The Chant of Savant

Wednesday 10 November 2021

Jamii nchini ishirikiane na mamlaka kufichua hujuma

Mkurugenzi wa TBL Jose Moran alikaririwa hivi karibuni na vyombo vya habari akisema kuwa “Tanzania ina idadi kubwa ya watu wanaokunywa pombe feki. Inakadiriwa kuwa asilimia 54.7 wanatumia pombe hizo ambazo hazina ubora na hazilipiwi kodi” Tujiulize haraka haraka–––kama TRA ingekusanya kodi hii–––kweli tungekuwa kapuku na ombaomba sifa ambayo tunaanza kuipenda, kuikubali na kuizoea? Je tunamkomoa nani? Je nani wanafaidika na utaahira na uvivu huu? Usishangae ukakuta ni wageni wanaoitwa wawekezaji ambao baadhi yao–––kama hawa wanaozalisha na kusambaza pombe hii haramu–––wameingia kama wawekezaji wakati ukweli ni wachukuaji. Ni mara ngapi baadhi ya matapeli wa kigeni wakishirikiana na matapeli wenyeji wamekamatwa wakijihusisha na wizi wa wazi kama vile kutoa huduma za simu bila vibali, kuuza bidhaa zisizolipiwa kodi wala kusajiliwa? Je tumejifunza nini kutokana na kadhia kama hizi kama taifa? Je kuna namna baadhi ya watendaji wetu wanahusika na kufaidika?
           Hapa kuna haja ya kufanya kibarua chetu vizuri kama serikali na wananchi. Kuna haja ya wananchi–––ambao ndiyo waathirika wakuu–––kushirikiana na mamlaka kufichua hujuma hii kwa taifa letu. Japo wengi wasioona mbali na walafi wanaona kuwa wakijipatia fedha ya haraka wanaukata wasijue baadaye wajukuu wao watalipia hata wao. Kama kawaida ya safu hii, narejea. Tuanzishe lifestyle audit yaani kila mtanzania kueleza alivyochuma na anavyotumia ili kujua namna ya kutozana kodi na kuchunguzana kwa wale ambao utajiri wao hauna maelezo.
          Tukirejea kwenye kashfa ya zaidi ya asilimia 50 ya pombe nchini kuuzwa bila kutozwa ushuru. Je kama taifa tunapoteza fedha kiasi gani na fedha hii ingeweza kutusaidia kufikisha huduma kwa wananchi na kujenga misingi ya uchumi kiasi gani? Kupata jibu, jiulize. Kama TBL imeweza kuchangia uchumi kwa kutoa kodi ya shilingi trilioni 3.7–––ambazo bado ni kidogo–––hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania ina walevi wengi. Je hii pesa inayopotea tokana na uzembe katika usimamizi ni kubwa kiasi gani na ingeweza kutusogeza kiasi gani? Kwa wanaokumbuka wimbo maarufu aliokuwa akiuimba Hayati Magufuli kuwa Tanzania si maskini bali tajiri inayoweza kutoa misaada badala ya kupokea, watakubaliana nasi kuwa tatizo la umaskini ni la kujitakia tu ima tokana na uvivu, tamaa au ujinga tu wa kawaida ambao hata nyani hawawezi kuujaribu achilia mbali kuutenda.
         Kawaida, kwa wenye akili, kilicho kigumu ni kutafuta pesa lakini siyo kuikusanya. Je inakuwaje sisi tunatenda visivyo kawaida kama jamii ya watu na taifa. Je hii pesa inakwenda wapi na kwanini? Je hali hii ya shamba la bibi imekuwa hivi kwa muda gani na tumepoteza kiasi gani? Je hakuna ushahidi wa kuwakamata walioko nyuma ya kadhia hii? Je nani atajibu maswali haya kama siyo mimi na wewe tunaosema serikali ni mali yetu wakati mambo yanakwenda hivi? Je serikali inasemaje kuhusiana na ukweli huu mchungu? Je hiki si chanzo kizuri kwa Mheshimiwa Rais kutumbua na kupangua hata kutengua?
          Kama kwenye ulevi ni hivi, kwenye maeneo mengine kama vile madini, utalii, uwindaji, uvuvi, ubadilishaji fedha za kigeni, uingizaji na uoaji bidhaa na mizigo, uhamiaji, ulinzi wa mipaka, utoaji vibali mbali mbali vya biashara, ukazi, ajira na mengine kama hayo hali ikoje? Je tunapoteza fedha kiasi gani ikilinganishwa na kile tunachokopa au kubomu?
            Najua wapo wanaoweza kushuku maswali yangu. Hawa wanapaswa wajiulize: kwanini Tanzania ni kimbilio la wageni toka mabara yote wakati watu wengi kwenye nchi nyingi za kiafrika wanakufa baharini wakikimbia umaskini nchini mwao? Jibu ni rahisi kuwa Tanzania kuna neema ambayo–––kwa bahati mbaya–––si mamlaka wala wananchi wanaweza kuziona na kuzifaidi zaidi ya kuwa mashahidi wa wizi wa mali zao kiasi cha kugeuka shamba la bibi. Je tuna tofauti gani na chura ambaye licha ya kuishi kisimani bado yu uchi? Tuna tofauti gani na nyani ambaye hukali mawe yenye madini asijue ni mali au wanyama mwitu wanaoingiza fedha nyingi za kitalii wakiendelea kuwindwa na kuuawa na kuwa maskini tokana na uhayawani wao? Je sisi ni wa hovyo hii? Hapana. Sisi ni binadamu kamili ambao tunapaswa kubadilika na kuanza kufikiri na kutenda kama binadamu wenye akili timamu, utashi na mipango ya baadaye.                                
         Tumalize kwa kusema kuwa imetosha. Tubadilike tufaidike badili ya kuwafaidi wengine ambao wanatucheka, kutubagua na kutuona mataahira au hayawani waliojaliwa utajiri ambao hawawezi kuufaidi wala kulinda na kuutumia. Ama kweli alijesemea Hayati Magufuli. Tanzania si maskini wa mali bali uwezo wa kuelewa na kusimamia na kufaidi alichoijalia Mwenyezi Mungu. Ama kweli, mjinga huumwa kwenye tundu la nyoka mara moja. Mpumbavu hung’atwa mara mbili na zaidi. Tieni akilini ndugu zanguni.
Chanzo: Raia Mwema leo                                                                                                                                                                                                                                                                                                 

No comments: