The Chant of Savant

Saturday 10 August 2013

Mlevi apanga kufanya biashara ya bwimbwi


Baada ya vyombo vya umbea kuripoti kuwa siku hizi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Mchonga unatoa nafasi kwa wauza bwimbwi kupitisha `kago’, mlevi nimekuja na mkakati mzito wa kujiingiza full masinonda kwenye hii kitu.
Nani asiyependa `kuukata’ tena kirahisi kama ilivyo kwenye kaya kwa sasa ambapo kila jambazi analala apeche alolo na kuamka bilionea?
Nani anajua historia za ukwasi wa watu kama vile Roast tamu L Aziz wa Kagoda, Moody Deweji, Idd Azaham, Get Rwakataree, Alexio Masawewe na wengine wengi?
Si walifanya mambo wakaukata na hakuna anayewabughudhi zaidi ya kuwaita wafanyabiashara mashuhuri.
Ukiukata hata kama ni jambazi wa kawaida utapewa majina makubwa tu.
Tangu walevi walipoamua kujikaanga wenyewe kwa kusema eti ujanja kupata, hata kama unafanya jambo lisilo jema, utaheshimiwa. 
Kila mlevi anaweza kuuibia umma, kuuza bwimbwi hata kutapeli kisiasa na kuula.
Hamjasikia wale wazito walioghushi shahada na kuitwa madaktari wakati ni vihiyo? Nani anabughudhi ulaji wao zaidi ya kuongezewa vyeo?
Hamkusikia kuwa mzee wa Rada aama Vijisenti ameingiza kaya mkenge mwingine kwa kusuka lile kampuni la Kikameruni la BaE, kupewa ulaji mwingine? Hii ndiyo kaya ya walevi bwana. Usipokula utaliwa.
Kwa kuwa Mkuu ameonyesha kugwaya hii kitu, lazima niingie kama sina akili nzuri.
Hakuna sanaa ziliniacha hoi kama jamaa zangu wa kusaidia kuenea kwa bwimbwi kusema eti mkuu aliwapa majina ya wauza bwimbwi. 
Hata hivyo, mbona bwana Katoo amekanusha kuwa hakuna cha kupewa majina zaidi ya sanaa na hakuna aliyekanusha?
Yaani katika kulindana na kusaka sifa tumefikia mahali hata wakubwa wanaongopa mchana kweupe! Hivi mnawafundisha nini wadogo?
Ngoja tuzidi kutumia kichwa badala ya masaburi.  Anawapa majina hayo kama nani iwapo majina yenyewe ni ya vidagaa? Bongo kweli bongo bondoogle! Sijui wanamdanganya nani kiasi cha na wao kujidanganya?
Ningekuwa mkuu, nisingejitia aibu kwa kusema eti niliwapa majina ya wauza bwimbwi washitiri wa bwimbwi. Hii maana yake ni kwamba wote ni washitiri wa bwimbwi.
Hivyo, nikifanya biashara hii watanikingia kifua kama walivyofanya kwa walioghushi na wauza bwimbwi vigogo.
Kwa vile bwimbwi na jinai vimehalalishwa kimya kimya, nitaanza kupiga kampeni kwa walevi wachangamkie biashara ya bwimbwi ili kukuza uchumi wao na wa kaya.
Bahati nzuri hakuna atakayenilazimisha kutaja utajiri wangu wala nilivyoupata. Kama wakubwa wenyewe wanapata kigugumizi kutaja mimali yao nani atanisumbua?
Jogoo aliwafundisha vifaranga ku-poo ndani ati!
Nani hataki utajiri wa haraka haraka? Hivyo wasomaji msishangae siku moja kunikuta naendesha midudu ya bei mbaya na kuishi kwenye mahekalu huku nikimiliki misururu ya biashara za uongo na ukweli.
Kwa mfano, baada ya kuvusha kago langu na kuingiza mabilioni, shurti ninunue uwanja maeneo ya wazito kule Masaki na kwingineko ambako nitaangusha bonge ya hekalu lenye kuvutia kuliko hata Ikulu.
Nadhani hekalu langu litashindana na lile na mchunaji Get Rwakataree ambalo nalo nasikia kwa jeuri ya mshiko alijenga kwenye eneo lisiloruhusiwa.
Hivyo, nafanya mipango kuwasiliana na washikaji wa Pakstani, Afghanistan na Hong Kong ili nianze kuwasukumia mizigo.
Kwa vile mimi ni mlevi na siwezi kuishi bila kanywaji, sitaweza kusafirisha kago mwenyewe hasa kwa njia ya kumeza. Bwimbwi na kanywaji huwa haviendi na isitoshe siko tayari kujigeuza shoga kubeba mimba za bwimbwi.
Jamaa yangu ambaye ni mheshimiwa fulani ‘alinitonya’ kuwa ukitaka mizigo yako ipite pale uwanjani, ima uwape ‘kitu kidogo’ watu wa Zima moto au uongee na maafisa wakaguzi na kila kitu kinakuwa mswano.
Jamaa amenifumbua macho. Nilikuwa nashangaa kuona vijana walioajiriwa juzi juzi pale uwanjani, kuwa wakwasi wa kunuka wakitukoga sisi akina yakhe kumbe hili ndilo zali lao!
Sasa watanikoma na lazima within not time niwe bilionea kama akina Roast Tamu La Aziz ambaye alichanganya karata kupitia Kagodamn akatokea kuwa bilionea.
Hapa marafiki zangu kama Yusufeli Manjii hawanizidi tena. Kumbe mambo iko uwanja wa ndege! Siku hizi mambo ni kwa bwimbwi!
Lazima nifanye haraka kuukata kabla Mkuu hajabadili kibao au kuachia ngazi.  Kwa vile alitoa `livu’ kwa wauza bwimbwi ambao alisema ana majina yao, langu halitakuwamo.
Hivyo, I’ll become a new kid in the block. Kwa vile Hong Kong na `Sauzi’ kimenuka, mizigo yangu nitakuwa natuma kupitia uwanja wa ndege wa Roma.
Hapa lazima niongee na washikaji zangu wanaofanyia biashara hii kule Ugiriki wanipe tafu ya jinsi ya kupenya uwanja huu.
Pia nitahakikisha nanunua uwanja maeneo ya Magomeni ambako wengi wa dealers naambiwa wanachangia karata zao kirahisi. Hii itaniwezesha kuwa karibu nao na kujifunza mbinu mpya.
Pia maeneo ya Sinza Uzuri na Palestina lazima nako niwe na mijengo ili kuwa karibu na washirika wengine. Nikishamaliza kupata mijengo hapa lazima nitafute mkubwa wa ndata mmojawapo hasa wa kitengo cha bwimbwi na kumpa `inshu’ na jinsi tutakavyokula pamoja.
Kwa vile kaya yetu haina sheria ya kumtaka mtu aelezee alivyopata utajiri wake, nina hakika nitapeta na kupetuka kirahisi. Kunogesha `geimu’ lazima nikate mshiko kwa chama kinachoonyesha kuwa na nguvu ili nipate mshitiri kwenye `dili’ zangu.
Mambo yakizidi kuchanganya lazima nigombee uheshimiwa. Ikizingatiwa kuwa nimebukua kama sina akili nzuri, lazima nitaupata uhishimiwa.
Kama `vihiyo’ wasio na elimu au wale walioghushi wameweza kuupata, kwanini mlevi nisiupate nikaitwa mhishimiwa Mlevi Mkuu wa wakuu?
Kama nitaingia Mjengoni nitahakikisha inatungwa sheria ya kuubinafsisha Uwanja wa Mwalimu Mchonga kwetu wauza bwimbwi ili tufanye vitu vyetu bila kutolewa upepo na maafisa wa uwanjani ambao nao wametokea kuwa matajiri simply because wanakula cha juu toka kwenye `zali hili la mentali’.
Ili kuwazuga walevi, nitafungua Bureau de Change ili wadhani kuwa ukwasi wangu unatokana na kubadili `fweza’ tena za kigeni.
Pia nina mpango wa kuanzisha benki ili nizidi kuheshimiwa na kuiweka kaya mfukoni mwangu.
Ngoja niwahi uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bwimbwi kusuka laini ya kupitisha kago langu. Salamu kwa wazungu wa unga wote na wale wanaowalinda.

Chanzo: Nipashe Jumamosi 10, 2013.

No comments: