The Chant of Savant

Wednesday 28 August 2013

Usanii, Mihadarati na madini first

Baada ya washindani wake kuja na usanii uitwao “Kilimo Kwanza” Kijiwe nacho kimekuja na sera yake ya kuukata na kuwakomboa wachovu. Waijua sera yenyewe? Simpo, inaitwa Usanii, Mihadarati na Madini first. Kwa vile nao kwenye kijiwe chao cha Idodomya wanatumia Kiswanglish tena uchwara, kuna tatizo gani nasi kutumia kiswangilish tena grammatical?
Basi, baada ya wanakijiwe kusukuti jinsi ya kupambana na ukapa, ukwete na ukata, wamekuja na uvumbuzi mpya. Hebu fuatilia mjadala kwenye bunge letu pale Kijiweni mitaa ya Msimbazi Shule ya Uhuru.
Mgosi Machungi, kama kawaida yake, amewahi kijiweni. hii ni kutokana na bi mkubwa wake Nengoma kumkoromea jana baada ya kurudi nyumbani bila kitu mfukoni.
Akiwa ameudhika anaanza, “Wazee nina mpango wa kujikomboa kimaisha. Maana jana hatikulala.”
Kapende anauliza, “Sasa kutolala kwenu kunahusianaje na kujikomboa?”
“Kumbe hujui!” Anasema Mgosi Machungi kwa mshangao.
“Kumbe sasa nijuaje unataka niote siyo?” Kapenda anajibu.
Mgosi anaendelea, “Jana hatikulala kutokana bi mkubwa kuchukia nilipoejea nyumbani bila njuuku mfukoni.”
“Hilo mbona jambo la kawaida mgosi,” Anajibu Mzee Maneno anayeendelea, “Mie nshazoea kutukanwa na bi mkubwa kuwa ni mwanamume suruali kutokana na uchovu.”
Kicheko!
Msomi Mkatatamaa ambaye alikuwa akisikiliza huku akisoma gazeti anaamua kuchangia, “Japo mmeeleza matatizo yenu kwa lugha ya mitaani, mna hoja. Kimsingi, kinachowagomba ni ugumu wa maisha wakati muliahidiwa maisha bora kwa wote.”
Mipawa hangoji Msomi apanue hoja yake, “Ngosha, maisha bola kwa wote au maisha bola kwa wao?”
Msomi anajibu, “Umesema vyema Ngosha. tunachopaswa kuuliza ni yako wapi maisha bora na kwanini maisha bora yamekuwa ya wachache tena wahalifu kama vile mafisadi, wauza unga, watoroshaji madini na mitaji na wanasiasa uchwara?”
Mgosi hangoji, “Ndiyo maana timesema lazima tijikomboe. kama wao wanauza mihadaati na kutoosha madini na wengine kujifanya wasanii ili watooshe mihadaati kwanini nasi tisibadii sera yetu?”
“Japo hili laweza kuchukuliwa kama utani, lina ukweli ndani yake hata kama ni baya. Maana ukiona watu wanavyoibuka kupitia siasa, usanii na biashara zisizojulikana na kuukata unashawishika. Mgosi hapa umeona mbali japo si jibu kwa matatizo yetu kama kaya hata wanakijiwe.” Anasema Msomi.
Mpemba ambaye alikuwa kimya muda mrefu akivuta tasbihi yake anaamua kukatua mic, “Yakhe sie twafa kwa ukapa wenzetu waula. wajua kuwa siku hizi usanii ni njia rahisi ya utajiri? Waona wakisafiri nje kumbe wenda fanya mambo!”
“Kwaweza kuwa na ukweli kwenye madai yako Ami. Maana mie sijaelewa hawa wasanii na wahuribiri wa dini walioibuka jana kuwa mabilionea kama jamaa zangu wa viwanja vya ndege na mipakani. Lazima kuna namna wanafanya hasa kuhusiana na mihadarati na utoroshaji wa madini.” Anasema Kapende.
Msomi anakubaliana naye, “Hamkusikia yule afisa wa uwanja wa ndege wa Mwisho wa Reli alivyokamatwa akitorosha madini ya mamilioni? Je amefanya hivyo mara ngapi? Je wapo wangapi? Hapa bado hujaongelea mihadarati iliyonaswa kwa mzee Madiba kwa tani. Inaonekana jamaa wametuibia kweli.”
“Ajabu baadhi ya wapuuzi na matapeli wa kisiasa eti wanakuja na kilimo kwanza wakati mambo ni ufisadi, mihadarati, uhubiri, usanii na jinai nyingine.” Mzee Kidevu anaamua kuronga la moyoni.
Mgosi Machungi kuona hoja yake inapata mashiko anazidi kulikoleza, “Wagosi sasa tiamke toka kwenye usingizi wa pono. Kama Kijiwe tianzishe sera ya kuwa wasanii na baadhi yetu kama msomi waombe kazi uwanja wa ndege ili tipitishe kago zetu au siyo?”
Mbwa Mwitu anasema, “Mie nitakuwa mshika mkoba ambaye nitakwenda uwanja wa ndege kuwahonga jamaa ili Mipawa na Kapende wapitishe kago.” Anasema huku akiwaangalia Kapende na Mipawa ambao hata hivyo hawajali sana.
Mara Kanji anaingia. Anasalimia na kukaa na kuomba awekewe kahawa. Anamtania muuza kahawa, “Veve kwanini nashanga mimi? Tia gahawa veve siyo shanga mimi kama shangaa shangaa nenda feri.”
Muuza kahawa aitwaye Shem hajibu.  Anamwekea kahawa huku akitabasamu.
Mbwa Mwitu anamuuliza Kanji, “Kanji hebu tupe siri ya mafanikio yenu.”
Kanji anajibu, “Fanikio yangu husu nini veve? Nenda fanya kazi fanikiwa veve.”
Mpemba anachomekea, “Wallahi Kanji haya matusi. Wadhani tusiofanikiwa hatufanyi kazi au twafanya kazi isiyo na faida ya kunyonywa na kulipa kodi ili wezi wakubwa watanue na wake zao?”
Kanji anajibu, “Kwanini tusi veve. Mi sema kweli tu hapana chukia mimi.”
Msomi kuona mambo hayaende kama alivyotarajia anaamua kuingilia kati, “Ni kweli Kanji usemayo. Wakati wanasiasa wakihubiri wachovu kilimo kwanza, hawaji kwenu kwa vile wanajua hamuwezi kulima kama vile mko India.  Kanji wambie siri ya mafanikio yenu ni kufanya biashara.”
Kanji anatikisa kichwa kukubaliana.
Machungi anasema, “Msomi tiambiane ukwei. si kila biashaa inalipa.”
Anamgeukia Kanji na kusema, “Kanji wajua biashara ya unga?”
Kanji anatoa macho na kujibu, “Mimi hapana uza unga. Kila siku sema mimi si halifu.”
“Kaka hutaniwi! Namaanisha unga wa mahindi shehe. Hata ukiuza bwimbwi si rais ameamua kuwanyamazia wauza wasi wasi wako nini Kanji ndugu yangu?” Kanji anajibu akitabasamu, “Kama hiyo naweza uza lakini ile unga nusa hapana uza.”
Msomi anaingilia, “Unadhani atakwambia ukweli? huoni kila muuza unga anapobanwa anakana kana kwamba hauzi unga. Mimi nadhani kama alivyopendekeza mgosi, lazima kijiwe hiki kibadili sera. Badala ya kilimo kwanza tuanzishe Usanii, Uhubiri, mihadarati na madini kwanza. Maana wenzetu wanamiliki vyote. Ufisadi wao, usanii wao, kutorosha madini wao, kuuza miunga wao. Sisi tutakuwa wageni wa nani jamani?”
Kanji hakubaliani na hili. Anapayuka, “Kama somi yote nafikiri kama veve basi somi yote bure.”
Msomi hamkawizi, “Wasomi tena wa kughushi wanaowapa nyie tenda ya kutuibia si hovyo? Acha unafiki. Wasomi mliowakabidhi kaya ni hovyo kuliko mimi ninayewaza tu wakati wao wakitenda. Kwa taarifa yako sina mpango wa kujiingiza kwenye jinai yoyote zaidi ya kuhakikisha uchaguzi ujao tunawapiga chini.”
Kijiwe kikiwa kinaacha kuchangamka si kunguru alimnyea Msomi!
Chanzo : Tanzania Daima, 28, 2013.

No comments: