How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday, 17 August 2013

Mlevi apanga kukutana na Mkuu Kiquette

Juzi mlevi alipata hard time, baada ya walevi wenzake kumzodoa kuwa yeye ni kibaraka. Unajua ilikuwaje?
Tukiwa tunapata whisky vodka na Devil Ale 666 na `mipombe mingine’ ya bei mbaya na majina magumu magumu wanywayo wenye nazo. Nasi zilikuwa zimetutembelea na kupata `zali la mentali’.
Basi ulifumka mjadala wa uadilifu. Kuna mlevi mmoja aliniudhi nusu nijinyotoe roho. Nilikuwa nikimsifia Rais Black Obamiza kwa uadilifu wake bila kujua kuwa kumbe naye si muadilifu.
Mlevi yule si alinitolea `kavu kavu’ kuwa Obamiza angekuwa muadilifu, asingefungua mradi wa kijambazi wa Richmonduli wa Ubungo.
Kuanzia hapa `machale’ yalinicheza nikaacha mchezo wa kuwasifia wakuu. Baada ya kumalizana na Obamiza, si jamaa akamgeukia mkuu wetu mpendwa kipenzi na chaguo la Mungu na kipenzi cha watu Jake Kiquette!
Ulidhani nitasema Kiquette. Umenoa! Jamaa alihoji eti ni kwanini `amekula jiwe’ kuhusiana na kutaja mali zake `nkewe’ na vitegemezi vyake, wanaosemekana kuwa mabilionea wa kutupwa.
Ajabu his bloody spin doctors are giving everything he does a positive spin! Go figure guys. We know how wicked and dirty you always are. Samahani ‘mizuka ya kikameruni’ imepanda hadi nikasahau kuwa humu si mwake. Nisameheni wajameni.
Dai hili liliniumiza, nikawaahidi walevi kuwa nitafanya kila liwezekanalo nikutane na mkuu kumuomba awafunge wanaomtaka ataje mali zake, ili walevi waache kumdhalilisha kwa kusema eti hana uadilifu.
Niliposema nitakwenda kukutana na mkuu, jamaa walinizomea wakisema eti nakwenda kukutana naye kisanii. Niliwajibu kosa ni nini kama atakutana na msanii sawa, na anavyokutana na wasanii wenzake?
Nilishasema kuwa si vizuri kwa mkuu kutaja mali zake maana wezi wanaweza kumvamia na kumuibia.
Pia nina mpango wa kumshauri Mkuu awapandishe washikaji wajanja hasa walioghushi shahada zao kwa vile waliokoa muda ambao wangepoteza madarasani na kuchelewa kuula na kuchuma.
Mawaziri wanaopaswa kupandishwa vyeo na kuruhusiwa wafundishe mbinu zao kupata shahada bila kupoteza muda kwenye vyuo vikuu. Hawa ni Makorongo Muhanga, Marry Nyagu, Bill Lukuwi, Emanweri Nchimbizi na balozi Deodoruz Kamla.
Pia nitamuomba mkuu awapandishe vyeo washikaji zake wanaoonewa wivu kwa kufanikisha masuala mbali mbali kama vile Juma4 Kawa-dog, aliyefanikisha na kuboresha elimu kwa kuwapa ushindi wale waliokuwa wametangazwa kuwa wameshindwa kwenye mtihani wa kidato cha nne.
Kawa-dog ni wa kupigiwa mfano hasa kwa kuwa na roho ngumu. Huwa nikikumbuka alivyokataa kujiuzulu pale alipofanikisha elimu, natamani nimpe `kanywaji’.
Mwingine ni Anne Tiba- Ijukayo ambaye `aliwapiga mkwara’ wenye mjengo dada wa ulioua, lakini baadaye akachomoa baada ya kugundua kuwa kama `mghorofa’ ule ungebomolewa, ungeliingizia taifa hasara kubwa kiuchumi.
Pia mawaziri kama Dk Mgimua, wanapaswa kupewa nishani ya ubunifu kama vile kubuni kuwakamua watumiaji wachovu wa simu `madafu elfu’ kwa mwezi. Lazima atunishe mfuko wa taifa na kutoa misamaha ya kodi kwa wawekezaji ili kuwavutie wazidi kuwekeza na kuchukua.
Kwanza, simu nyingi zinatumika kufanya `misheni’ ya kuiibia kaya, ukiachia mbali kwenye mambo ya uroda na upuuzi mwingine kama huo. Siku nyingine nitashauri Dk Mgimua awatoze watu kodi ya kupiga kelele zitokanazo na matumizi ya simu.
Hakuna sehemu ambapo Mgimua `alinikuna’ kama kuyaacha makampuni ya simu yawasulubu wachovu kama hayana akili nzuri. Nimefurahi kuona yanavyowapa huduma mbovu, sorry, bora ambazo zinawafanya wapate taabu ya kupiga kelele mara kwa mara, kutokana na kuambiwa kwa kubana pua “samahani namba unayopiga ni ya bosi.”
Mingine ikisema, “samahani utumie dola si madafu tumeyachoka,” na upuuzi mwingine.
Pia, nitamshauri mkuu ahakikishe anaendelea kuwakamata `mateja’ na kuacha wanaoingiza bwibwi kayani kwa vile wanasaidia kutengeneza mabilionea ambao huliletea sifa taifa, kama ilivyotokea hivi karibuni ambapo bilionea wa Kagodam alitajwa kuwa alikuwa miongoni mwa waliokutana na Rais Obamiza.
Hawa ni watu muhimu kwa uchumi wa kaya ilmradi wasikamatwe kama ilvyotokea walipopitisha bwibwi kwa kumalizana na wakaguzi wa uwanja wa ndege wakanaswa Sauzi.
Hii ilinikumbusha vita ya bangi almaarufu Opium war kati ya Uchina na Uingereza 1839-1842 na 1856-1860. Hii kaya ya wajanja bwana. Hamkusikia jinsi jamaa wa zimamoto wanavyotumia `michuma’ yao kusafirisha kago inayoibiwa toka kwenye mizigo ya abiria pale uwanjani?
Nani amekamatwa? Akamatwe wa nini wakati anakuza uchumi wa kaya? Akamatwe wa nini wakati anawapa burdani vijana wasio na ajira? Akamatiwe nini iwapo waathirika si vitegemezi vya wakubwa?
Akamatwe kwanini iwapo anaweza kutoa michango katika chaguzi mbali mbali kwa kufadhili vyama tena vyenye nguvu? Akamatwe nani wakati ujanja ni kupata na mtaji wa matajiri ni mamlaka yao?
Watu wanataka kumpotosha mkuu eti akamate wauza unga, majambazi hata mafisadi wakati ahadi zake wakati wa uchaguzi ilikuwa ni maisha bora kwa wote.
Hawa wanaomtaka mkuu awakamate hao hapo juu hawaoni walivyo na maisha bora, tena wote wakitanua na `migari’ ya bei mbaya na kuishi kwenye mahekalu?
Waziri mwingine ninatakayependekeza apandishwe cheo ni Adamu Milima ya Kigoma.
Hiyo ni kutokana na ushupavu wake wa kutembea na `mibunduki’ hadi wezi wakamuogopa. Unakumbuka sekeseke kule hotelini Moro? Huyu jamaa alipaswa afanye kazi FBI siyo jimboni.
Pia nitakapokutana na mkuu nitamuomba awape nishani watendaji waliofanya kazi iliyotukuka. Hawa si wengine, bali waziri mkubwa Mzee Pinder ambaye alinikuna alipowaambia `ndata’ watukunyuge hadi tutie adabu.
Na kweli baada ya amri ya Mzee Pinder, nasikia `ndata’ weshanyonga mchovu. Pia PIG Saydu Mhwema lazima apewa nishani kwa kusimamia `ndata’ hasa wanapotembeza kichapo na hata kunyotoa kama walivyofanya huko Nyonyolo ambapo Daud Mwangosi.
Alimwangosiwa na aliyeongoza umwangosi huu bwana Kamu- Handa, alipandishwa cheo. Huyu anapaswa kupewa nishani kwa kuleta amani na utulivu kiasi cha kumfanya mkuu atulie bila kuwa na haja ya kupoteza muda kufukuza watu wala kutoa maelezo kwa wachovu.
Mwisho kabisa, nitamshauri Mkuu ampe nishani bi mkubwa Salmae kwa kuendesha NGO yake vizuri, kiasi cha kupewa nishani huko majuu.
Amefanikisha kuonyesha kuwa lazima Lady Numbero Uno awe mjasiriamali anayejua kuzichanga na kutengeza `fweza’. Unadhani ukishaondoka maulajini utapata wapi mtaji wa kuanzishia biashara?
Hamjamuona Anna Tamaa Makapu anavyotesa baada ya kuzichanga kupitia NGO yake ya Fursa kwa Wote Walaji? Lazima Lady Numbero Uno awe mjasiriamali.
Je umeipata ya bwimbwi kuuteka uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu?
Nani anajali iwapo wananufaika na jinai hii? Napanga kuanzisha Madudu Prize ambayo watapewa wafanya madudu. So jiandaeni na kukaa mkao wa kula.
Nitaiongelea wiki ijayo. 

Chanzo: Nipashe Jumamosi Agosti 17, 2013.

No comments: