The Chant of Savant

Tuesday 23 November 2021

Tutumie Malimwengu Kujitafakari na Kuitafuta Busara

Hapa duniani kuna vitu vingi vipo na si wengi wanavidurusu hata kukukumbuka kuwa vina mengi ya kuwafundisha ili lau wapate busara. Kama ilivyo ada ya safu hii, huwa tunadurusu mambo ya kijamii ya kila siku bila kusahau kufundisha busara. Leo tungalia busara yetu inachimbuka wapi na kwanini na ili iwe nini. Tuanze na kitu ambacho kila mmoja anakifahamu. Kaburi hung’ara kwa juu lakini ndani hujaa uoza wa mifupa na harufu mbaya. Ndani ya kaburi umejaa uharibifu usio wa kawaida. Nani haogopi kaburi? Je hawa wanaozini kwenye makaburi siyo mashetani hata kama wana sura na viwili wili vya binadamu? Hawa siyo makasha matupu yasiyo na mioyo wala akili timamu ukiachia mbavu ubinafsi na upogo wa kunuka? Kipi bora; kufanya kazi ya kusafisha kikombe ndani na nje? Je nani mpumbavu anaweza kupamba mzoga?         Dunia ya sasa imeharibika. Imelaaniwa si haba. Haina tofauti na mzoga. Je waja hawapendi uchafu kuliko usafi, giza kuliko mwanga, uongo kuliko ukweli,  haramu kuliko halali ukiacha mbali kupenda kujidanganya na kudanganya? Anayebisha aniambie kwanini tunahangaika kama tunavyohangaika. Mwenye mali anamuogopa asiye nayo na maskini anamchukia tajiri kwa sababu ya utajiri wa na si vinginevyo. Je sisi si makaburi?             Hatung’ari juu na kunuka ndani? Dunia imejaa silaha za maangamizi kila aina. Zipo za sumu na moto. Zipo hata za kelektroniki. Zipo hata za kibaolojia na nyingine nyingi zitagunduliwa katika mashindano haya ya ukichaa wa kuiangamiza dunia. Dunia imejaa chuki kuliko upendo, tamaa kuliko kuridhika na upofu kuliko kuona.
        Kazi ya silaha ni kuua siyo kuponya. Leo binadamu wanaogopana kuliko hata simba! Lugha ya sasa ni ya vita vita vita tupu. Mhalifu anamhukumu mhalifu saa nyingine mwenye nafuu kuliko yeye! Hapana. Mwenye hatia anamhukumu mwenye haki huku mchafu akimfundisha usafi msafi. Je hakimu na polisi waombao na kuchukua rushwa siyo wahalifu? Waulize mshahara wao na thamani ya mali zao utajua kinachoongelewa. Mtu anaamka maskini analala tajiri ni watu wanaona. Hata kama hawamwambii wanajua kinachoendelea. Je haya ni maisha ya heshima au ni nifaki na kujilisha pepo?        
         Kujilisha pepo ni tabia ya wapumbavu sawa na wavuta bangi. Maana mvuta bangi akiishavuta bangi yake hujuhisi yeye ni yeye wakati si chochote wala lolote bali mhalifu wa kawaida apaswaye kuishi korokoroni. Je ni wahalifu wangapi wanatanua mitaani ilhali wasio na kosa wanaoza magerezani? Fikiri na upige picha uone hali ikoje.
Binadamu wameukumbatia uharibifu kiasi cha kuigeuza dunia kuwa kaburi na wao wakiwamo! Je viumbe wa aina hii wanaweza kumcheka hayawani pweza ambaye kwa mapezi yake mwenyewe na upumbavu wake hujiteketeza?
        Machukizo makufuru na baya zaidi ni kichekesho kuwa wanadai waliumbwa kwa mfano wa Mungu! Mungu gani anajiteketeza mwenyewe? Watamjuaje Mungu wakati hawajijui? Kwanini kumsingizia Mungu au ni kwa vile hawezi kuonekana? Leo dini kwa dini zinachukiana hata kuwagawana watu! Dini bora ni ile itumikiao utu na kuijenga jamii siyo kuinyonya na kuibomoa. Si njia  zote huelekea kuliko hata kwema. Njia nyingine huelekeza machinjioni na bado ni njia. Kwa hiyo siyo kila njia ni njia ya kufuata.
        Kuna vilio kila kona. Kila kona kuna vilio. Uchafuzi wa mazingira, uwindaji haramu, utoroshaji wa magogo na madini. Yote hii ni ukaburi.  Uchafuzi wa maadili na haukubaki nyuma. Dunia imechafuka kweli kweli. Nani ataisafisha kama siyo wewe na mimi? Watu wanatumikia leo wakiisahau na kuiharibu kesho utadhani wataishi milele!
Wanadamu wameharibikiwa. Wanatumia pesa nyingi kwenye misiba wakati marehemu kabla ya kufa alilazwa hospitali kwa muda mrefu wasiende kumuona wala kumlipia gharama za matibabu. Wengine walimfilisi kwa kumfanyia matibabu ya uongo huku bila aibu wakimhadaa kuwa wamemsaidia kutibu ndwele yake wasijue wamemsaidia kubeba dhambi zake kwa sababu ya kutu yao ya kuchuma na kuvuna wasipopanda. Kwao hawa matatizo ni mtaji. Lakini wanasahau kuwa na wao wana matatizo saa nyingine makubwa na mengi na magumu kuliko ya huyu wanayemuongezea matatizo wakijidai wanayapunguza!
        Watu wapumbavu wanachangishana pesa za kusafirisha maiti lakini siyo za kuuguza! Je waliwahi kufikiria wangelikuwa ni wao? Ukitaka kujua ukubwa wa mguu wa tembo vaa viatu vyake. Utamchongeaje mtu jeneza la mamilioni wakati kuna umma unataka maelfu bado ubaki mzima? Wewe huna tofauti na mdudu bungua aozeshaye ubao maana unazika vitu ukijua vitaoza. Mbona hamuwaziki na vyakula na vinywaji walivyovipenda hata watu waliowapenda ambao ni nyinyi?
        Tumalizie kwa angalizo. Mara zote, busara huwa inaumiza kuwa nayo hata kuitafuta. Hivyo, sitashangaa kusikia kuwa kuna wasomaji wanaona hili katika haya niyasemayo hapa. Ndiyo busara ilivyo. Busara ni sawa na kwenda jandoni kutahiriwa. Siyo sawa na kwenda harusini au. Kwenye party. Ni sawa na kwenda kwenye matanga. Hivyo, msichoke kuitafuta busara kwani, kama ukweli, itawaweka huru.
Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: