The Chant of Savant

Saturday 20 November 2021

Barua kwa Serikali na Wazazi Tuwasaidie Vijana Wetu

Wapendwa, nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Tanzania. Kwanza kabla ya kuandika au kueleza nitakayoandika hapa, lazima niseme wazi kuwa mimi ni mzazi ambaye alisoma bure enzi za Ujamaa. Hata andiko langu la tasnifu yangu ya Shahada ya Uzamivu ni juu ya namna Ujamaa ulivyoondoa ukabila Tanzania na kujenga taifa lenye amani na mshikamano mbali na kutumia raslimali za taifa kwa usawa na kwa faida ya wananchi wote. Hivyo, niandikayo siyo tu yanatako moyoni tu bali yanatokana na uzoefu na hata usomi. Naandika kama mzazi mwenzenu japo watoto wangu wanasoma nje na kama mtanzania mwenzenu ambaye nilisoma bure. Najisuta na kutaka kila mmoja wa kizazi chetu ajisute abebe mzigo badala ya kuusukumiza kwa vijana wetu wakati ni mzigo wetu kwanza.
Hakuna ubishi kuwa mikopo inawaumiza vijana wetu wanaomaliza masomo yao sasa hivi. Hii ni kutokana ugumu wa kutopatikana ajira. Juzi nilimsikia kiongozi mmoja akiwashauri vijana wanaomaliza kwa sasa wasitafute ajira bali kazi asijue kazi ni ajira na ajira ni kazi.  Tumesoma bure na sasa–––baada ya kulazimishwa na mifumo ya kibepari na kinyonyaji ya duni–––kuwalazimisha watoto wetu wasome kwa mikopo isiyo na uhakika. Ama kweli wahenga walisema kuwa nyani haoni nonihino lake au tuseme mwenye shibe hamjui mwenye njaa. Sina maana ya kulaumu jamii bali kuisuta lau tufanye kitu kuwasaidia vijana wetu wanaosoma kwa sasa lau kwa kupunguza makali yao. Japo alichomaanisha waziri huu ni kuwa vijana wajiajiri, alijisahau na kusahau kuwa–––kama serikali yenye maguvu na uwezo wa kukusanya kodi, kukopa na kupewa misaada kwa niaba ya wananchi inashindwa kutengeneza ajira au mazingara ya kujiajiri–––wao watajiajirije? Nadhani kinachowashinda baadhi ya wenzetu ni kushindwa kutofautisha nadharia na vitendo. Ajabu, hawa ndiyo wanawalaumu vijana wetu kwa kushindwa kujiajiri wakati wao, pamoja na kusoma bure, hawakujiajiri. Sina ugomvi na kujiajiri. 
Vijana wetu wanajiajiri kweli kweli. Wengi wamewekeza kwenye mistari ili wawe wasanii na kuukata bila kujua kuwa usanii ni kazi inayohitajika kwa jamii baada ya jamii kufanya kazi na kuchoka ila si mtaji. Kwa ajira za kisanii kama hizi, tutatoa fursa kwa wageni waliowekeza kwenye elimu ya kweli kuja kufaidi fursa ambazo vijana wetu hawawezi kuzifaidi kutokana na kutowezeshwa au kuajiri kwenye mambo kama sanaa. Nchi ya DRC inasifika kwa muziki wake. Je umeisaidia nini wakati madini lukuki iliyojaliwa yanafaidiwa na wageni wakati wananchi wako wakitumia muda mwingi majukwaani. Msinielewe vibaya kuwa nachukia sanaa au muziki. Lazima tuangalie nini kifanyike kwanza kama jamii ili kujikomboa na kuwakomboa watu wake.
Wakati tukiwataka vijana wetu wachukue mikopo na kusoma na baada ya hapo wajiajiri, tujiulize. Je wote waliomaliza masomo yao ambao walipata elimu ya awali na serikali kwa kuchukua mikopo wamerejesha fedha ya mikopo hiyo? Nadhani wengi hawajalipa wakiwamo hata hawa wakubwa wanaowalaumu vijana kwa kutojiajiri. Je kama jamii tuna mpango gani kuwapunguzia adha? Je tuna haki ya kuwalaumu bila kujilaumu? 
Huwa sipendi kulaumu bila kutoa suluhisho. Je nini kifanyike kuwasaidia vijana wetu kupata ajira au kazi? Nina mapendekezo yafuatayo:
Mosi, tukusanye kodiu na mapato yatakiwayo itakiwavyo ili yawe sufufu, na kuimarisha uchumi huku tukipambana na ufisadi vilivyo tukifanya hivyo, tutaweza kuwasomesha vijana wetu bila kulazimika kuwakopesha mikopo yenye riba kubwa. Ilikuwaje kipindi kile cha awamu ya kwanza, tena tukiwa taifa changa, tuliweza kuwasomesha vijana wetu bila kuwatoza au kuwakopesha?  Kuwakopesha ni jambo zuri ili wasibweteke. Hata hivyo, kuwapunguzia gharama za masomo au kuwalipia baadhi ya karo siyo vibaya.
Pili, badala ya kuwalaumu, tukubali kuwa kama taifa tumewadhulumu vijana wetu. Hivyo, tuna jukumu la kuwatafutia suluhu ya tatizo lao badala ya kuliona kama ni lao peke yao wakati tumechangia pakubwa. Ukifanya uchunguzi hata wa kusoma kashfa zinazoibuliwa na magazeti kwa mwaka mzima, utagundua kuwa bara la Afrika linapoteza mabilioni ya fedha ambayo yangetosha kutoa huduma za kijamii kama afya na elimu bure na kufanya mambo mengine. Pia hata ukiangalia matumizi yetu kwenye kununua zana za kukandamiza watu wetu, unagundua namna tunavyochezea fursa. Inakuwaje, kwa mfano, wagonjwa wakose dawa au vitanda wakati polisi wetu hawakosi maji ya washawasha au marungu ya kuzuia vurugu? Inakuwaje watoto wetu wakose fedha ya kusomea lakini wakubwa wetu wapate fedha za kutanulia? Haya ni baadhi ya maswali tunayopaswa kujiuliza badala ya kuwalaumu au kuwasukumia mzigo vijana wetu. 
Tatu, tubane matumizi yasiyo ya lazima hasa kwa wakubwa wetu. Nimekuwa nikipigia kelele kuondoa utaratibu wa kuwawekea madereva, walinzi, wafagiaji, kuwapa nyumba za kuishi bure hata mafuta ya magari yao wakubwa zetu ili wajiendeshe wenyewe sawa na wengine. Nimekuwa nikipigia kelele kuanza utaratibu wa kuwataka watu wetu wa kujaza taarifa na ripoti za mapato na matumizi yao ili kupunguza ufisadi na wizi. Hili likifanyika, wale tutakaokuta wana fedha isiyo na maelezo, tunaweza kuitumia hata kusomeshea vijana wetu au kufanya mambo mengine ya muhimu kama taifa.
Tumalizie kwa kushauri, kama jamii na taifa, tuliangalie tatizo la vijana wetu kukosa ajira kama letu pamoja kama taifa na si lao binafsi. Kuwalaumu au kuwashauri  mambo yasiyowezekana hakutusaidii wala kuwasaidia.  Kama mnaona elimu tunayowapa haifai basi irekebisheni ili tutoe elimu inayowawezesha kujiajiri.
Chanzo: Raia Mwema kesho J'pili.

No comments: