The Chant of Savant

Monday 15 November 2021

Tuepuke Kujigeuza au Kugeuzwa Jamii ya Mitumba

Kuna nyani aina ya Kabuche ambao hupatikana nchini Panama. Nyani hawa wanasifika kwa umahiri na upenzi wao wa familia. Mara nyingi utawaona mama au baba wakiwaongoza watoto kwenye kundi! Kinachonivutia ni ile hali ya mama na baba ambao ni viongozi kula wa mwisho! Ni viumbe wachache wana tabia hii ya kujali na upendo kwa wanyonge. Je hawa hawajawazidi binadamu wanaojihudumia kwanza wakati umma unaangamia kwa njaa? Je hawa siyo bora kuliko wanadamu–––hasa viongozi wanaokula kwanza–––wanaokula kabla ya wanyonge waliowaamini mamlaka? Je hawa si bora kuliko wenzetu wanaokula kwa mikono na miguu tena bila kunawa? Leo nitamsaidia Mheshimiwa Rais kuwaasa viongozi mafisi, mafisadi, wachoyo na walafi. Kama unajilimbikizia mali unapokea rushwa na kuwa na sera za kubabaisha jua unakula kwa miguu na mikono. Unawageuza wenzio vijiko wewe ukijigeuza domo japo chafu. Huu siyo utu ni umtumba; na ni ukosefu wa maarifa sahihi. Unachofanya hakina tofauti na kuku mpumbavu alaye mayai yake au simba auawe vitoto vyake. Huna tofauti na hayawani kwanini wewe utende kama wao wakati wajiita binadamu wakati ukweli wewe ni hayawani kuliko hayawani? Je wewe siyo shetani kuliko shetani si kahaba kuliko kahaba?
           Uhayawani hauishii hapa. Mamlaka zinayowalisha wananchi wake vyakula vibovu huku ikivuruga huduma za jamii na uchumi nayo ni mtumba. Serikali zinazoagiza vyakula wakati zina watu wenye nguvu na udongo wa rutuba,mito maziwa na hali nzuri ya hewa nazo ni mitumba. Maana uwezo wake wa kufikiri na kutumia maarifa umevia na kuisha wakati wake kiasi cha kugeuka mitumba ya kifikra. Zipo tena nyingi. Zipo tena zinakusanya kodi hata kuiiba. Huu ndiyo umtumba. Viongozi wanaoua mashule na mahospitali wakawatuma watoto wao kusoma na wao kutibiwa nje wana tofauti gani na vipofu wa roho?
        Serikali inayofumbia macho rushwa ufisadi na mikorogo mingine ya kimwili na kimaadili nayo ni mtumba. Serikali isiyowajibika kwa umma wala kutimiza wajibu wake nayo kadhalika ni mtumba. Huwezi kutowajibika kwa umma unaopaswa kuwajibika kwake usiwe mtumba. Wewe ni sawa na chumvi iliyokwisha muda wake au mabaki ya chakula jalalani. Ni sawa kiporo cha juzi kilichogaga na kutoa harufu mbaya huku kikizungukwa na mainzi. Mainzi nayo yapo ya aina nyingi. Yapo yaliyoumbwa na Mungu na yale yaliyoumbwa na shetani. Mafisadi, mafisi ya kiuchumi, majambazi, majizi, wala rushwa na wengine kama hao ni mainzi tena mafu hata kama tunayatukuza kwa vile yana fedha.
           Je katiba  zisizoleta mabadiliko kwa umma badala yake zikauuma umma nazo ni mitumba? Ni mkataba gani ambamo wana mkataba wanalazimishwa kuuingia zaidi ya kifo? Mikataba hii huingiwa na mainzi mafu ambayo nayo ni mitumba. Je dunia haikujaa mikataba kama hii iitwayo katiba? Bahati mbaya, mingine imejaa viraka kama gunia. Mikataba kama hii ni ya hovyo kuliko hata mtumba.
       Kiuchumi. Uchumi usiojitegemea badala yake ukategemea kukopa na kuombaomba na ufadhili ilhali nchi ina kila raslimali nao ni uchumi mtumba. Sera za kuazima zisizoangalia maslahi ya wengi na kubeba ya wachache,  ukiachia mbali kutotekelezeka, nazo ni mitumba maana ziko imported kuja kutengeneza pesa kwa kutoa bidhaa chafu kama rushwa, kujuana,uzembe,wizi na mengine kama haya ambayo yameifanya dunia kuwa na matabaka. Huwezi ukaishi kwa kuomba omba usiwe mtumba hasa unapokuwa umejaliwa kila kitu kama raslimali na mazingira ya kuziendeleza. Hii ni changamoto chanya. Una ubongo mikono na utashi. Kwanini uridhike na umtumba au ukuku?
         Hata wale wasiojijua kuwa ni mitumba nao ni mitumba. Kama hutimizi wajibu wako iwe shuleni nyumbani au ofisini basi wewe ni mtumba tu tena ule uliokwisha wakati wake kulhali. Wakimbizi haramu wa kiuchumi na wafanyabiashara sawa na washirika wao wenye madaraka mitumba nao ni mitumba. Wafanya magendo wauza madawa ya kulevya, wakwepa kodi na wengine kama hao nao ni mitumba ya kiuchumi. Kwani hawapo? Wamejaa mipakani, viwanja vya ndege, kwenye bandari na kwingineko.
Kiutamaduni: Mmonyoko wa maadili na kutamalaki kwa dini kanyabwoya nayo ni dalili ya jamii mtumba. Kwani hazipo? Zipo tena nyingi zimejazana mijini zikitenda miujiza ya kutajirisha wajanja kwa kuwaibia umma maskini wajinga na wapumbavu huku mamlaka zikiangalia. Huwezi kuendekeza sadaka na mazingaombwe huku ukiwapigia watu wa Mungu kelele usiwe mtumba. Huwezi kutenda tofauti na ufundishavyo usiwe mtumba.
        Kuna mitumba ya madawa. Yapo mengi yaliyopitwa na wakati na mengine feki. China na India zimepata mahali pa kutengenezea pesa kwa kuuza vifo vya kujitakia kwa waathirika hasa wenye mamlaka. Zitashindwaje iwapo tumevamiwa na mifumo kichaa ambayo imezifanya nchi zenye utajiri mkubwa wa raslimali kuwa maskini kimaisha huku zikikenua meno na kuridhika kiasi cha kuitwa za ulimwengu wa tatu? Kwanini nchi, tena zenye watu wenye utimilifu wa viungo timamu, ziishi kwa kuomba omba kukopakopa na kufadhiliwa? Nani anakula hizo raslimali? Je huu siyo umaskini wa ubongoni na wa kujitakia?
        Kwanini mganga wa kienyeji wa kichina aweze kupewa leseni kuuza madawa ambayo hata lugha yake haieleweki kwa wateja wala alikopata ujuzi? Jaribu uende Uchina kufanya kama afanyavyo mchina hapa uone watakavyokufukuza kama mwizi. Inakuwaje waswahili walioko India wabaguliwe ilhali wale walioletwa na wakoloni watanue? Hivi unaweza kuviona kama vitu vidogo. Madhara yake ni makubwa. Leo, kwa mfano, mtanzania hawezi kuomba visa kwenda Uchina au India kutafuta riziki lakini wachina na wahindi wanakuja kila uchao. Hii siyo kujibugua na kuonekana fala bila sababu. Ndiyo maarifa. Lazima maarifa yakwambie kulinganisha mambo ili usipunje au kupunjwa. Maana kupunja na kupunjwa zote ni dhambi.
              Kuna hata siasa za mitumba. Kama kuna kitu balaa na cha hovyo duniani basi ni hiki. Maana yake ni kwamba ni sawa na kumuachia mtu mtoto mchanga amlee akamuua. Maana, siasa hizi zimeua nchi nyingi kiasi cha kuzalisha madiktetea walioacha historia inayonuka kama zebaki. Kufanya hivi ni kosa kubwa. Maana ni kuwaamini viumbe wasioaminika. Hawa hawana tofauti na kahaba apendaye kumridhisha kila bwana lakini moyoni akidhamiria kumuibia. Wengi wametumbukia katika mtego huu. Damu nyingi imemwagika na mataifa mengi yameparaganyika. Yote hii ni matokeo ya mawazo mitumba ambapo binadamu hujigeuza kupe akiwageuza wenzie ng’ombe. Wewe unaweza kuwa mtumba hata mimi. Kwani, nyani haoni nonihino lake. Muhimu, tieni akilini na kufikiri sawa sawa kila ulipo. 
Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: