How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 16 November 2021

Tujifunze Kuwa Jamii na Watu Bora na Si ya Kuku

Siku hizi kuna uoza unafanyika na unaitwa usasa. Siku hizi watoto hawana adabu. Watu wazima hawana adabu. Wavulana wanaoa mama wazee huku wazee wakitimbea na vitoto vichanga umri wa wajukuu wao. Matusi yamegeuka dili na staha maudhi. Hebu sikiliza miziki inayoitwa ya kizazi kipya ilyojaa ukalena ukakasi. Mingi ni matusi na utopolo kama wasemavyo watoto wa mjini. Ajabu ina soko kwa sababu wajinga na malimbukeni ni wengi. Siku hizi elimu haina thamani sawa na usanii. Sichukii usanii wala wasanii wa kweli wala simaanishi usanii wa sanaa bali ule ujanja ujanja wa kutafuta kuukata. Aukataye huonekana mjanja kuliko hata msomi asiyependa kuutumia usomi wake kutenda movu kwa kisingizio cha kuukata. Siku hizi hata watoto wanawatukana wazazi. Utawasikia wakisema kuwa wazazi hawakuwatengenezea mazingira mazuri ya kufanikiwa kana kwamba wao waliwatengenezea. Wengi waliofanikiwa kiukweli walisota ndipo wakafanikiwa. Mafanikio hayana njia ya mkato. Mtawalaumu na kuwatukana wazazi wenu bure.
        Amtukanaye mzazi mmoja huwa kawatukana wote. Amtukanaye mzazi wake anajitukana mwenyewe. Kwani, bila yeye asingekuwa yeye wala chochote. Na aibu ya mzazi mmoja ni aibu ya wazazi na taifa zima kwa ujumla. Amdharirishaye mtoto wa mwenzie anamdharirisha mtoto wake na yeye mwenyewe.  Hana tofauti na kuku alaye mayai yake. Je nani anafikiria hivi siku hizi ambapo kila mmoja ameshikilia lake utadhani yeye ni kisiwa kiishicho peke yake? Watu hutegemeana na huu ndiyo ubinadamu. Ni kaburini peke yake ambapo mja huacha utegemezi kwa wenzake. Hata afikishwe huko lazima afikishwe na wenzake.
        Mzazi na mwalimu bora duniani ni yule amfundishaye mtoto au mwanafunzi wake asiamini kila asikiacho bali akichunguze kwanza ndipo naye ajiamurie badala ya kufuata mkumbo kama bendera ifuatavyo upepo. Mwanafunzi mzuri ni yule anayohoji kiakili hata kuasi asipoelewa kuliko anayekubali kila jambo. Mpumbavu hushonewa joho bila kupimwa naye huliingia asijue laweza kuwa kitanzi! Hata panya na nyoka hawaishi kwenye mashimo yasiyo yao. Anayekubali kila jambo hana tofauti na mbwa afuataye kila aamrishwacho na bwana wake hata awe mpumbavu. Mbwa amejaliwa kunusa. Hakujaliwa uwezo wa kufikiri ingawa anafikiri kimbwambwa. Afanyaye hivi hana Maana. Huyu ni sawa na kondoo aweza kuongoza njia yake kuelekea machinjioni. Kama kichaa anaweza kuongozwa na kipofu kwenye maangamizi yake mwenyewe kwa jambo ambalo hata angelishinda. Siyo kila imani ni imani safi bali nyingine ushetani. Hata hizi dini zilizoota kama uyoga kila mahali siyo zote ni dini nyingine ni makampuni ya wajanja wachache wanaomtumia Mungu kutenda uovu wao.
            Ajabu waswahili walivyokuwa limbukeni, japo si wote, wanaagiza hata vinyago wakati jadi yao ni kuvichonga! Wanavinunua kwa bei mbaya sawa na mtu aokotaye bomu akidhani kapata kumbe kapatikana! Wanavaa mitumba wakati wanalima pamba! Je huku siyo kuwa na ubongo wa kuku kiasi cha kuisha kwenye jamii kuku? Haya yanaudhi. Lakini lipi baya kuyasema na kuyalaani au kuyatenda?
         Ukuku siyo wa nguo tu. Hata watu hata jamii vyaweza kuwa na ukuku visijue. Tumuangalie kuku kwa kuiainisha katika nyanja karibu zote za kimaisha.
             Kuna kuku katika kuukuu ambapo kuku hutegemewa na maskini waliosikinishwa na ufisadi na tawala mbovu uliotamalaki dunia nzima. Watu na akili zao wanageuzwa bidhaa nao wanakubali! Kisa? Kukosa maarifa. Maarifa siyo usomi wa shahada bali wa nyakati. Kuna watu wanalima pamba lakini wanaishi kwa kuvaa mitumba! Huu ndiyo ukuku mwenyewe wa kuzalisha usichokula na kula usichozalisha. Kuku hutaga mayai yenye kila viini viufaao mwili. Lakini wenye maarifa huja na kumnyang’anya mayai yake na kuyageuza yao huku wakimvimbisha na nafaka kavu. Hapa jibu ni rahisi, umoja, ujasiri, kujitambua na kufanya mapinduzi ya kifikra na kuthubutu. 
            Mara nyingi wanyonyaji huwa woga. Hujificha kwenye vitisho hata kutengeneza maadui wa kufikirika ilmradi kuwaaminisha wanyonyao kuwa bila wao kuwa walipo maisha hayawezi kwenda. Kuwavumilia watu hawa ni umbuni ambaye humuona adui akaficha kichwa kwenye mbawa zake. Huu ni ukapu kupokea kila kiingizwacho.
           Je watu walioaminishwa kuwa pamba ni zao la biashara wakati ukweli ni la kikoloni wakalima pamba wakaishia kuvaa mitumba siyo sawa na kuku? Je hawa wanaowasimamia katika jinai hii inayoitwa biashara wakiwaaminisha kuwa huu ndiyo uchumi wa kisasa chini ya dhana mbali mbali kama ubinafsi wanaouita ubinafisishaji, utandawizi wanaoupa jina zuri la utandawazi siyo kuku kimaarifa? Heri ya kuku hayawani kuliko kuku binadamu wa ubongo. Maana kuku ni muathirika wa utumwa mbaya kuliko hata ule wa kufungwa kongwa viungoni maana unaweza kujikomboa kwa kukata kongwa. Utumwa wa hiari ni mbaya kuliko hata ukoma. Maana ukoma unaweza kuzuiliwa na kuzuilika kuliko fedheha hii ya binadamu. Watu wajipelekao utumwani hawana tofauti na mbwa ajipekaye kwa chatu.
        Kuku maskini ni mahuluku. Ameumbika hivyo. Amejaliwa hivyo. Hana maarifa hata ubongo wake ni mdogo haujai hata kijiko cha chai. Pamoja na udhaifu huu kiumbe huyu mdogo maskini bado hawanyonyi wenzake kama binadamu wanavyofanyiana. Hata vifaranga vyake havimnyonyi yeye kama ambavyo asivyonyonya wenzake zaidi ya kunyonywa na binadamu. Kuku ana nafuu hatendi dhambi hii chafu. Je binadamu anapoukumbatia ukuku siyo kudhalilika zaidi ya kuku?
        Kuna haja ya kutafakari na kupenda maarifa hata kama kuyapata ni mateso na jitihada nyingi na ngumu za muda mrefu. Heri kuanza kwa mateso ukamaliza kwa raha kuliko kuanza kwa raha ukamaliza kwa mateso. Japo watu wengi huamini kuwa kutafuta maarifa ni kazi ngumu, ni kazi rahisi; muhimu, mja awe tayari kuzingatia kila afanyalo aonalo asikialo na kadhalika. Kila mahali kuna maarifa. Dunia nzima ni darasa moja kubwa sana lenye kila nyenzo ya kuwasilisha maarifa. Kuna jamaa mmoja alichukia sana magugu kiasi cha kujigamba mbele ya wenzie kuwa magugu ni mimea isiyo na thamani wala faida yoyote duniani! Maskini hakujua kuwa magugu na mimea mingine ya kijani ndiyo ivutayo mvua. Hakujua kuwa magugu ndiyo mimea mingi hata kuliko nyasi! Je magugu ya mimea siyo bora kuliko magugu binadamu?
        Mwisho wa jambo baya ni mzuri kuliko mwisho wa jambo zuri. Na mwisho wa jambo zuri si mzuri kama mwanzo wake. Heri kulia kwanza ukamalizia na kicheko kuliko kuanza na kicheko ukamalizia kilio. Heri kudhulumiwa kuliko kudhulumu kwani adhulumuye hatakufa bila kuonja dhuluma ya dhuluma yake. Wahenga walisema heri kumaliza kuliko kuanza. Hujasikia kuwa akuanzaye mmalize? Msema kwanza hajui atajibiwa nini na vipi. Hivyo, kufikiri hata mara mia kabla ya kuropoka haraka ni bora kuliko vyote. Maana, ulimi uliponza kichwa. Lakini ulimi huo uwezao kuozesha mwili kama ukitumiwa vizuri unaweza kuliokoa taifa. Ndiyo maana diplomasia haitakufa wala kuachwa katika dunia iliyojaa mamlaka nyingi za kikuku kuku.
        Kuna kuku wenye magari hata majumba. Hili ni eneo la walionacho. Je magari ya bei mbaya wanayotembelea wale wapendwao kuitwa waheshimiwa hata kama hawana heshima siyo matokeo ya unyonyaji iwapo wale wanaoyagharimia wako hoi bin taabani? Pesa wanayotumia siyo sawa na mayai ya kuku achukuayo binadamu toka kwa kuku? Kama siyo basi wayapandayo wanaweza kuwa mwewe. Watashindwaje kuwa iwapo wahusika wanakula na kushiba ilhali wanaodai kuwatumikia kumbe wakiwatumia wanakufa njaa? Watashidwaje kuwa iwapo wanajiwakilisha wenyewe badala ya umma? Umma siyo kuuma bali kuhudumia. Bahati mbaya, tangu uongozi ulipokosa miiko ya maadili, kila mwenye kuupata aliutumia kuliwakilisha tumbo lake badala ya wale adaio kuwawakilisha.
Chanzo: Raia Mwema kesho

No comments: