The Chant of Savant

Wednesday 8 August 2012

Hongera mchunaji Rwakatarehe kwa miujiza ya Tanesco


NASIKIA wewe ni bingwa wa kukwapua umeme kwa miujiza ya Yesu. Kumbe jamaa walikuwa hawakujui? Hawajui ulivyotumia miujiza ya Yesu kuukwaa uheshimiwa ukiachia mbali kuwaingiza mjini manungayembe ukiwaahidi ungewapitia waume wakati nawe ni wale wale?
Huyu Yesu siku akija kitakuwa kizaazaa wallahi kama siyo kuumana! Nakumbuka uliwaliza wengi ukiwaahidi dhahabu wakaishia kupata adhabu na adha ya ulimbukeni na ujuha.
Wewe na midhahabu yako itokanayo na sadaka zao unazidi kutanua tu! Ama kweli wajinga ndio waliwao!
Pia, benki moja pale Tabata nanyi nawapongeza kwa kusaidia kuleta teknolojia ya kuiibia TANESCO maana nao wanawaibia wateja wachovu. Nyie watu wa benki chonde chonde nawaomba msije mkageukia vijisenti vya walalahoi waliowaamini wasijue nanyi ni wale vibaka.
Siku hizi watu wanakwapua kwa jina la Yesu bwana. Haukuwasikia wenzako pale nchi ya Nyayo wanavyowabaka vyangudoa na kuwapa chochote kitu kwenda kutoa ushuhuda kuwa wameona miujiza wakati miujiza yenyewe ni uzinzi na wizi mtupu?
Hata kaya yetu imeona miujiza. Afrika ingawa iko nyuma kiuchumi, inaongoza kwa kutumia umaskini kutengeneza utajiri. Hamjawaona watu, tena matapeli wa kutupwa wakitumia jina la Yesu kutengeneza utajiri wakati yeye alikuwa lofa aliyeshindwa kulipa kodi hadi Mungu akafanya muujiza kumlipia?
Hamuwaoni waheshimiwa sana wanaotumia kura za maskini kutengeneza utajiri wa kunuka kama walivyofichuana juzi mjengoni?
Sasa kama ni hivyo, kwanini Bill Mhando asifanye miujiza pale TANESCO? Bill nakupongeza na bi Eva na wanenu Vero na Fred kwa kuuza gunia la misumari pauni 500,000. Hakuna muujiza mkubwa kama huu.
Hapa bado hujaongelea miujiza ya Bob Mboma kuwa mkiti wa bodi na bado eti anataka makampuni yake yafanye biashara na shirika na asiguswe.
Hamkuwasikia akina Mzitto Kabwela wakihanikiza kuwatetea akina Mhando wasijue kuwa na yao yatafichuka? Nasikia dogo huyu ambaye watu wanamwonea kwamba ana uchu wa urahisi kama fisi ana ukwasi. Sijui kama ni kweli ila Mungu pekee anajua! Kaya yenu si ya wana mazingaombwe bali watenda miujiza hata kama ni ya mashaka.
Kaulize wale jamaa wajiitao NSBT wanavyohadaa watu kuwa mauchumi yamekua. Yakueje muendelee kubomu na kukopa kila uchao? Acheni utapeli wa kijinga ingawa mtajifanya nanyi mnatenda miujiza kama ya baba yenu mzee wa sanaa na miujiza anayeweza kuleta vurugu lakini akiiita amani hata kama ni ya imani.
Hamkusikia miujiza ya mapilato ya kupokea amri toka Ikuu ili kutoa hukumu zenye kuleta malalamiko kila uchao? Waulize matabibu au maticha they’ll tell you all.
Yote hii miujiza na si mazingaombwe kama ya akina Ka-Tortoise, Gamanyua, Lusekela, Gwajimai na matapeli wengine wengi waliotamalaki kwa jina la Yesu.
Haya si mazingaombwe kama ya mashehe Khamis Khariff (yule Mrundi anayejiita Mgoma), Juma Pondaponda (Mkongomani anayejiita Mgoma), Ali Basherehe (Myemeni anayejiita Mbongo) na wengine wengi waliojificha nyuma ya Mtume wakati ni vibaka wa kawaida tu.
Wala haya si mazingaombwe kama yale ya genge la uangusho au gabacholi ajiitaye Juha Ismail Radhi anayejifanya ana uchungu na Zenji wakati mababu zake waliletwa na Muingereza kuihujumu. Hayo tuyaache.
Kwanini nyinyi mjivunge wakati rahisi akiingia madarakani mama anafanya miujiza na kuaanzisha NGO ya kutafuta fweza binafsi? Muulize Salima binti Kinyozi toka kule Mitandi.
Kama mbunge kama mama Askofu Rwakatarehe anaweza kuanzisha NGO ya dini akajenga mishule ya bei mbaya na kuishia kupewa uheshimiwa, kwanini mama TANESCO naye asifanye miujiza hiyo hiyo ya kuunda NGO yake ambayo ni kampuni yake na vitegemezi vyake ili kuwaibia walevi kwa miujiza ya madaraka?
Hivi unadhani kuuza gunia la misumari kwa shilingi 125,000,000 ni mchezo? Ukiwaona wanaendesha midude ya bei mbaya unadhani wajanja kumbe vibaka!
Wao wanakula huku nyinyi mnakula kule ila waliwaji mnawatia matatani jamani. Anyway, nao wana maeneo yao ya kufanyia miujiza. Maana kila ng’ombe anakula kwa urefu wa kamba yake.
Hamkuwasikia waheshimwa wakifanya miujiza kwa kutajana pale walipogundulika kuwa kumbe wanatetea ulaji wao?
Huu nao ni muujiza. Mtu anachaguliwa awawakilishe walevi anawakilisha tumbo lake na hakuna anayemtoa puta wala ngeu! Angalia akina Sonko na Waitish pale Kenya wanavyopambana na polisi kutetea wapiga kura wao sio nyinyi mnaowasaliti wapiga kula wenu.
Hii kweli kaya ya miujiza. Mkuu wa kijiwe anatenda dhambi ya kulala kitanda kimoja na Richimondi. Anamtoa waziri wake mkubwa kafara wakati wote ni mradi wao na kuendelea kupeta huku akifanya miujiza mingi sana kama vile kuitalii dunia na kujilisha pepo, lakini hapewi displini kama waliyopewa akina Kashaffi kule Libia.
Anaweza kutenda miujiza ya kuwaahidi walevi maisha bora tena kwa wote kama alivyofanya Bwana Yesu kuwalisha maelfu kwa samaki wawili, lakini akaishia kuwalisha hewa na wasimsulubu. Wafikiri mchezo? Bila miujiza kaya isingeweza kukalika.
Hebu angalia mtu ananunua unit 200 za umeme, lakini kwa miujiza unakuta mita yake ina unit 200,000! TANESCO hapo mpo?
Jana imeibuka TANESCO ndogo ambayo inafanya kila kitu kama TANESCO halisi kwa bei poa. Hapa bado hujaongelea miujiza ya wachukuaji, sorry wawekezaji ambao wanapewa miaka mitano ya msamaha wa kodi na ikiisha wanabadilisha majina ya biashara zao na kuendelea kupeta.
Wako wapi akina Sheraton? Si wana majina mapya mara Shelaton, Moving pick mara Serena kesho Nesaa mradi miujiza tu.
Sijui kama hawa hawaibi umeme sawa na ile benki ya Tabata. Wako wapi akina Richimondi? Si wanaitwa Dowansi? Wako wapi akina Luwasha si wanaitwa wa Kupinda pinda? Sakarani na firauni wa madaraka utawajua ingawa hawajijui kuwa kuna kesho, tena yenye hukumu.
Kaya yetu kweli ya miujiza! Unashindwa kumwamini na kutomwamini nani. Leo utaambiwa mabaya ya mkurugenzi mkuu wa TANESCO aliyesimamishwa kazi, lakini huambiwi mabaya ya bodi na lisirikali linalokopa umeme miaka nenda miaka rudi!
Hapa bado utasikia waheshimwa wakishutumiana kupewa chochote kitu. Kila mmoja anajifanya anawatetea walevi wakati alishawapiga seli miaka mingi. Kwanini asiwe mkweli na kuwaambia walevi go to hell au kula majani?
Kwanini asiseme kuwa jimbo lake ni tumbo lake na familia yake? Hii nayo ni miujiza maana waliwao wametulia na kuendelea kuliwa tu. Hivi kupe ana faida gani mgongoni mwa ng’ombe? Je, ng’ombe anawahitaji kupe tena awabebe kwa heshima na mbwembwe kama hao?
Acha nijikate kona, nikavute sigara yangu kubwa ili inibangue niweze kupambana na mafisi waheshimwa hawa.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 8, 2012.

No comments: