The Chant of Savant

Wednesday 10 November 2021

Waraka kwa Rais Kuhusu Mauaji ya Walemavu wa Ngozi

Mheshimiwa Rais,
Nakusalimia kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kukupongeza kwa kazi kuendelea japo kuna mengi yanaanza kwenda ndivyo sivyo. Leo sina habari njema kwako. Nina majonzi na uchungu kuhusiana na uhayawani na unyama unaoanza kurejea taratibu nchini. Hakuna ubishi. Tukio la kufukuliwa kwa mwili wa mtu mwenye ulemavu wa ngozi ni aibu japo ni kiashiria kuwa tunaanza kurudia kwenye maisha ya zamani ya jinai kabla ya serikali ya awamu ya tano kuyakomesha. Vyombo vya habari viliripoti kuwa kufukuliwa kwa mwili wa Heri Kijangwa hivi karibuni katika kijiji cha Tanda wilayani Lushoto.  Je hawa wanyama wenye sura za binadamu, Mheshimiwa Rais, kweli wanastahili kutendewa na kutenzwa kama binadamu iwapo hawawajali binadamu wenzao? Licha ya kuwa ukatili na unyama visivyomithalika, ni aibu kwa taifa na jamii ambayo bado ina baadhi ya watu wenye mawazo ya kinyama na imani za ajabu ajabu za kulea uvivu na kutegemea kupata mafanikio na utajiri kupitia miujiza na ushirikana. Kimsingi, ujinga, umaskini, imani na dini za kijinga na uvivu ndivyo vichocheo vikubwa vya imani potofu na unyama huu. Tunapaswa kuchunguza asasi hizi na kuzifutilia mbali liwalo na liwe.
            Mheshimiwa Rais, kama taifa linalojitambua na lenye akili na utu–––tena likiongozwa nawe–––tunapaswa kutunga si sheria kali tu bali hata kujenga ustaarabu wa kutovumilia ukatili na upumbavu huu. Hapa tunapaswa kuwa wakatili dhidi ya ukatili hata kuliko hawa hayawani wanaotenda ukatili unaolifedhehesha taifa letu. Ni juzi, nikiwa natetea andiko langu juu ya mafanikio ya Ujamaa na namna ulivyoondoa ukabila nchini, msimamizi wangu aliuliza swali kuhusiana na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi. Nilimjibu kuwa watanzania siyo malaika wala mashetani. Ni jamii ya binadamu yenye kila aina ya watu wema na wabaya.
Mheshimiwa Rais, hawa hayawani na majnuni wanaoamini kuwa viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi vina ‘ngekewa’ washughulikiwe vilivyo tena bila huruma wala subira. Sijui kama huwa wanajiuliza: kama wao wangekuwa ndo wahanga wangependa watendeweje? Je kama taifa tuna haja wala sababu ya kuwatenza kibinadamu wakati matendo yao ni mabaya kuliko hata wanyama?
Mheshimiwa Rais, najua. Ulikuwa msaidizi mkuu wa mkuu wa serikali ya awamu ya tano chini ya kiongozi mahiri Hayati Dkt John Pombe Magufuli ambaye serikali yake ilikomesha unyama huu tena mara moja. Hivyo, unajua mikakati na siri zote mlizotumia kufanikiwa kukomesha upumbavu na ukatili huu. Je nini kinakosekana ili tukusaidie kuangamiza unyama huu unaotuletea aibu kama taifa na kutuoonyesha kama watu wajinga, wapumbavu na wavivu wanaotegemea upuuzi kupata mafanikio kiuchumi?
Mheshimiwa Rais, toa elimu ya uraia kila kona nchini huku ukipambana na waganga wa kienyeji na baadhi ya fisi walio kwenye ngozi ya kondoo wanaotumia dini kuwaaminisha baadhi ya watu wetu wapumbavu na wajinga kuwa wanaweza kutajirika bila kuhangaika na kutoa jasho.
Tunayashukuru mashirika ya kupigania haki za binadamu LHRC na THRDC kwa kulaani unyama huu kwa namna inayotakiwa na haraka. Pia tunawapongeza TAS, chama cha wenye ulemavu wa ngozi, ambao walikaririwa wakisema “tunaona kabisa kunahitajika jitihada za makusudi, na kuwepo na mkakati madhubuti wa kuimarisha hali ya ulinzi na usalama na kushughulikia matatizo haya. Pale ambapo serikali inashindwa kushughulikia na kufanya uchunguzi inawezekana ikawa ndio sababu ya matukio haya kuendelea kutokea.”
Pamoja na TAS kuwa wahanga, wameonyesha kujua chanzo cha tatizo. Je inakuwaje serikali iliyoapa kuwalinda wananchi, utu wao na mali zao kushindwa kufanya uchunguzi tena haraka iwekezekanavyo kana kwamba wahanga hawastahiki haki hii? Je ni serikali peke yake yenye kustahiki lawama au hata wananchi wanaoshiriki au kuficha vitendo hivi ukiachia mbali wanaovichochea hasa waganga wa jadi? Je kama wananchi binafsi tumefanya nini kupambana na kadhia hii?
Mheshimiwa Rais, hili linaweza kukukera na kukuchusha. Hata hivyo, sina jinsi. Itabidi niwe narirudia lau kama hukusoma ujumbe wa kwanza, utasoma huu au utakaofuata kulingana na ambavyo tatizo litakuwa limeshughulikiwa. Nimekuwa nabii wa kutaka Tanzania ijenge utamaduni wa kuhoji utajiri wa watu wake ili kuweza kujua wanavyoupata mbali na kukatisha tamaa wale wanaoutafuta kwa njia za mkato kama vile mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi na vikongwe, rushwa, ufisadi, wizi, ujambazi, utapeli na mengine kama haya. Hii ikifanyika, wahusika wataogopa kutumia njia tajwa kwa vile wanajua watahojiwa na wakishindwa kutoa maelezo watanyang’anywa mali husika hata kushitakiwa kwa kupatikana na mali ambazo hazijulikana zimepatikana vipi wala kuwa na maelezo ya kina.
Mheshimiwa Rais, tujengee utaratibu wa kila mtanzania kuanzia mdogo hadi wa juu ataogopa kujiingiza kwenye unyama na uchafu wa kutaka kutajirika bila kutumia akili vizuri wala kuvuja jasho.
Mheshimiwa Rais, kwa taadhima, naomba niishie hapa kwa kukuomba. Chonde chonde. Watu wenye ulemavu wa ngozi ni watanzania wenye haki ya kulindwa na kuishi sawa na watanzania wengine. Hivyo, kama wasemavyo waingereza, the bucks stops with you kama kiongozi mkuu wan chi. Chonde chonde. Rejea mbinu mlizotumia na Magufuli kukomesha jinai hii. Wape onyo polisi wakishindwa teua wengine wenye uwezo wa kukomesha kadhia hii pamoja na nyingine. Muhimu, anzisha ustaarabu na utaratibu wa kutaka watanzania waonyeshe wanavyopata mali zao.
Chanzo: Raia Mwema Leo.

No comments: