Hivi karibuni, vyombo vya habari viliripoti uwepo wa uhaba wa wahadhiri na wafanyakazi kwenye vyuo vyetu vikuu na taasisi za elimu ya juu jambo ambalo linaathiri vibaya elimu yetu kama taifa. Hakuna lilioendelea au kujikwamua bila kuwa na elimu na namna ya kufanya hivyo. Hivyo, tatizo la uhaba wa wahadhiri na wafanyakazi kwenye taasisi zetu na vyuo vya elimu ya juu halina mjadala. Lazima tujiandae kulikabili na kupambana nalo vilivyo kama taifa na watu wenye akili. Kwa mujibu wa TCU, Tanzania ina uhaba wa wahadhiri 949 waliajiriwa kati ya 2019 na 2020. Hili linatia moyo na linapaswa kupewa umuhimu wa aina yake. Hata hivyo, kulikuwa na ongezeko na asilimia nne kufikia wanafunzi 206,305 kwa mwaka.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Lughano Kusiluka alisema shida hiyo bado haijashughulikiwa. Alikaririwa akisema “tumeshuhudia katika maeneo mengine wafanyakazi wakiajiriwa mara kwa mara, lakini inaonekana vyuo vikuu vimesahaulika kidogo. Tunaomba eneo hili pia likumbukwe.” Huu ni ukweli mchungu unaopaswa kuzingatiwa na kupewa suluhu na siyo kusema au kusoma na kuweka pembeni hasa kwa serikali yetu.
Kwa mujibu wa vyanzo na vyombo vya habari, ripoti ya 2017 ya Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU) ilibainisha uhaba wa wafanyakazi wa masomo katika taasisi za elimu ya juu nchini kuwa asilimia 44 jambo ambalo linazikumba taasisi nyingine nchini. Mfano, ripoti husika inaonyesha kuwa Mwaka 2019, Programu ya Elimu iliandikisha wanafunzi 54,156 (wahadhiri 524), Sayansi ya Tiba na Afya ilikuwa na wanafunzi 23,374 (wahadhiri 802). Programu za Sanaa zilikuwa na wanafunzi 6,345 (wahadhiri 616), Sheria wanafunzi 12, 424 (wahadhiri 205) na Biashara ikiandikisha wanafunzi 28,300 kwa wahadhiri 466. Hapa hakuna uwiano lengwa na stahiki.
Baada ya kugundua hali ilivyo, kama taifa, tufanye nini ili kuondokana na kadhia hii? Nashauri serikali ifanye yafuatayo:
Mosi, tuongeze umri wa kustaafu kwa watu na wafanyakazi wa taasisi za elimu ya juu ili kupambana na uhaba. Haina maana kuwapeleka nyumbani wastaafu wetu wenye ujuzi unaohitajika wakati wanaouhitaji hawana watu wa kuwapa ujuzi huu. Mambo ya kustaafu ni mambo ya kizamani na ya kikoloni. Ingekuwa amri yangu, ningeshauri itungwe sheria ambapo mtu ataamua mwenyewe kustaafu kama ambavyo huamua kuajiriwa, kujenga, kuuza nyumba, kuoa, kuolewa na hata kutoa msaada. Mbona wanasiasa hatuwawekei ukomo wa kugombea uongozi? Kwanini tunawaruhusu wastaafu wataalamu kugombea nafasi za kisiasa ambazo siyo sehemu ya ubobezi wao lakini tunawastaafisha toka kwenye maeneo walimobobea?
Pili, kuna haja ya mamlaka kutoa motisha kwa watanzania wanataaluma walioko nje kurejea na kufundisha nchini ili kuondoa au kupunguza tatizo. Hili ni muhimu. Kwani, watakuwa wanatoa mchango wa jamii na taifa lao kama watanzania na wana jamii iliyowatengeneza na kuwalea. Nchi zilizoendelea za magharibi zimeendelea kwa kuwatumia na kuwanyonya wataalamu wetu. Mishahara wanayopata–––kama ikilinganishwa na wananchi wa nchi hizi–––ima ni midogo au huifikia baada ya kunyonywa sana kupitia kwenye ajira au kupata ubobezi na ujuzi walio nao. Kuna wakati mwingine wanalazimika kuchukua uraia wa nchi za nje ili kusoma, kusomesha watoto wao hata kuishi kwa ujumla. Mfano, mtu aliyesomea udaktari wa binadamu au wanyama nje, haruhusiwi kufanya kazi moja kwa moja anapofika kwenye nchi za Magharibi. Licha ya kumrudisha shuleni, hulazimika kufanya mitihani mingi na kazi za majaribio kwa muda mrefu jambo ambalo–––licha ya kumnyonya na kumkatisha tamaa na kumchelewesha kimaisha–––hutoa nafasi ya mfumo na nchi husika kumnyonya na kufaidika. Ni bahati mbaya kuwa nchi zetu huwa hazioni hili na hata kama zikiliona, huwa hazilifanyii kazi ili kunufaika na wananchi wake wanaonyonywa nje ya Afrika. Hatuwahangaishi wataalamu toka nchi za magharibi wanapokuja kufanya kazi Afrika tokana na imani haba kuwa wao ni bora kuliko sisi jambo ambalo si kweli.
Tatu, ongeza uwekezaji kwenye kutengeneza wahadhiri wa vyuo vya elimu ya juu badala ya kuweka mkazo kwenye vitu kama miundombinu badala ya watu. Raslimali ya kwanza ya maana na muhimu kwa taifa na jamii yoyote ni watu wake na siyo vitu vyake. Tuwekeze kwenye utu kabla ya kuwekeza kwenye vitu ambavyo viko kwa ajili ya wat una siyo watu kwa ajili ya vitu.
Nne, ondoa vikwazo dhidi ya watanzania wenye taaluma za juu walioko nje kurejea na kuwajengea mazingira wezeshi kuchangia kuondoa tatizo hili mfano, kuruhusu uraia pacha na kuongeza mishahara vitakavyowashawishi na kuwavutia wasomi walioko nje. Kumekuwa na vuta nikuvute na sintofahamu kuhusiana na uraia pacha bila kujiuliza: inakuwaje nchi tajiri zinawapa uraia makapuku wetu na kuwaruhusu kuwa na uraia wao asilia, kutuma fedha kwao na kuwahudumia hata wakiwa kwenye nchi zao za asili lakini sis tunaogopa kufanya hivyo? Nani mwenye cha kupoteza kati ya nchi kapuku na tajiri? Mkenya mmoja mwenye uraia wa Kanada na Kenya alikuwa Kisii kimatembezi. Alikwama kurejea tokana na kuripuka kwa Ukovi-19. Kanada ilikuwa ikimpa dola 500 kila wiki kwa miezi tisa ili kujikimu. Je huyu Mkenyamkanada–––licha ya kutowabebesha mzigo ndugu zake na taifa lake–––pesa hii ilisaidia ndugu zake wangap tukizingatia ni fedha nyingi kwa viwango vya maisha ya kiafrika? Hapa tunachopaswa kufanya kama watu wenye akili timamu ni kutumia common sense kuangalia tunakosa au kupata nini tunapowanyima watu wetu urais pacha wakati nchi tajiri zikiwaruhusu wawe nao.
Nne, fidia wasomi walioko nje waliojigharimia kufikia shahada za PhD watakaoamua kufundisha nchini. Nchi za Ghana, Kenya, Nigeria na Uganda zinasifika kuwavutia wananchi wake walioko nje wenye viwango vya juu vya elimu kuwekeza nchini mwao kwa kuruhusu uraia pacha. Mfano, rafiki yangu Profesa Makau Mutua–––mwanasheria nguli mkenya mwenye uraia wa Marekani–––aliteuliwa mwenyekit wa tume kukusanya maoni ya katiba mpya na kufanikisha zoezi hili bila kuwa na hofu ya uzalendo kama ilivyo kwa Tanzania. Hakuishia hapo. Aliwania cheo cha jaji mkuu–––baada ya rafiki yangu mwingine Jaji mkuu mstaafu Dkt Willy Mutunga kustaafu–––japo hakupita siyo kwa sababu ya uraia pacha bali sifa.
Tumalizie. Kuna haja ya kuajiri watanzania walioko nje wenye PhD au ubobezi na utaalamu ambao wako tayari kulisaidia taifa lao kuchangia kama watanzania. Tuachane na mawazo mgando ya kimaskini kuwa watanzania walioko nje si wazalendo wakati mafisadi wetu wengi hawana huo uraia pacha na wala hiyo pesa wanayotumia ndugu zao hatuihoji wala kuigopa. Ama kweli, baniani maskini kiatu chake dawa!
Chanzo: Raia Mwema leo
No comments:
Post a Comment