How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday, 3 August 2013

Mlevi aja na MLO na sera ya Uhujumaa na Kujimegea



Ninajua wengi wanajiuliza MLO ni nini. Msikonde. MLO ni kifupi cha jina la chama changu cha Mlo Laini Organization, kilicholenga kuwakomboa bila kuwakomoa walevi baada ya kugundua kuwa sasa wanakomolewa.

Hebu fikiri jinsi `kanywaji’ kanavyopandishwa bei kila unapofika msimu wa bajeti. Jaribu kufikiri usumbufu wanaopata walevi wanapogundua kuwa kila mwaka `fegi’ zinapandishwa bei huku `ganja’ ikizidi kupigwa vita.

Sasa wafanye nini kama siyo kuchangamkia ukombozi utakaoletwa na chama hiki kitukufu? Nimeanzisha chama hiki kipya, ili kushiriki kwenye uchaguzi ujao, amini usiamini. Lazima 2015 niwemo kwenye debe au sanduku la kula za kura.

Chini ya MLO na sera yake safi ya Uhujumaa na Kujimegea, nitawakomboa walevi. Nilishatangaza kuwa kwenye uchafuzi, sorry…uchakachuaji sorry tena, uchaguzi ujao `natia timu kinomanoma’ na kuhakikisha nazoa kura za kula zote.

Nimeazimia kufanya yafuatayo: Mosi, kuvunja rekodi ya kufanya ziara nje ya nchi, nikiombaomba misaada kwa ajili ya walevi.

Pili, nitahakikisha nyumba yangu na `waramba viatu’ wangu tunajimegea `mshiko’ wa nguvu kama alivyofanya Ben Chinga Tunituni na Anna Tamaa chini ya kampani ya ANIBENII, alipojitwalia mgodi wa `nkaa’ mawe wa Kiwila.

Tatu, nitahakikisha kila mwenye nafasi hasa walevi anafanya uhujumaa bila kuficha `mshiko’ Uswisi wala Uswazi.Nne, nitahakikisha kila kitu kinatafutiwa wawekezaji. Naona yule anasoma na kusonya huku akitikisa kichwa.

Usikonde ndugu yangu. Sitatafuta wawekezaji wa kuchukua jiko lako ingawa nitafanya hivyo kwa nyumba ndogo. Lazima kuwekeza kwenye nyumba ndogo ili ziweze kukua na kuwa nyumba kubwa kama ile ya ‘jumba kuu’ la Kaya.

Tano, chini ya sera ya Uhujumaa na Kujimegea, wawekezaji hawatalipa kodi. Badala yake nitawatoza wasiolewa kodi kuanzia ya simu, juisi, big G, vitumbua, unga na makandokando mengine, kuboresha maisha ya walevi.

Wajua kwanini napanga kutoza simu kodi? Nalenga kukuza uchumi kwa kupunguza kupoteza muda kwenye ku-text na kutumia simu sana, ili waja wasipoteze muda na kuharibu masikio yao.

Sita, nitahakikisha nawamegea `ndata’ mamlaka ili wawakomeshe wapinzani wangu ambao sitaruhusu wafurukute kwa kuunda vikundi vya kujihami na vipigo vyangu.

Saba, chini ya chama cha MLO kila mwenye mamlaka lazima ale na si yeye tu. Lazima arithishe `maulaji’ kwa kitegemezi au vitegemezi vyake, ikitokea `akadedi’ au kustaafu kama alivyofanya Jose Makambaa.

Na wengine wengi waliojaza vitegemezi vyao kwenye ubalozi, wizara na hata bungeni kama walivyofanya akina Chris Mzindi Kaya, Rashidin Kawahawa, Kigoma ya Milima, Joni Nchimvi, Ally Hasahan Mwinyi, Get Mongella, Joni Guni Nita.

Hivyo walevi wenye majina makubwa mkae mkao wa kula na walevi mkae mkao wa kuliwa. Sharti muhimu hapa lazima mhusika awe mlevi wa kweli anayejulikana kwa walevi.

Nane, lengo hasa la sera ya Uhujumaa na Kujimegea ni kuhakikisha kuwa tunalindana na kufadhiliana. Hivyo, hatua ya kwanza itakuwa kuunda mikoa, wilaya na majimbo kwa ajili ya `washikaji’ zangu bila kujali kama ni gharama na hatari kwa `fweza’ ya walevi itokanayo na `kuwakamua’ kodi.

Tisa, ili kuimarisha Uhujumaa na Kujimegea, nitahakikisha vitegemezi vyangu na `bi-nkubwa’ wanagombea `ulaji’ kwenye chama changu hasa kwenye Kamati Kuu ya Siasa ya Taifa ili kuhakikisha ulaji wetu hauendi mbali.

Kumi, chini ya sera ya Uhujumaa na Kujimegea, nitahakikisha mali zote za umma zinaumwa. Nitauza mashirika yote yenye kuleta faida kwa wawekezaji ili niwasamehe kodi, lakini wanipe ten percent yangu ili kuonyesha mafanikio ya sera hii.
Mshiko huo nitakula na walevi watukufutu. Hivyo, jamani anzeni kulewa mfaidike na sera zangu. Shauri yenu! Cheza mbali!

Kumi na moja, nitahakikisha ninatisha kweli kweli hata kwa kutumia wapiga ramli kuwathibitishia walevi, kuwa sera hii ni ukombozi kwao. Hata sina shaka kwani nimesoma sayansi za utabiri kama vile astrology, astrotherapy, biorhythms, cartomancy, chiromancy, the enneagram, fortune-telling, graphology na `madude’ mengine mengi. Hebu niwape mfano. Wakati wapiga ramli wenu uchwara hutumia nyota 12, mie najua kuwa ziko 13 ambapo ya mwisho inaitwa Ophiuchus yenye kushughulika na waliozaliwa Novemba 29 hadi Desemba 17.

Je, hii si sayansi mpya ingawa hapa si muhala mwake? Frankly speaking, pseudosciences and pseudothoughts are the clay out of which my successes are going to be born.

Naongea `kimombo’ si kuwatisha bali kuthibitisha kuwa nimesoma bila kughushi kama wale jamaa zangu wa kukuu. Hayo tuyaache. Tuendelee na mipango kamambe ya kuwakomoa, sorry, kuwakomboa walevi.

Sera zangu zitakuwa wazi chini ya dhana adhimu ya uwazi na ukweli, ambapo kila kitu kitakuwa wazi bila kuhitaji mimi kutoa maelezo hata zitakapozuka shutuma. I am a wise monkey that sees nothing and says nothing.

Kuonyesha nitakavyokuwa mkweli, nitateua `washikaji’ zangu walevi kwenye serikali yangu bila kificho na kuacha wenye kusema waseme bila kuwajibu.

Sera ya kujuana na kufadhiliana nimeiteua kwa makusudi, ili kuonyesha upendo wa hali ya juu kwa walevi. Sitakuwa na haja wala sababu ya kuwafunga mafisadi kwa mfano, ili kuepuka kuonekana sina mapenzi kwa walevi wenzangu.

Hivyo, kama hujipendekezi kwangu na kuniimbia sifa utafute pa kula. Pia ifahamike sitakuwa wa kwanza kufanya hivyo. Nani amesahau jinsi, kwa mfano, mzee Idd Lion alivyofutiwa mashtaka na Afisa Mkuu wa Sharia wa Lisirikali hivi karibuni?

Waulize wahusika. Wale jamaa wakwapuzi wa `njuluku’ za walevi walioficha kule Jersey na Uswisi wako wapi zaidi ya kuendelea `kupeta’ na `kutesa’, wakikwapua zaidi na zaidi? Ukisikia kujuana ndiyo huko. Haya ndiyo matunda na matokeo ya sera za Uhujumaa na Kujimegea ya jamaa zangu wanaokula kwa sasa.

Mnajimegea, mnawamega, mnamegeana hadi kumegana. Kila mtu anammega na kummegea mwenzake na hakuna anayeumia wala kulalamika. Mungu awape nini?

Beware guys. Si kila king’aacho ni dhahabu. Angalie msiliwe katika harakati za kutaka kula na wajinga ndio waliwao. Mnataka tule lupango siyo?

Ngoja niishie. Naona chama twawala kimeishaanza mizengwe kunizuia nikitoe kwenye ulaji. Kipindi hiki ama zangu ama zenu mmezidi ujuha. Shame on you!

Chanzo: Nipashe Jumamosi 3, 2013.

No comments: