The Chant of Savant

Tuesday 23 November 2021

Wengi Wasichojua Kuhusu Ng'ambo

Hivi juzi, nchi ya jirani ya Marekani, kijana wa kizungu Kyle Rittenhouse aliishangaza dunia alipoachiwa huru baada ya kukutwa hana hatia kwa mashitaka matano ya uuaji. Kilichofanya ashangaze dunia ni ile imani kuwa angekuwa siyo mzungu, angefungwa kwa makosa yote si kwa sababu aliyatenda au la bali kwa vile ni mweusi. Hivyo, leo, nitaongelea ubaguzi wa kimfumo japo kwa usiku. Kabla ya kuanza kuishi hapa Kanada, sikujua ubaguzi katika uhalisi wake. Ubaguzi haukuwa moja ya suala ambalo lingenihangaisha kama ilivyo sasa hasa baada ya kuingia kwenye taaluma ya kusuluhisha migogoro, diplomasia na vita hasa ugaidi. Nikiwa nyumbani, nilizoea kumsikia Hayati Christopher Mtikila akilaani ubaguzi japo kwa ubaguzi jambo ambalo sikuliunga mkono. Hata hivyo, Mtikila atakumbukwa kama mtanzania aliyesimamia haki na usawa wa watanzania ambao–––hata hivyo, bahati mbaya–––si wengi walimuelewa.
Nilipoanza kuishi hapa nilianza kumkumbuka na kumuelewa Mtikila kuliko wakati nilipokuwa nyumbani hasa baada ya kuona hapa tunavyoitwa watu wa rangi au peoples of colour. Niligundua ubaguzi ndani ya ubaguzi. Nani alidhani, kwa mfano, mhindi hapa angewekwa daraja moja na mswahili wakati mzungu huyu huyu alipokuwa akitutawala alimpa daraja lake na kumtofautisha nasi ukiachia mbali kuwa, kihistoria, wahindi wana mfumo wa kibaguzi uitwao caste? 
        Nilishangaa kuona wazungu wakiwaweka waafrika, waarabu, wahindi, wafilipino na wengine kundi moja huku wachina na wajapan wakiwekwa kwenye kundi lao. Nilikumbuka nilipokuwa kwenye mji wa Winnipeg nilipoingia kwenye duka la mhindi mmoja nikasikia anaongea Kiswahili nikamsalimia naye akajibu kwa kusema “karibu brother’ kitu ambacho si rahisi kulisikia tukiwa Dar. Hapa ndipo kilipo kigeugeu, kizungumkuti na mizungu ya mzungu kwa wale wasiomjua.
Katika kuishi hapa, niligundua kuwa hataw wazungu wanabaguana wao kwa wao kama wahindi. Hivyo, japo siungi mkono ubaguzi wa aina yoyote, naweza kusema kuwa bila ubaguzi, wazungu hawana maendeleo ya kivitu wanayojivunia. Ndiyo, bila ubaguzi, wazungu na hata waarabu wasingemkamata binadamu mwenzao na kumfanya mtumwa au punda mnyama na wakaendelea kumbagua na kumnyonya hata akiwa barani mwake. Hii ndiyo siri ya nchi za kiafrika kuendelea kuwa maskini. Zinatumikia mfumo wa kibaguzi wa dunia ambapo mtu hunufaika kutokana na rangi yake bali siyo stahiki wala ujanja wake. Hii ndiyo maana mzungu akija Afrika ananyenyekewa na kuonekana mjuzi hata kama hana ujuzi wakati mswahili akionekana hajui lolote hata kama hana ujuzi. 
Tokana na kujenga na kunufaika na mfumo wa kibaguzi na kinyonyaji, si ajabu kukuta mswahili mwenye elimu ya juu na nzuri akiwa na bosi ambaye hata hafai kuwa mwanafunzi wake. Si ajabu kukuta waswahili wanaonekana tishio Ulaya sasa wanapovuka bahari kwenda kule wakati wazungu walipovamia na kuitawala Afrika halikuwa tatizo la kumtoa mtu jasho kama ilivyo sasa. Ndiyo maana hata wenzetu walioko China na India na Mashariki ya Kati wanabaguliwa sisi tukiwanyenyekea na kuwashobokea wao. 
        Kwa wenye kutaka kufuatilia, hebu tafitini jamii moja ya kiafrika iliyoko India iitwayo Jarawa waishio kwenye kisiwa cha Andaman ambapo wahindi huenda kuwaangalia kama waangaliavyo wanyama kwenye mbuga za wanyama na hakuna nchi ya kiafrika inayotaka angalau maelezo. Hapa ndipo ulipo mzizi wa fitina. Je nini somo hapa?                     Msipoanza kujithamini na kuacha kushobokea wageni hasa kwa kuwaona wao ni wa maana kuliko nyinyi mtaumia. Je nani anasoma haya na kuchukua hatua? Kwanini hafanyi hivyo zaidi ya kuponzwa na imani kuwa mtu mweupe ni bora kuliko mtu mweupe na mkombozi wake wakati kihistoria ni mtesaji na mnyonyaji wa kawaida kama tutarejea biashara ya utumwa, ukoloni, unyemelezi na ulowezi kama haya mabaki ya watu walioletwa na wakoloni na kuendelea kutukuzwa wakati hawana pa kwenda na kama kuko hakuna lolote sawa hapa.
Nadhani wengi mnakumbuka mauaji ya waswahili kule hapa nchi ya jirani ya Marekani yanayofanywa na polisi. Mswahili anauawa kama mnyama na hakuna kinachofanyika. Tatizo ni mfumo huu wa kibaguzi.  
        Mzungu mmoja akitekwa kwenye nchi ya kiafrika, au ya Asia, wenzake wanavunja hata sheria kwa kutoa fedha aachiwe. Je mswahili akifanyiwa hivyo?  Nani anajali iwapo hata waswahili wenzake–––kama wanyama pori wanaomwacha simba amrarue mwenzake–––hawajali. Tujifunze kujaliana, kujithamini na kuheshimiana. 
        Kipindi fulani nilitaka kuwapiga picha ombaomba wa kizungu nilipokuwa nimefika hapa–––nikiwa bado mshamba. Nilionywa nisifanye hivyo. Kwani, madhara yake yangekuwa makubwa kuliko nilivyotegemea wala kudhania.  Niliufyata. Kwani, nilikuwa kwenye nchi ya watu njapo nilidhani mambo ni kama kwetu ambapo kila kitu ruksa hata udhalilishaji utokanao na ujinga wetu wa pamoja, collective ignorance. Je ni waswahili wangapi wanapigwa picha na mashirika ya kizungu na kuja huku na kutengeneza mabilioni ya dola kwa kisingizio cha kusaidia waswahili maskini wakati ukweli ni kwamba wanapewa kiduchu, na kuaminishwa kuwa wao ni maskini wasioweza kuishi hadi wafadhiliwe? Hapa ndipo lugha ya wafadhili ilipoanzia na kuota mizizi.
Tumalizie kwa kusema wazi. Hisani huanzia nyumbani. Upendo, heshima na thamani vinaanzia nyumbani. Kama hujipendi, usitegemei wengine wakupende. Kama hujiheshimu au kujithamini, usitegemee wengine wakupende au kukuthamini. Kama watu tuliojaliwa na Mola wetu rangi yetu, tuionee na kujionea fahari huku tukijifunza na kupambana na mifumo inayotubagua na kutukandamiza ili iendelee kutunyonya. Kwa wasiojua hali ilivyo majuu, lau wamepata mlango wa kuanza kujifanyia utafiti na kugundua na kuibua mengi. Nangoja maoni ya wasomaji wangu.
Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: