The Chant of Savant

Sunday 21 November 2021

Jiulize kwanini mambo huwa hivi

Tokana na kutamalaki kwa Upungufu wa Busara Duniani, safu hii itakuwa ikiwaletea wapenzi wake makala juu ya busara ili lau tufundishane na kupeana busara. Tungetamani kusikia maoni ya wasomaji wetu. Baruapepe ipo. Kuna sababu nyingi kwanini wema na wenye busara hawadumu. Yawezekana hutokea hivi ili kuepuka kukua na kujichanganya. Hivyo uhai wa mwenye busara sawa na mwenye mali huwa mfupi lakini wenye maisha marefu baada ya yeye kuondoka. Maana huaacha mali na maarifa. Ni wangapi wanaishi maisha ya kijungujiko lakini marefu kuliko waishio kwa vinono na sifa wakakatiziwa uhai wao? Je lipi bora–––maisha marefu ya ufukara au maisha mafupi ya ushufaa? Mungu hawezi kukupa wala kukunyima vyote. Kama waliopewa vyote ni wachache. Ukipata hiki unakosa kile ili uweze kusaidiana na kutegemeana kuwa sawa na wenzako. Hii ndiyo maana ya tembo mwenye maguvu ya kuangusha miti kukosa nyumba lakini mchwa na ndege wasio na maguvu wala vikumbo wakawa na viota vyao. Wakati wanyama wenye maguvu hawana pa kuita kwao au kuweka mbavu zao, viumbe wadogo kama wadudu na ndege wana viota na mashimo yenye joto la kuwafanya walale kama wafalme kwa viwango vyao. Je fisi na simba wangejua kutumia visu wanyama wengine wangekuwapo? Je Nyati na tembo wangekula nyama fisi na simba wangekuwapo? Je pamoja na maguvu, meno na makucha yao fisi, simba na tembo huwa hawalali hata wakati mwingine kufa njaa? 
         Usicheze wala kufanyia njaa masihara. Hata malaika hulala njaa wakati mwingine. Mtoto mchanga anapofiwa na mama hula nini? Je wenye nguvu wote wangepewa utajiri nani angebeba mizigo? Je matajiri wangepewa kujiamini maskini wangekula nini? Je matajiri si maskini wa sifa ambao hutaka wasifiwe na maskini? Je matajiri wana vyote? Kama wanavyo, mbona wanatumia utajiri wao kuwaridhisha maskini? Je utajiri wa wenye nao waliupata wapi kama siyo kwa maskini ambao nao utajiri wao waliukosa kwa vile uko kwa wenye utajiri? Je wakubwa hawawaogopi wadogo tena wanaowatawala? Kama hawawaogopi, walinzi na mituringa vilivyowazunguka vya nini?
Je kati ya mwanamme na mwanamke kuna aliye bora kuliko mwenzake wakati wote wanategemeana? Bila mwanamke, mwanaume angezaliwa na nani na bila mwanaume mwanamke angezalishwa na nani? Wengi wangejua ushujana uvumilivu ukiachia kukjitoa mhanga vinaohitajika kuhimili uchungu, wasingehata fikiria kuwadharau wauhimilio. Je ni wanaume wangapi waliweza kushuhudia wake zao wakijifungua lau wapate elimu na kujua busara hii maana yake ni nini?                 Kabla ya kumdhalilisha mwanamke, mkumbuke mama yako. Na kabla ya kumdharau mwanaume, mkumbuke baba yako. Bila wawili hawa ungekuwa wapi kiumbe wewe? Epuka na ogopa mtu anayejua namna ulivyotengenezwa hata kama ni kwa bahati mbaya au makosa. Shukuru umetengenezwa. Je ungekuwa mdugu ungekuwa wapi sasa? Kwa kujua ukweli na umuhimu huu, epuka kumtukania mwenzako wazazi wake kwani nawe unao. Je hapa kuna mjanja wa kumdharau au kumnyonya mwenzake au ujinga na upogo mtupu? Je mtoto wa jana siyo mkubwa wa kesho na mkubwa wa kesho siyo mtoto wa jana?
        Kila zama ina yake; ndiyo maana wakaja wanafalsafa katika maumbo mbali mbali. Wapo waliokuja na falsafa za kisayansi wengine kidini kadhalika na kadhalika. Lakini wote lengo lao lilikuwa moja; kujaribu kuyadurusu malimwengu kwa kadri walivyoona kuelewa na kuweza. Walifanya yote haya pamoja na hatari na ugumu wake ili kuwapa jibu wanadamu waishi maisha mazuri. Wapo waliofanya hivyo ili kujinufaisha tokana na wengi kutopenda kutafuta maarifa. Wapo waliosukumwa na upendo wao na thamani yao kwa utu vilivyowasukuma kutoa zawadi hii ambayo wengi hawajui kuipokea wala kuitumia. Kadhalika wapo waliokuja kujilisha pepo kwa kuwatumia badala ya kuwatumikia wengine. Wapo waliosukumwa na tamaa zao kutafuta kuwatumia na kuwafaidi wenzao.
         Wengi mnakijua kisa cha mwanafalsafa wa kiyunani aliyesifika kwa  kudurusu. Aliwahi kutembea mchana kweupe akiwa na chemli. Alipoulizwa kwanini alikuwa akiwasha taa mchana kweupe, alijibu kuwa alikuwa anawatafuta watu wenye maadili asiwaone. Kadhalika nami nikikwambia kuwa kuna watu wanakufa kwa kiu wakiwa mtoni au ziwani utadhani uzushi. Kama unadhani hivyo, angalia ulipo. Jiulize ni kwanini wageni hukimbilia nchini kwako wakati wewe ukiikimbia. Kama tutajiruhusu na kukubali kufikiri kwa pamoja tutagundua vitu vingi ajabu.                         Usishangae ukakuta mahakamani hakuna haki na madhabahuni wamejaa wenye dhambi wakiwapoteza watu wema lakini waliokosa maarifa na busara. Wala usishangae kukuta vyuo vimejaa wajinga huku wenye elimu wakiwa mitaani bila ajira wala kuthaminiwa. Je kuelimika ni kupoteza miaka mingi vyuoni na kuwa na utitiri wa vyeti au kutatua matatizo yetu na ya wenzetu kama binadamu? Je msomi anayepotezwa na mjinga na mjinga nani msomi nan ani mjinga wa kweli? Je wasomi wanaodai rushwa hata ya ngono na majambazi wanaoua watu wana tofauti? Msomi anayedai rushwa anaua kesho ya mhanga wake sawa na jambazi anayemfanya mhanga wake asiione kesho.  Je tajiri mwenye magonjwa yanayomzuia kula kila atakacho hazidiwi na mbwa aliyemfuga anayeweza kula kitu?
        Ujambazi huu wa kuchezea hata kufikia kuiuza na kuinunua haki umewafanya watu wenye haki kuwa wanyonge. Hakuna suluhu baina ya mnyonyaji na mnyonywaji isipokuwa moja. Mnyonyaji kuacha kumnyonya mnyonywaji na mnyonywaji kuacha kukubali kunyonywa kwa kila hali hata kama kwa shari. Mkandamizaji aache kumkandamiza mkandamizwaji. Je kuna mkandamizaji mwenye akili timamu atakubali kuacha kukandamiza wakati kwake maisha ni ukandamizaji? Ni kupe gani yuko tayari kutoka mgongoni mwa ng’ombe? Hapa lazima mwenye kupambana na viumbe hawa laanifu aamue liwalo na liwe kwani hana cha kukosa bali kujikomboa. Nani hajui kuwa simbiko halisimbuliki ila kwa mikukuriko?
        Hapa hakuna mjadala wala namna isipokuwa kutenda haki tena haki tupu. Anayepaswa kutenda haki asipoitenda wanaofanya kutendewa lazima wamuasi kwa gharama yeyote. Je haki tupu ni ipi? Kila mmoja kuishi kwa jasho lake huku utu ukiongoza na kupanga kila kitu kwa ajili ya utu na watu wote kwa usawa. Zaidi ya hapa hakuna maelewano wala maisha hayana maana tena. Kiongozi hata mtawala mpumbavu ni yule asahauye waliompandisha kwenye ukuu. Maana hana tofauti na apandiaye ngazi akaipiga teke asijue wakati wa kuteremka ukifika ataporomoka badala ya kushuka. Hana tofauti na mtu apangusaye mashonde kwenye busati analotumia siku zote. Huu ni upumbavu hata ufanywe na wateule.
Chanzo: Raia Mwema kesho.


No comments: