The Chant of Savant

Tuesday 9 November 2021

Matendo Yazungumze Badala ya Maneno

Uongozi ni dhana ya wachache kuendesha. Na kusimamia shughuli za wengi kwa ridhaa ya wengi. Uongozi pia unaweza kuwa dhamana kwa mtu mmoja kufanya kuendesha shughuli za kundi kulingana na masharti, utaratibu na miiko vilivyowekwa na wenye shughuli husika. Kimsingi, uongozi ni utumishi wa wachache kwa wengi. Uongozi usio na miiko ya maadili si uongozi bali ujambazi. Maana bila kanuni kutakuwa na mvurugano na mparaganyiko. Je ni nani awezaye kufundisha usafi ilhali yeye ni mchafu? Huu nao ni unafiki tena mbaya. Kuongoza siyo kuwa juu ya watu bali kuwaonyesha njia ukitangulia katika kila jema na katika kujitenga na kupambana na mabaya na maovu. Ni kuwasikiliza na kuwatumikia watu waliokupa uongozi ambao ni nguvu yao ya kufanya mambo yao.

 Uongozi ni huduma na siyo kujihudumia. Unapaswa kuwa macho na kuyaenga, kuyadurusu na kuyajua haya bila kusahau kuyazingatia na kuyatimiza kwa matendo. Kwani, matendo huongea zaidi ya maneno matupu. Je macho yangekuwa kichogoni tungeona nini vipi tungeona vilivyopo mbele yetu? Je kipi bora kuona mbele au nyuma? Unapoongoza ukikaa nyuma ujue umma pamoja nawe kiongozi mtarudi nyuma hata kukusaga wewe uliyeko nyuma yake. Ila ukiwa mbele utakufuata kwa hatua maridadi na mwendo salama. Jaribu hili uone utakavyopumua badala ya  kujifungia nyuma ya walinzi wenye bunduki. Je nani anaweza kuukimbia umma milele? Huyu hakika ni mpumbavu sawa na mtoto akimbiaye kivuli chake asikiache. Je ni bora kwa mtu mzima kufanya utoto? Mtoto hufanya utoto akitegemea kuelimishwa na kukua na kuelewa. Na je mtu mzima asiyekuwa si hovyo kuliko hata mtoto anayekua? Je maskini mwenye busara si bora kuliko tajiri mpumbavu?

Kuna viongozi wa baadhi ya mataifa hawalipi kodi. Ajabu wanaishi kwa kutegemea kodi za maskini! Huu ni uchui na siyo lazima kila chui awe na madoa. Kuna madoa mengine huwa ndani yakifichama. Ni wenye busara wanaoweza kuyaona ila wapumbavu huwa hawawezi kuyaona. Kiongozi wa kweli haogopi anaowaongoza ila mtawala huwahofia na kuwaogopa anaowatawala. Kiongizi wa kweli ahitaji walinzi na mitutu kwani utendaji wake ni ulinzi wake wa kweli.

Hamshangai kusikia eti kuwa taifa kubwa duniani lazima uwe na silaha za maangamizi! Dunia iliharibikiwa pesa na nguvu vilipochukua nafasi ya maarifa. Kuna nchi hutoa pesa kugharimia vita lakini zikadai hazina pesa ya kugharimia afya na maendeleo ya jamii! Nchi hizi ni bingwa wa kuomba na kupokea misaada ya silaha na wataalamu wa kivita! Na nchi tajiri hutoa tu. Ili iweje? Wapumbavu na wenye tamaa wamalizane huku nchi zijionazo wajanja ziwaibie. Yametokea Liberia, Angola, DRC, Sierra Leone hata mashariki ya kati kwenye vita ya mafuta. Kwani dunia haikushuhudia dikteta akimpindua dikteta na gaidi akimsaka gaidi? Nani hajui ukweli huu hata kama tunaogopa kuwambia ukweli wababe? Uliza akina Saddam Hussein walipinduliwa na kukamatwa na kuuawa na nani kama siyo watu wenye uovu tena mkubwa kuliko wao. Uliza akina Kwame Nkrumah, Patrice Emile Lumumba na wengine kama hao waliuawa na nani na kwa nini? Uliza akina Jonas Malheiro Savimbi, Joseph Desire Mobutu, Idi Amin, Jean-Bedel Bokassa na wengine walitengenezwa na nani na kwa ajili gani? Nani alianzisha kuendesha utumwa na ukoloni na kufaidika na jinai hizi?

Kuna nchi ziko tayari kutumia mabilioni kuuza tamaduni na mila zao bure. Maskini wasio na busara hupokea mambo haya wasijue wanaharibiwa kama viwanda vya sigara vigawavyo sigara bure kwa watu wasiovuta ili wakishavuta wakolee viwauzie! Akufundishaye kuvuta sigara au kunywa pombe hukuingiza kwenye utumwa na umaskini. Maana kesho utakopa ili ununue upuuzi huu ambao ukikutawala utatumia hata pesa ya chakula kuununua ushinde njaa. Utumwa siyo wa kufungwa kamba maungoni hata kufungwa kongwa ubongoni ni utumwa tena mbaya kuliko ule wa kamba maungoni. Mfugo hauwezi kumcheka mtumwa. Utumwa wa kujitakia hauna tofauti na kufugwa. Maana mhusika hushindwa kujiamini akaamini kuwa maisha yake yanaweza kuendeshwa na mtu mwingine vizuri kuliko yeye mwenyewe. Mtumwa wa kujitakia amchekaye mbwa au mbuzi hata kuku ni sawa na nyani amchekaye tumbiri. Maana tumbiri ana nafuu kimaisha akilinganishwa na nyani.

Wafalme wengi hupenda usimba ili waonekane mashujaa na tishio kwa wanaowatala. Lakini husahau kuwa sifa kubwa ya simba hasa dume ni uvivu na unyonyaji! Wengine huupenda ujogoo wasijue kuwa sifa ya jogoo ni umalaya na kuwafundisha vifaranga kunya ndani!

Kuna viongozi wa baadhi ya mataifa hawalipi kodi. Wanawahimiza walipa kodi walipe kodi ili wao watumie. Kwani wanaishi kwa kutegemea kodi za maskini! Huu ni uchui na siyo lazima kila chui awe na madoa. Kuna madoa mengine huwa yanajifichandani. Ni wenye busara wanaoweza kuyaona ila wapumbavu huwa hawawezi kuyaona. Mzee wa kichina–––ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuhofia kupatilizwa na wale ambao mawazo na maoni yake yangewaudhi–––aliyejinyima na kutoa kodi ili kuendeleza jamii yake kwa ajili ya vizazi vijavyo–––alipoulizwa nani kiongozi alisema “kiongozi asiyelipa ni mnyonyaji sawa na mkwepa kodi anayewanyonya walipa kodi tena maskini.”

Dunia ilianza kuharibika zaidi maarifa yalipoanza kuuzwa. Ajabu hata utamaduni siku hizi unauzwa! Takataka nazo zinauzwa! Kuna nini kwenye filamu za mauaji na uzinzi zaidi ya kuwa sumu na takataka? Je huu siyo utamaduni wa kukipoteza kizazi kipya? Ajabu kikishapotea wale wale waliokipoteza wanakuwa wa kwanza kusimama na kupaza sauti kukilaumu! Unamnulia mwanao bunduki ya bandia ili akikua afanye nini? Akikua akawa jambazi au muuaji utamlaumu yeye au wewe? Nani anamnunulia mwanae njiwa siku hizi? Ajabu katika vikorokoro vya kuchezea majumbani siku hizi hakuna mfano wa mizani hata mmoja! Je hawa kweli wataijua haki? Je mizani ikichezacheza kwenye egemeo lake siyo somo kwa watoto? Je nani alisahau michezo aliyoicheza utotoni? Leo tunawaonyesha watoto wetu mapicha na mafilamu ya wauza unga wakianza kudandia meli kwenda kutafuta unga huo huo tunawakamata viwanja vya ndege wakati sisi ndiyo chanzo! Je mamlaka zinazoua elimu zinategemea nini? Kuna mambo ya ajabu na ya kipumbavu siku hizi. Je midori mingi tuagizayo siyo aghali kuliko vitabu vya watoto? Nani anamnunulia kitabu mtoto achezee badala ya midori? Kucheza ni sehemu ya kujifunza. Kama taifa na jamii ya watu tieni akilini.

Chanzo: Raia Mwema Jumatano kesho

No comments: