Mheshimwa Rais, nakusalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama kiongozi wake tena mwanzilishi wa salamu hii. Leo barua yangu inaweza kuonekana kama yenye kungung’unika hata kukata tamaa. Naweza kukiri kuwa sina raha kuhusiana na ninalokuandikia. Naandika kuhusiana na sintofahamu ya mradi tata wa uwekezaji wa Bandari ya Bagamoyo ambao Hayati Dkt John PombeMagufuli alisema wazi wazi tena mchana kweupe kuwa ni wa hovyo; na hata kichaa hawezi kuukubali. Tarehe 7 Juni, 2019, akihutubia Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Hayati Magufuli alisema kuwe “kwenye mkataba wa ujenzi wa bandari hiyo kulikuwa na vipengele vya hovyo” ambavyo hata kichaa asingeweza kuvipitisha na kuutekeleza mradi tajwa. Alisema kuwa “wawekezaji hawa wanakuja na masharti ya ajabu na ni kichaa tu anaweza kuyakubali.”
Magufuli aliendelea kumwaga mtama ambao kuku sasa wanatema kuwa “huruhusiwi kukusanya revenue…. unatakiwa uwape guarantee (dhamana) ya kwanza bila hata kuulizwa kwa miaka 33. Unatakiwa uwape lease (mkataba wa kumiliki wa ardhi) tofauti na sheria za nchi ‘for 99 years’ (kwa miaka 99) na huruhusiwi hata kwenda kumuuliza atakayekwenda kuwekeza pale na wao wawe na mandate (mamlaka)ya kuchukua hilo eneo kama ardhi yao.”
Kuzidi kutoa maarifa zaidi Magufuli alisema “ni nchi gani hiyo ambayo unajenga Bandari ya Da res Salaam, tunachimba sasa hivi bath (gati) 0 hadi 10 kwa gharama ya Sh1.2 trilioni, tumekopa fedha… na contractor (mkandarasi) yupo na inawezekana at the end of this year (mwishoni mwa mwaka) watamaliza…tutakuwa tunapata mizigo karibu ya mara tatu inayoingia…leo hii unakwenda kudump (kutupa) hela pale Bagamoyo maana yake siutakuwa unaua bandari hii iliyoachwa na Nyerere?”
Japo Magufuli alikuwa binadamu, linapokuja suala la uzalendo, sijui kama kuna mwenye shaka juu yake hasa tukiangalia mambo aliyoweza kufanikisha ndani ya muda mfupi wa uongozi wake mfupi lakini wenye kutukuka. Hivyo, tunapomlinganisha na wanaotuambia mambo tofauti na yale aliyosema, ukweli, tunaingia kwenye kishawishi cha kuanza kujenga mashaka hata kabla ya kupata maelezo japo Magufuli hakuwa malaika bali binadamu na mwanasiasa.
Mheshimiwa Rais, hata kabla mwili wa Hayati Magufuli haujaoza wala kauli zake kufanyiwa kazi, aliibuka Waziri wa Viwanda na Biashara Godfrey Mwambe––naye akisema hadharani japo bila kutoa maelezo ya kina kuwa––––hakuna mkataba wakati Rais alisema upo na ni wa hovyo. Kusema ukweli, Mwambe alituchanganya na kutushangaza wengi kwa kusema na kurudia kuwa hapakuwa na mkataba. Alituacha hoi zaid pale aliposema kuwa mengi yaliyosemwa hata hajui yalitoka wapi wakati si ya kweli. Mapaka sasa, tunaomfahamu Hayati Magufuli nawe Mheshimiwa Rais hatujaamini masikio yetu achilia mbali ukweli wa suala zima. Tunashindwa kuelewa ukweli na uongo ni upi na kwanini na kunani.
Mheshimiwa Rais, katika kukumbuka na kutafakari kauli za Magufuli, je hapa ukweli ni upi? Je hapa tumwamini nani kati ya Hayati Magufuli, mzalendo wa kweli kwa maneno na vitendo na mteule wake Mwambe ambaye anasema anakuwakilisha wewe ambaye ulikuwa msaidizi wa Magufuli ambaye bila shaka ulijua kila kitu tokana na nafasi yako? Je maneno na msimamo wa mwambe ndiyo vyako? Je wakati Magufuli akisema aliyosema si ulikuwepo? Kama hukujua tueleze na kama ulijua tueleze na kwanini sasa U-turn kama wasemavyo watasha.
Mheshimiwa Rias, kwa vile Hayati Magufuli na Mwambe ni binadamu tena wanasiasa, tungeomba uingilie kati tujue ukweli na uongo na sababu za kugeuka ghafla bin vu kwa jambo ambalo liliwekwa wazi na kiongozi ambaye wengi walimwamini.
Mheshimiwa Rais, kwa kumbukumbu zilizopo ni kwamba wewe na Waziri Mkuu mlihudhuria mkutano huu ambapo Hayati Magufuli aliamua kuweka mambo wazi. Sina uhakika kama Mwambe alihudhuria japo nina uhakika anajua kila kitu alichosema Magufuli. Kwa vile maelezo ya Mwambe yanakanganya na yanakosa kujitosheleza, ima wewe uingilie kati au umuamuru aeleze ukweli zaidi hasa akitueleza kati ya yeye na Magufuli nani anasema ukweli au la na kwanini na ili iweje.
Mheshimiwa Rais, naomba, kwa heshima, taadhima na unyenyekevu nikushauri kuwa uwe makini mradi huu ambao ni wa fedha nyingi na wenye ushawishi mkubwa. Nadhani ni haki ya umma wa watanzania si kujua ukweli tu bali hata maslahi ambayo mradi unayo kwao. Kwani, haya matrilioni yatakayokopwa na kutumiwa na mradi watalipa wao au watoto au wajuu zao. Kimsingi, watalipa watanzania. Hivyo, wanaoingia mikataba ya hovyo wajue wasijue ni kwamba mwisho wa siku watakaolipa ni watanzania hata kama siyo wa sasa. Niseme wazi kuwa una bahati kuwa uhusiki na kuanzishwa kwake. Hivyo, unaweza kukaa pembeni na kufanya uchambuzi wa kina upya kujua pumba na mbegu baina ya mtangulizi wako na hawa aliosema kuwa walikuwa wakifanya lobbying kupitisha mradi wa hovyo ili kuwaibia watanzania.
Mheshimiwa Rais, naomba–––chonde chonde–––ututuoe kizani kwa kutafuta na kuupata ukweli ili ukuweke na kutuweka huru kama taifa badala ya kutuacha na shaka huku wasio na subira wakiona kama mtangulizi wako anasalitiwa na watu wake jambo ambalo halifai hata kulifikiria. Naomba leo nisiseme mengi nikingoja kuona uamuzi na hatua utakazochukua.
Chanzo: Raia Mwema kesho
No comments:
Post a Comment