How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 20 August 2013

Patakatifu pa patakatifu si kijiwe cha mateja


8E9U3986 62170
BAADA ya kijiwe kunyaka taarifa kuwa msanii mkuu alifanya kikao na mateja kukuu kama njia ya kuionesha jamii jinsi ya kupambana na bwimbwi, kilikaa kama kamati kulaani jinai hii.
Maswali yalikuwa mengi kiasi cha kuniacha na kizunguzungu cha kizungumkuti.
Mara Kapende anaingia akiwa anasonya. Anasalimia kinyonge: “Waheshimiwa salama?” Tunamjibu haraka haraka.
Mipawa anamchokoza: “Kapende mbona huna raha leo, kunani?” Kapende anajibu: “Kwani hukusikia mateja yalivyonajisi patakatifu pa patakatifu au husomi magazeti?”
“Hebu urudiage nikuelewe hadi ni-‘comprehend’ na ‘ku-understand’ na ‘ku-underscore’. Unasema eti mateja yamekwendaga ikuru? Beng’we, hii hatari bajameni. Nani huyu kawaruhusu hawa mateja kwenda kulaga miunga patakatifu pa patakatifu?”
Kabla ya kuendelea, mgosi Machungi anachomekea: “Kwani mateja kwenda patakatifu pa patakatifu mnaona nongwa. Hukumbuki mgosi Mchonga alisema kuwa palishageuka pango la wanyang’anyi? Sioni tatizo kwa mateja au wauza unga wakienda kule kuyamaiza.”
Mpemba naye hajivungi, “Yakhe hii sasa kufuru. Yaani watu waacha wenzao wabwie unga halafu wakaribishana kupongezana kwa jinai? Hii si sawa wallahi.”
Msomi aliyekuwa akisikiliza kwa makini na kukuna kichwa anaamua kutia buti. Anasema: “Kama alivyosema mgosi sishangai kuona mateja yakienda huko kupata chai na mkuu. Kwanini yasiende kule? Kimsingi, huku ni kuonesha kushindwa kwa wazi kupambana na mihadarati. Kunywa chai na mateja hakuwasaidii bali kukamata wauza unga. Huku ni kuwatumia tu kisiasa. Huwezi kukutana na mateja halafu ukasema unapambana na unga. Badala ya sanaa, kamata wanaowauzia haya madude. Vinginevyo ni usanii wa kawaida na kutaka sifa kama sikosei.”
Kanji inaonekana kaguswa pabaya: “Kwanini vatu nakuwa baya hiwi. Tukufu iko onyesha penzi kwa vatu yake yote bila baguzi. Sifu yeye basi.”
Mzee Kidevu hamkawizi Kanji. Anampaka: “Kanji nawe unajua ubaguzi enhee? Unadhani hatujui mnavyowabagua waswazi majumbani mwenu mkiwatumikisha kama punda? Huwezi kuona ubaya wakati wanufaika wa unga mko wengi baba.”
Kanji naye hakubali: “Mzee Devu sema mimi uza unga? Omba samaha mimi kabla ya shitaki veve.”
“Kitoe huko! Umshitaki nani wakati wauza unga hawana alama? Kwa akili yako ya kiponjolo unadhani tunaweza kupambana na unga kwa kunywa chai na mateja au kukamata mizungu ya unga?”
Mbwa Mwitu aliyekuwa akitafuta upenyo wa kuchangia kapata nafasi. Anasema: “Nguluvi wane! Hawa jamaa nao kweli mateja. Yaani badala ya kuwaendea wauza mnakamata wanunuzi siyo? Huku nako kuishiwa kulhali.”
Kabla ya kuendelea Msomi Mkatatamaa anaamua kurejea kwa ‘force’. Anakwanyua mic: “Mimi nitatoa suluhisho la mihadarati. Kwanza, nasema turejeshe maadili ya utumishi badala ya kuendekeza madili.  Hapa lazima tuwabane watumishi wanaolala maskini na kuamka matajiri kwa kuruhusu unga upite. Ningeshauri hawa wabanwe waeleze walivyopata utajiri wa ghafla bin vuu.”
Anakwanyua kashata na kuendelea: “Kama mkuu anamaanisha kupambana na unga, basi awabane matajiri wote wenye kutia shaka. Afanye ukaguzi wa kushtukiza kwenye majumba na akaunti zao, mfano, wafanyakazi wa viwanja vya ndege, Uhamiaji, polisi na mamlaka nyingine zinazoshughulikia ukaguzi na jinai. Ndio wanufaika wakubwa wa jinai hii.”
Kanji hakubaliani na Msomi. Anachomekea haraka haraka: “Veve Somi danganya sisi. Hapana jua jinsi sirikali fanya kazi yake. Hapana ona juzi naweka tego na uza unga napitisha unga airport na inakamatwa Hong Kong?”
Wote kwa pamoja tunaangusha kicheko cha kebehi.
Msomi anaendelea: “Kanji usitufanye majuha, kama fisadi mkuu anakingiwaje kifua. Unamaanisha unga uliokamatwa Sauzi na Hong Kong ulikuwa mtego wa lisirikali? Go tell it birds my friend. Sema jamaa ameona awatumie waathirika kujipatia sifa tu. Mbona wauza unga wanafahamika?”
Kanji anarejea: “Veve Somi ongopa sana. Taja uza unga unajua veve.”
“Well done my friend! Nitataja. Kwanza, mkuu mwenyewe alisema anawajua, sema anawalinda tu kwa sababu zake. Yeye hakutaja. Mie nataja. Kama wote wale tunaowaona mitaani wakijidai na migari ya bei mbaya huku wakiishi kwenye mahekalu kama superstars wa Hollywood. Kwani hawajulikani?”
Anajifuta kijasho na kuendelea: “Wengi wanajulikana kuwa watoto wa kapuku walioibuka na kuwa mabilionea ghafla bin vuu.
Au hili nalo linahitaji FBI kuja kuwabaini? Ukitaka kuondokana na jinai ya unga, simpo. Amuru kila mmoja aeleze alivyopata ukwasi wake.”
Kabla ya kuendelea Kapende anachomekea, “Nani amuamuru nani kutaja mali zake iwapo mwenyewe anagwaya kufanya hivyo?
“Umesema vizuri my friend. Hiki ni kiini macho bin changa la macho. Huwezi kuwashughulikia mbuzi kwa kuliwa na fisi wakati ukilala kitanda kimoja na fisi wawalao bwana. Huu ni ujuha, msitugeuze majuha wenzenu.”
Mara Kanji anatoa kisingizio cha kuishia. Anasema: “Mimi iko na appointment. Hivyo, sasa kwenda mimi kuepuka hii ongo ya chana.”
Anaamka na kuondoka huku Mipawa akimsindikiza na matusi akisema: “Nendaga mwana kwendanga na ushuzi wako.”
Kicheko.
Msomi Mkatatamaa anaendelea: “ Si waseme wazi kuwa wanalea wauza unga kwa vile wana masilahi nao. Huwezi kuua maadili ukategemea madili nayo yafe. They know what they are doing, thanks to their myopia and blindness.”
Anakunywa tangawizi na kuendelea: “Hata kichaa akipewa nafasi anaweza kupambana na unga na kushinda. Badala ya kuamuru watuhumiwa wachunguzwe na kukamatwa tunajifanya kuwa na huruma na waathirika? Upuuzi mtupu! Mie nasema wazi. Siogopi kitu. Mkuu awataje wale aliosema ana orodha yao vinginevyo ni sanaa kama kawa.”
Mpemba anachomekea: “Yakhe naona angetangaza wazi kuwa sasa unga halali na wanaoupinga wanafanya jambo haramu.”
Mgosi Machungi anaamua kurudi tena. “Sisi timeshazoea hizi sanaa. Kesho titasikia eti mkuu anakutana na wauza unga na kuwasihi waache mara moja. Ila tijue tinaangamiza kaya.”
Msomi anajibu haraka. “Mgosi leo umetoa pwenti za maana sana. Heri wahalalishe kama alivyosema ami hapa mchezo uishie badala ya kugeuza watu mabunga. Hata hivyo, ana hasara gani wakati waathirika si vitegemezi vyake?
Pia, nani anajua? Huenda wapo watu wake ambao akiwakamata wanaweza kumuaibisha. Heri ajinyamazie kama alivyonyamazia kutaja mali zake.”
Kijiwe kikiwa ndiyo kinachangamka si alipita teja mmoja. Mbwa Mwitu alimwambia: “We teja nenda kanajisi patakatifu pa patakatifu na wakutumie kupata ujiko na kupiga picha nao.
Nikiwa najiandaa kutoa pwenti mama wa zote si lilipita gari la zungu la unga. Tuliamua na kuanza kulirushia kashata na kulimwagia tangawizi hadi ndata wakaja kutukamata.
Kila mmoja alijikata kivyake na kuwaacha ndata na teja lao ili liwapeleke kwa wauza unga wawatoe kitu kidogo na kitu kikubwa. Imetoka hiyo! Message sent au siyo?
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 21. 2013.

4 comments:

Anonymous said...

Duh, hii kali. Kwani utaratibu huu wa kuonana na "mateja" wastaafu ni endelevu au? Wapi wana-sain...? Ngoja nami nifanye jitihada za kubwia bwia miunga ili nistaafu kabla ya "mkutano" mwingine ujao, pengine nitapata bahati ya kuingia Ikulu. Maana hii inaonesha ndiyo njia ya mchongo kuvinjari kwenye mjengo wetu pale.

Hivi mkuu Mhango, hujawahi kusikia kuwa "mateja" wengi huwa wanapata "stimu" mitaa ya Magogoni kule na fukwe zake? Yawezekana mkutano huu ni wa "ujirani mwema" tu, kuwa jamaa kawaalika majirani ili wafahamiane na kubadilishana mawili matatu. Pengine kuzungumzia kuunda ulinzi/uzinzi/uwizi shirikishi n.k n.k.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

ANON hapo juu umeniacha hoi! Unasema eti ujirani mwema siyo? Huogopi wanaweza kumsajili mkuu naye akawa taje kuu kama alivyosajiliwa na mafisadi na kuwa fisadi mkuu? Hii ya kuanza kubwia sikushauri. Maana si mateja yote yanakaribishwa Ikulu. Ukitaka ukaribishwe omba Mungu mama Salma apanue makampuni yake ya kusaidia mateja au uongee na Pili Misana akusajili kwenye kampuni yake ya ulaji wa kutumia mateja. Upo hapo mkuu?

Anonymous said...

Fr. Mhango na Anon,hapa sina mbavu. Mimi sijawahi kusikia raisi mwenye uji badala akili kichwani kwake. Nafikiri yuko peke yake tu ulimwengu mzima. Kwa upuuzi anaofanya basi na hii ishu ya maungaunga aiungeunge kwa WAMA ili iwe WAMAUNGA(Wanawake wa wakubwa Maulaji na Unga) ninauhakika itawafaa,kwani hata akina Ridhi wa Wani nao watazidi kupanua biashara zao zaidi ili kuendeleza familia yao.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Huo ndiyo ukweli na huyo ndiye rais wenu. La muhimu ni kwamba msirudie kosa kwa kuchagua bunga tena.