine wallahi mie nasema,” Mpemba anazidi kutoa dukuduku lake.
“Unashangaa kupanda bei za bidhaa? Kuna siku watu wengi watafuturu pesa haramu hata ya mihadarati wakati wakijua fika kuwa wanaowafuturisha si watu chochote bali majambazi. Kesho utamsikia ndugu yetu Ewassa naye anafuturisha pesa ya Richmond. Hata huyu mzee Lion anaweza kufuturisha watu pesa aliyochomoa Uda.” Anaongezea mzee Mipawa huku akiungwa mkono na Kapende anayetikisa kichwa chake kwa nguvu zake zote.
Kwa vile Kapende alikuwa hajatoa mchango, anaamua kumwaga sera zake naye. “Tangu kaya yetu igeuzwe uwanja wa mapromosheni uchwara na ufuturishaji wala mimi sina hamu na hawa watu. Kwanini uibie watu halafu ujidai unawafuturisha?”
“Wazee msijisumbue bure. Baada ya wezi wa pesa ya umma kugundua kuwa wanaweza kujitakasa kwa kupeleka pesa yao chafu kwenye shughuli za Mungu basi kila jambazi atafanya hivyo ingawa ni kujidanganya,” Anasema mzee Maneno huku akijipanga vizuri kwenye fomu.
“Usemayo ni kweli. Hebu jaribu kufikiri kusikia alhaji profesa fulani eti naye anafunga wakati biashara yake ya baa ni haramu tupu. Huyu kweli ana tofauti na mzee Lion wa Idd?” Anaongezea Mchunguliaji ambaye kwa muda wote alikuwa akichungulia gazeti. Alivutia na kisa cha kuweweseka kwa Nambari wani pale Chakudema ilipotishia kuanzisha vikundi vya kupambana na wizi wake.
“Mkuu Mchunguliaji unashangaa haya. Jamaa wameishiwa kulhali na kila wanachofanya ni makufuru matupu. Hebu waulize. Wako wapi waliolipua mibomu kule Arusha? Wako wapi walioficha njuluku zetu Uswisi? Wako wapi walioiba mabilioni ya njuluku kwenye ujio wa Obamiza? Wizi mtupu. Kufuru tupu. Eti nao watajivuna wana dini. Dini au duni? Shame on them all.” Anamalizia kwa kukanyaga ukameruni ambao huwa haumwishi kila apatapo nafasi ya kuchangia.
“Wengi tulidhani kuwa ufisadi lau ungepungua wakati wa mwezi ntukufu. Kumbe watu ndiyo wanazidi kufuru!” Anarejea Mpemba kwa lafudhi yake ya Kipemba kama kawa.
Tukiwa tunashangaa makufuru ndani ya mwezi mtukufu mara anatokea mlevi aliyeupiga chakari akiwa anajiimbia nyimbo za Kiarabu.
Mara gari la mzee Idd Lion linapita nasi tunaamua kulimwagia kahawa kwa hasira zetu.
Wabillahi tawfiq.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 7, 2013.
No comments:
Post a Comment